Pages

Friday, July 12, 2013

Vitu muhimu vya kuangalia au kufanya unapojiandaa kuwa na mwenzi wa maisha------SEHEMU YA 8


 
Bwana Yesu asifiwe wapendwa,leo tunaendelea na Somo letu la Vitu muhimu vya kuangalia au kufanya unapojiandaa kuwa na mwenzi wako wa maisha.

Nitazungumzia jambo muhimu sana ambalo watarajiwa wote wawili yaani mwanamke na mwanaume inabidi kujifunza na kuliombea ili mnapokuja kuishi pamoja muwe na ndoa yenye Amani na inayomtukuza Mungu. Jambo lenyewewe ni;

Hasira – Mjipange kuizuia isije ikawaharibia mahusiano ya sasa au ya mbele.

Hasira kwa kifupi ni hali ya mtu kujisikia vibaya,au kuchukia na kuwa na msukumo mkali unaomfanya mtu afanye kitu ambacho hakutegemea kukifanya mara nyingine.

Kwa miaka mingi ambayo Mungu amenipa hapa duniani,nimekuwa katika familia yetu,familia zingine,makanisa mbalimbali,mashule,vyuo,maofisi mbalimbali sijawahi kuona mtu ambaye hana HASIRA.

Kwa hiyo nataka nikuambie kwamba kila mtu ana hasira ila tu tofauti tu ni jinsi watu wanavyoweza kuikabili. Hasira inaweza kuwa mbaya au nzuri au mbaya.

Ninaposema nzuri ni kwamba kuna ile hasira ya kuchukia vitu vibaya au dhambi hiyo ni nzuri.

Hebu tuangalie neno la Mungu linaloonyesha ni hasira ambayo iko chanya (positive) ,fungua na mimi Zaburi 7: 11 “Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku”

Katika neno la Mungu hapo juu tunaona kwamba Mungu naye anachukizwa lakini anachukizwa na dhambi.

 Pia Kutoka 11: 4-8 tunaona jinsi ambavyo Musa alikuwa na hasira juu ya matendo mabaya ya Farao twende tuone Maneno ya Mungu yanavyosema;

“4 Musa akasema, Bwana asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri;

5 na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama.

6 Ndipo kutakuwa na kilio kikuu katika nchi yote ya Misri, ambacho mfano wake haujakuwa bado majira yo yote, wala hautakuwako mfano wake tena kabisa.

7 Lakini katika wana wa Israeli hapana hata mbwa atakayetoa ulimi juu yao, juu ya mtu wala juu ya mnyama; ili kwamba mpate kujua jinsi Bwana anavyowatenga Wamisri na Waisraeli.

8 Tena hao watumishi wako wote watanitelemkia kwangu mimi, nao watanisujudia, wakisema”

Sasa Hasira ninayotaka kuzungumzia hapa kwa msisitizo sio hii ya kuchukia mabaya ni ile ambayo inakusababisha ukafanya au ukasema Maneno mabaya au makali na kuleta madhara kwa muhusika.

Neno la Mungu katika Yakobo 1:20 “Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki”, Kama neno linavyosema ni vizuri watarajiwa ambao mnapanga kufunga ndoa mkaanza kujifunza na kuomba msiwe na Hasira ambayo itaaribu uhusiano na Mungu na wa kwenu nyinyi wenyewe mtakapokuja kuishi pamoja.

Hili litawezekana kama mtakuwa wawazi kwa kila mmoja wenu na kupeana mrudisho nyuma mnavyokuwa katika hatua zote za maisha yenu,kuanzia uchumba hadi kwenye ndoa.

Mkiwa wawazi na kuishi maisha halisi kwa kila mmoja inasaidia kutoweka vitu na kusameheana kwa haraka, lakini kama hakutakuwa na uwazi mwenzako hatajua umekwazika na nini kwa hiyo ni rahisi akafanya kitu kikakukwaza na kuumiza, hapo ndipo hasira inakuja kwako unaweza kutumia Maneno makali au matendo kwasababu moyo wako unawaka moto umejaza vitu vingi hujasamehe,wenzetu wanasema una blow –out ni mbaya sana yaani unalipuka.

Nakumbuka kuna kipindi nilikuwa napenda kusema nitakulipukia kama Sodium, kwa wale mliosoma Chemistry mtaelewa mlipuko wa Sodium ulivyo ni mkubwa haswaa. Nilipoendelea kujifunza neno la Mungu nikagundua kwanza mdomo wangu na Maneno ya kinywa change yana nguvu ya mustkabali wangu maana neno linasema katika Mithali 18: 21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.” Hili neno lilinifundisha sana sana nikaacha hayo maneno na kukataa kabisa maana neno linakufanya uwe kama unavyosema,kama na wewe una kitu unasema cha tofauti badili kwanza. Nilisoma pia katika kitabu cha Think Big Dr Ben anaelezea pia kusoma Mithali kulimsaidia sana kuwa mbali na hasira mbaya.


Ushauri wangu kama una hasira fanya yafuatayo;

1.         Muombe Mungu akuondolee hasira mbaya

2.         Ongea na mwenzako akusaidie pale anapoona una tabia ya hasira akupe mrudisho nyuma,kukushauri na kukuombea 

3.         Soma sana neno la Mungu fanya kama project ya kusoma Neno, anza na Mithali kwanza ina mistari mingi

4.         Pata muda wa kutulia unapokuwa umekwazika bora unyamaze kwanza baadae utafute suluhisho

5.         Kama unajijua unaweza kushikwa na hasira za haraka jihadhari na watu wenye hasira mbaya wanaweza kukufanya ufanye jambo la hasira,ukae nao kwa akili

6.         Kama hasira yako ni ile ya kuvunja na kurusha vitu na umeokoka au kupiga, nakushauri ongea na Mchungaji wako au wanamaombi wa kanisani kwako wakuombee maana hicho ni kifungo

7.         Chukua hatua na kuchukia hasira mbaya, ukiichukia utajifunza kujizuia kimenisaidia kiasi hiki

8.         Kuna rafiki yangu alinishudia alikuwaga na hasira sana sana, alianza kujifunza kuwa mtu wa mzaha mzaha tu kutochukulia vitu anavyofanyiwa serious ili msaidia kurejesha mahusiano na kuepusha magomvi. Ni njia nzuri pia hii unaweza kuifanya

Najua umepata Dozi nzuri sanaaa leo, na tumenufaika woote maana hata hapa najifunza na mimi

Namshukuru sana Roho  Mtakatifu anavyoendelea kunitumia katika Somo hili najua kuna mahusiano yanaponywa, Na utukufu ni Kwako ewe Bwana Yesu.

 

Tutaendelea…..

 

 

 

 

1 comment:

  1. Amen, This is so true not only to those who want to get married but even those who are already in the marriage. May the Lord bless you so much and use you more and more for His only glory!!

    ReplyDelete