Pages

Friday, January 3, 2014

JIFUNZE JINSI YA KUMUONA MUNGU AKIJIDHIHIRISHA KWAKO by Frank Phillip

Mtumishi Frank Philip
Heri ya Mwaka mpya 2014 mpendwa mtu wa Mungu, karibu katika makala haya yanayoletwa kwenu na Mtumishi wa Mungu Frank Phillip.
Karibu......

 Mara nyingi sana tumeona watu wanatamani kumwona Mungu akijidhihirisha katika maisha yao, hata ikiwezekana kwa ngurumo na matetemeko, ila kila mahali ni kimya kama Mungu hayupo. Nataka nikupe SIRI moja kati ya nyingi ambazo zinaweza kukusaidia.

Umewahi kujiuliza nini kinatokea wakati Mungu anatafuta watu wa kujidhihirisha kuwa mwenye NGUVU haw...aoni! na upande mwingine watu wanatafuta UDHIIRISHO wa Mungu kwenye maisha/huduma zao hawaoni kitu pia? Tunafahamu kwamba “Kwa maana macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita.” (Mambo ya Nyakati 16: 9)



Kwa upande mwingine kila mtu anajua na kukiri kwamba Mungu yuko karibu sana kuliko hata pumzi yake, nk. lakini kwa kweli anasema tu huku hata akiomba inakuwa kama Mungu yuko ng’ambo ya bahari au Mbingu imepauliwa kwa zege. Hata inafika watu wa Mungu wanaamua “kuteremkia Misri” (kufuata njia za kidunia kama rushwa, nk.) ili kupata msaada, kwanini? Wanaona Mungu yuko mbali na wanaona kila kitu mbele yao ni milima na bahari tu na hawawezi kuvuka hapo. Ghafla! Wanaanza kujirahisisha na kufanya dhambi kama vile Mungu hayupo. Huku tunaambiwa Mungu ni SHAHIDI mwepesi! Sasa mbona inakua NGUMU kujidhihirisha na matendo yake MAKUU akitutetea kama ni shahidi MWEPESI? “Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi.” (Malaki 3: 5)

Sikiliza kwa makini, Mungu sio mwanadamu, Yeye anaona “NIA iliyoko ndani yetu”. Weka moyo wako vizuri juu ya mambo uombayo ama sivyo hupati kitu. “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” (Yakobo 4:1-3)

Sasa utakuta wana wa Mungu wamefika mahali wamejichanganya sana. Nusu kwa Mungu nusu mtaani/kwa Ibilisi. Halafu unatarajia udhihirisho wa Mungu kwa radi na matetemeko. Utakuta mtu anakiri ushindi pale tu anapotaka KITU kwa Mungu ila akijaribiwa KUTENDA dhambi anakua mpole wala hafungui kinywa! Hadi anazini, kula rushwa, kusema uongo, nk. halafu baadae anatubu! Ule “UKAMILIFU wa UELEKEVU wa Moyo” (Nyakti 16:9) kama wa Ayubu wakati wa majaribu uko wapi? Kama moyo wako ni MWELEKEVU kwa UKAMILIFU (soma hapo juu kifungu cha pili), wakati macho ya Bwana yanakimbia-kimbia duniani KUSAKA watu wa kujidhihirisha mwenye NGUVU, lazima yataku NASA tu na Mungu anaanza kuwa shahidi mwepesi kwako ghafla! Ila kama bado nusu moyo umeweka kwa boyfriend/girlfriend na mnafanya uchafu au ku-chart dirty stories, au upande mmoja rushwa, dhuluma, na upande mwingine Mungu, hapo sahau kuona UDHIHIRISHO wa Mungu. Utaomba na mbigu itakuwa kama chuma juu yako, utasikia kama mkiwa jangwani kwa maana Roho Mtakatifu ni Mtakatifu kweli, usitarajie umburute kama silaha tu ya kushambulia wakati UNASHIDA halafu unaishi maisha ya KUMHUZUNISHA na KUMZIMISHA. Mungu ATAWAONA na atajionyesha mwenye NGUVU sio kwa kila mtu ila “waliokamilika moyo kuelekea kwake”, na jicho lake liko busy kutafuta, kwa kukimbia-kimbia duniani kote kumsaka huyu mtu. Kwanini Mungu anafanya msako? Kwasababu hawa watu ni ADIMU!

Watu wengi wamekuwa ADUI wa Mungu bila kujijua huku wanamwita Baba! Haiwezekani unafanya urafiki na DUNIA na mambo yake halafu unatarajia Mungu ni baba yako! Ndio maana “Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (Yohana 8:41-43).

Sasa chunga njia zako vizuri. Sisemi kila mdhaifu katika dhambi ni mtoto wa Ibilisi, tunajua kuna habari ya “Mwana lakini ni mpotevu”. Ameenda huko duniani kuishi kwa maisha ya anasa ya UZINZI lakini ni “mwana”. Tunajua habari ya Yesu kwamba kuna “kondoo” mmoja mahali nje ya zizi, amepotea, na Yesu yuko tayari kuacha hawa 99 ili AKAMSAKE huyu mmoja! Sasa nakupa shauri, kimbilia kwa Yesu haraka, kama wewe ni kondoo na unajua uko nje ya zizi au kama ni mwana mpotevu uko huko duniani, rudi kwa Baba. Weka moyo wako vizuri KUMWELEKEA yeye peke yake kwa UTIMILIFU utaona MACHO ya Mungu yakikutembelea kwa maana yanakutafuta siku nyingi na hayakuoni, na utashuhudia NGUVU zake maishani mwako kwa maana HAKIKA atajidhihirisha kwako.

Neema na Baraka zitokazo juu ziwajaze mnapozidi kuyatafakari na kuyatenda mapenzi ya Mungu. AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment