Pages

Tuesday, July 15, 2014

TAMBUA BARAKA ZINAZOKUJIA ZINATOKA WAPI na Mwalimu Samwel Mkumbo

Bwana Yesu asifiwe mpendwa karibu sana katika makala haya yanayoletwa kwenu na Mwalimu Samwel Mkumbo.

Mwalimu Samwel Mkumbo
Hakika Baraka ni jambo mojawapo la msingi sana kwa  watoto wa Mungu na ni jambo la Faraja tuonapo mwana wa Mungu akifanikiwa katika mambo yake yote. Kama inenwavyo;

..,….Mzee, kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli. Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo…,… (3Yoh 1:1-2)

Sasa basi ni vema ukafahamu  ya kuwa kubarikiwa ni jambo la msingi sana na tena ni moja ya ushuhuda kwa watoto wa Mungu. Lakini pia Baraka ni kutukuka sana katika Ukuu wa Mungu na pia juu ya haya yote tunaweza kuona ni kwa jinsi gani uweza  wa Mungu unajidhihirisha katika mambo yetu ya mwilini naam katika kutuma mema katika Tumaini jipya la imani yetu.

Lakini pia Biblia inatupa maelezo kadhaa juu ya kupata Baraka au mafanikio maana si kila mafanikio (Baraka) zina mkono wa Mungu ndani yake, au ni utukufu wa Mungu mingine ni mitego ya shetani katika kutuangusha katika imani yetu katika KRISTO YESU, naam! Maandiko matakatifu yanatupa mifano kadhaa ya Baraka zitokazo kwa Mungu na zile zinazoletwa na mwovu kama mtego kwetu.

Vielelezo!!

-Habari za Elisha na Naamani.

2 Wafalme 5:1-14 tunaona kisa kizuri na cha kutufundisha juu ya Baraka.

Nabii Elisha alipata nafasi ya kufanya muujiza wa uponyaji kwa Naamani (Yule jemadari wa Shamu) juu ya ukoma wake, na baada ya muujiza huo, mtu huyo, huyo Naamani alitaka kumpa zawadi Elisha, lakini Elisha hakukubali,. 2 Wafalme 5: 15-16 inasema;

Akamrudia Yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa  tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee, lakini akakataa.

Katika maandiko hayo utaona ya kuwa Elisha hakupokea Baraka kutoka kwa Yule Jemadari naam, huyo  Naamani, lakini ni vema tukafahamu ya kuwa si kwa sababu Elisha alikuwa na tabia ya kutopokea zawadi na Mbaraka kutoka kwa watu aliowahudumia, la hasha! Bali ipo sababu nyingine, maana  ni Elisha huyu huyu alipokea msaada kutoka kwa mama Mshunami! Tazama hapa;  2Wafalme 4:8

Kwa hiyo si kila tunuku unayopewa ni ya kukubali lakini pia si zote ni za kukataa maana kila jambo lina maana yake na matokeo yake ambayo kwa hayo twaweza kutambua kusudi na mapenzi ya Mungu kwetu lakini pia hila na mitego ya shetani.


-Mfano wa Yesu.


Moja ya mifano tunayoweza kupata kuhusu habari ya Baraka au kutunzwa ni kuhusu habari za Yesu mwenyewe. Luka 4:5-7 imeandikwa hivi;

Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.

Katika mistari hiyo unaweza kuona mfano wa Baraka ambazo huja kwetu kama mtego, maana katika kutazama hayo waweza kuona namna ambavyo shetani aweza kufanya aina flani ya mafanikio kwetu na huja kwa mtindo wa kututamanisha sana hata kutuvuta karibu nazo  lakini kumbe ni njia ya upotevu.

NAMNA YA KUTAZAMA BARAKA/MAFANIKIO YANAYOKUJIA YANATOKA WAPI.

Katika nafasi hii tupate kujua japo kidogo namna ya kutazama Baraka na mafanikio yetu na yanayotujia kuwa yanatoka wapi ili iwe ni nafasi nzuri kwetu kujua ni kwa jinsi gani tutamtukuza Mungu kwa anavyotuwezesha au ni kwa jinsi gani tunaweza kukwepa mishale ya mwovu anayoturushia kwakutumia kifuniko cha Baraka au mafanikio.

Ø  Lengo la Anayetoa.

Kutambua lengo la anayetoa sadaka ni njia mojawapo ya kujua ni chanzo gani hizo Baraka au mafanikio yanabubujika, maana kila sadaka au kitu unachopokea au anachokupatia mtu kina lengo lake, kwa hiyo kutazama nini lengo ni njia mojawapo inayoweza kusaidia.

Vielelezo.

·         Kuhusu Yesu.

Ukitazama vizuri habari za Yesu hapo juu unaweza  kugundua nini lilikuwa lengo la shetani kutaka kumtunuku mtu au kutoa kitu, tazama alivyomwambia Yesu;

…….. Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu,……..,,. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako..,...(Luka 4:5-7). Sasa unaweza kugundua kuwa si kwamba Yesu hakuhitaji hizo fahari ila nini lengo la shetani kumpa,.. tazama tena alivyosema; …….. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako..,..

Maana Yesu alikuwa ni muhitaji wa mambo ya mwilini pia yaani chakula, mavazi na malazi, ndio! Alihitaji hayo pia na kuna watu  walimhudumia katika hayo na hakukataa, maana imeandikwa hivi katika Injili ya Luka;

Na wanawake kadhaa wa kadhaa ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa;……..na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.(Luka 8:2)

Yesu hakukataa kwa wanawake na watu hao kumhudumia kwa mali zao lakini alikataa kupewa Milki na fahari ya Ulimwengu na shetani (kwa kumsujudia), nini sababu? Bila shaka ni LENGO!!


Tutaendelea wiki ijayo na vipengele vilivyobakia vya namna ya kuangalia Baraka zinazokujia zinatoka wapi

Karibu sana

No comments:

Post a Comment