Pages

Thursday, February 21, 2013

KANISA NA MAFANIKIO Na Bishop Nickodemus Shaboka Jr

Bishop Nickodemus Shaboka Jr

Leo katika Hoja yangu tutakuwa na mtumishi wa Mungu Bishop Nickodemus Shaboka Jr,karibu tujifunze.....
Mafanikio ni jambo ambalo limeshika hatamu katika ubongo wa kila mtanzania leo, awe kanisani au nje ya kanisa, katika kila eneo la maisha watu wanataka, wanapambana na kupigania mafanikio. Tafsiri nyepesi ya neno mafanikio ni kuongezeka au kubadilika kutoka ngazi moja kwenda nyingine au kutoka hali mbaya kwenda nzuri.
Hili ni jambo ambalo kanisa la leo kila upande utasikia semina za mafanikio, maombezi ya mafanikio na mambo kama hayo, na kwa kweli watu wanajitoa kuhudhuria hata kama ni kwa wiki mbili kujifunza namna ya kufanikiwa.Leo nataka tuangalie habari ya mafanikio katika kanisa hasa makanisa ya kipentekoste “kiroho” ambayo kwa karne hii ya 21 ishirini na moja yameonekana kuchukua nafasi zaidi katika jamii yetu.
Miaka ya 90’s kurudi nyuma, haikuwa rahisi kukuta hapa Nchini kanisa la kipentekoste linawashirika zaidi ya 300, lakini leo makanisa ya kiroho hapa hapa Tanzania yana washirika mpaka 10,000 elfu kumi na zaidi. Naweza kusema tumefanikiwa kwa mtazamo wa kuhama hatua moja kwenda nyingine.
Mtu mwnye akili timamu au anayeitwa kakamilika kiakili ni yule ambaye anaangalia alipotoka, alipo na anapoelekea, na ilikujua unakotoka, ni muhimu kujua msingi wako ni upi, ili kuangalia misingi uliosimamia au unaojenga juu yake kwa sasa kama unamizizi sawa na ile uliyoanza nayo au unayopaswa kuendelea nayo.
Msingi wetu kama kanisa ni Kristo, na ndiye tunayejifunza kutoka kwake. Yaani kwa maana rahisi tunatakiwa kupima mafanikio yetu kwa kuangalia tumejenga namna gani au kama kanisa tunaenenda namna gani juu ya kile alichokianzaisha Bwana wetu Yesu Kristo aliye jiwe kuu la pembeni na nguzo ya kanisa.
Kwakuwa Yesu ndiye nguzo yetu, yeye alifanyaje katika huduma yake na sisi tunafanyaje leo? Je tunadumsha kile alichoanzisha au tumegeukia mambo yetu wenyewe? Hicho ndicho kipimo halisi cha mafanikio ya kanisa.
Maana ninaavyoelewa mimi, kanisa ni mwili wa kristo na Yesu ndiye kichwa, hii inamaana kanisa halina matakwa yake lenyewe, bali lipo kutimiza yale anayotaka Yesu juu ya kanisa lake.
Katika huduma ya Yesu kwa miaka mitatu na nusu hapa duniani, ukisoma maandiko, alijihusisha sana na mambo mawili, kwanza alitoa huduma ya Kiroho na pili huduma ya kimwili ambayo ilileta uwiano. Muujiza wa kwanza aliofanya kabla ya muujiza wowote ambao Biblia imerekodi ni ule wa kugeuza maji kuwa divai na kuokoa jahazi katika harusi ya Kana ya Galilaya. (Yohana 2:1-11)
Swali linakuja, je sisi kama kanisa yaani wafuasi wa Yesu, watu wa uamsho, tunauwiano katika huduma? Tunaigusa vipi kimwili jamii inayotuzunguka? Tunasifa gani ya kuhudumia wanajamii?
Mwanafunzi mzuri, au mfuasi aliyefaulu,ni yule ambaye anamtazama mwalimu wake na kuigiza kila kitu anachokifanya mwalimu wake. Sisi kama kanisa tunafanya yote aliyofanya Bwana wetu Yesu?
Tukiangalia wenzetu wa upande wa pili, kila wanapojenga nyumba ya ibada kwa asilimia kubwa wanatoa na huduma za maji aidha ya kisima au ya bomba kwa jamii inayowazunguka. Sisi makanisa yetu yanafanya nini mbali kuongeza maspika kuwapigia makelele ya nyimbo wanajamii?
Sikatai kwamba tunaihudumia jamii kiroho kwa kutoa mapepo na kuwafungua vifungo mbali mbali, lakini hata Yakobo anasema imani bila matendo imekufa. Yesu aliwahubiria na kuwapa mikate ili waendelee kumsikiliza.
Mkazo tulio nao katika kukusanya pesa za sadaka, fungu la kumi na michango mbali mbali, kwanini tusiutumie pia kuangalia tunaigusa vipi kimwili jamii inayotuzunguka? Badala ya kutumia milioni nne kuandaa mkutano wa nje “Crusade” tutumie pesa hiyo kukodisha hata magari ya maji safi tukanywesha bure maeneo yasiyo na maji, huku tukitumia fursa hiyo kuwahubiria injili. Je hatutafaulu?
Ni jambo lisilopingika kwamba ulimwengu umebadilika, hata Tanzania imeingia kwenye mfumo wa digitali, mbona kanisa bado limeng’ang’ania mifumo ya analogia. Mimi naamini kuwa Mungu ndio “up to date” wakisasa kuliko hata wanadamu.
Ndio maana anamwambia Musa “Nami nilijulikana kwa Ibrahimu na Isaka, na Yakobo kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu Yehova, sikujulikana kwao.”(Kutoka 6:2-3) Kama Mungu wetu anavipindi vya mabadiliko, iweje sisi tubaki pale pale tulipokuwa miaka nenda rudi.
Hebu tuamke kama kanisa, Yesu ametuambia,” Mtu akinipenda atazishika amri zangu” basi na tushike amri zake kwa kufanya alichokifanya kiongozi wetu. Japo hata mara moja kwa mwaka basi kwenye karenda ya makanisa yetu ya kiroho, badala ya kuweka mikutano mitatu ya nje, tuweke angalau siku ya huduma kwa jamii.
Tukifikia mahali pa kuweka uwiano kati ya huduma za kiroho na kimwili, hapo tunaweza kusema tumefanikiwa. Wenzetu ngozi nyeupe walipotuletea injili, walifanikiwa kirahisi kwani waligusa huduma kwa jamii pia. Imani pasipo matendo imekufa.
Wamisionari wengi, ndio waliojenga mashule, vyuo mbali mbali, zahanati hadi hospitali kuu, na makanisa, na huo ndio msingi wa Ukristo. Lazima tutofautiane na wanasiasa. Hata wahenga walisema “Maneno matupu, hayavunji mfupa.”

Kwa maoni na ushauri tuma bishopshaboka@gmail.com au 0784 310 587.

 

2 comments:

  1. Bwana Yesu apewe sifa,

    Mtumishi Mungu akubariki kwa kutukumbusha majukumu yetu kama Wakristo na kama kanisa. Ni kweli yatupasa tutazame yale Kiongozi wetu Yesu Kristo alitenda nasi tutende na zaidi ya yale. Kwa njia hiyo, injili ikihubiriwa itapokelewa kwa urahisi zaidi, na Mungu atusaidie.

    In faith of the Lord Jesus Christ, Martha Macha Msale

    ReplyDelete
  2. Amina mtumishi Martha,ni kweli kabisa Kama Kanisa la Kiristo tumekumbushwa wajibu wetu katika makala haya

    ReplyDelete