Pages

Tuesday, May 21, 2013

Maombi Ya Ulinzi – Sehemu Ya Tatu na Mchungaji Florian Katunzi


Jenga Madhabahu Ya Mungu Aliye Hai

*Kutoka 8:22-23

“ Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni watu wangu wanayokaa ili hao mainzi wasiwe huko, ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi Bwana kati ya dunia name nitatia mpaka kati ya watu  wangu na watu wako, ishara hiyo italetwa kesho.”

-Nitatenga nchi, Nitaweka mipaka. Wakati misri wanapitia mapigo mazito  Bwana aliweka mipaka kati ya eneo la Gosheni walikokaa  Israel, eneo hilo likatengwa likawa na ulinzi wa Mungu.

-Unaposimama juu ya madhabahu ya Mungu aliye hai ndani ya nchi, Bwana anasema walikuwepo watu wanaomba na kumtumikia katika hali ya unyenyekevu, Bwana atashuka mahali hapa tuombapo na kuitenga nchi yetu na maangamizi.Tunapojenga  madhabahu ya Mungu aliyehai ndani ya nchi , tunasimama mahali hapa na kuomba Mungu aliye hai, anashuka na kuponya nchi yetu.
*2Mambo ya nyakati 7:15

“Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.”
*2Mambo ya Nyakati 7:13-14

“Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzinge kula nchi au nikiwapelekea watu wangu tauni, ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekesha  na kuomba na kutafuta uso , na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka  mbinguni  na kuwasamehe dhambi yao na kuiponya  nchi yao”.


-Lazima nchi yetu  iponywe na magonjwa , lazima tuombe nchi yetu iponywe na umasikini, lazima tuombe Mungu nchi yetu iponywe na magonjwa mazito.Tuombe Mungu alete uzima na uhai juu ya nchi yetu, Tanzania yetu lazima iwe na uzima, lazima tuombe na kuamuru ustawi na kukua kwa uchumi wetu, hii ndiyo madhabahu ya Mungu aliye hai. Bwana aweke mipaka sasa kati ya Ukimwi na watanzania, tuombe Bwana Mungu aweke mipaka kati ya umaskini na maisha yetu.Madhabahuni pa Bwana  huleta mageuzi kwa wote wanaokimbilia pale.

-Hakikisha familia yako, mali zako, wewe mwenyewe na watoto wako mnakuwa mmeungamanishwa katika madhabahu ya Mungu aliye hai kupitia damu ya ukombozi ya mwana kondoo wa Mungu YESU KRISTO MKOMBOZI.

-Bwana anakwenda kufanya mageuzi katika nchi yetu , mageuzi ya kiroho na kiuchumi.

*Ayubu 42:10

“Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu”

-Bwana  ninaomba kikamilifu kwa moyo wa dhati, ushuke na kufanya mageuzi katika nchi. Leo sasa tunapoomba mbele ya Mungu mwenye nguvu, tuombe Bwana afanye mageuzi , badala ya vita atupe amani, badala ya magonjwa atupe afya njema, badala ya umaskini atupe heshima, badala ya vifungo atupe uhuru, badala ya laana atupe Baraka.

*Yeremia 31:13-14

“Maana nitageuza masikitiko yao  kuwa furaha, nami nitawafariji na kuwafurahisha  waache huzuni zao, name nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema Bwana.”

No comments:

Post a Comment