Pages

Wednesday, November 12, 2014

JIANDAE KURUDI NYUMBANI Sehemu ya Kwanza na Mwalimu Samwel Mkumbo


Karibu katika mafundisho haya yanayoletwa kwenu na Mwalimu Samwel Mkumbo

Mwalimu Samwel Mkumbo
Utangulizi:
 
Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao. (Waebrania 13:14)

Mtu huweza kutoka asubuhi kwenda katika shughuli mbalimbali wengine huenda mashambani wengine maofisini na wengine kwenye shughuli za aina nyingine, biashara lakini ifikapo jioni au usiku HURUDI NYUMBANI, inawezekana kama ni watoto au ni wazazi waliachana asubuhi wengine wakienda kazini wengine shuleni lakini jioni WATARUDI NYUMBANI.

Mtu anapotoka mji mmoja na kwenda mji mwingine kwa ajili ya kuishi huko aidha kwa sababu za kikazi au hata biashara, akafanikiwa na akaanzisha maisha huko akawa na familia huko na akajenga na makazi yake huko, lakini siku akifariki mara nyingi wengi HURUDISHWA kuzikwa NYUMBANI.

Katika kitabu hiki ambacho kitakusaidia kukueleza mambo kadhaa juu ya wokovu ulioupokea katika maisha yako, utajifunza mambo mengi na ni maombi yetu ya kwamba kitabu hiki kiwe msaada mkubwa sana kwako.

Mambo utakayojifunza:

Sura ya Kwanza: katika sura ya kwanza utajifunza namna ambavyo dunia hii si mahali pa kupategemea na ya kwamba si mahali pa kudumu, na pia utajua kama dunia si mahali pa kupategemea je hatma yako ni nini, na ni nini mwisho wa maisha yako.

Sura ya Pili: itakusaidia kujua ni nini unachotakiwa kufanya kama dunia si mahali pa kudumu ili uweze kufika unakotakiwa kwenda, utajifunza kuwa unahitaji sana maandalizi ya kuelekea mahali unapotakiwa kwenda.

Sura ya Tatu: mambo ya msingi ikiwa ni mwendelezo wa sura ya pili ni kujua ya kwamba unakokwenda hutakiwi kwenda mikono mitupu, kuna mambo unayotakiwa kuyabeba, hivyo kwanza utajikuta kuna maswali unatakiwa kuyajibu ya ulichobeba kwanza na kisha utajua ni nini unatakiwa kubeba.

Sura ya Nne: sura hii itakuelekeza mambo ambayo ni muhimu uyafahamu katika safari hii, mambo yatakayotokea njiani, mambo ambayo yanapotokea usishangae, lakini pia utapata tumaini kwa kujua ya kwamba hauko peke yako.

Nimalizie utangulizi huu kwa kusema JIANDAE KURUDI NYUMBANI.

Sura ya kwanza.

DUNIANI SIO KWETU

Nataka niweke wazo hili kwanza kwako wakati unaendelea kusoma sehemu hii, ni kwamba DUNIANI SIYO KWETU, ndio! Namaanisha hata wewe hapo ulipo, Duniani siyo Kwako, haijalishi umeweka nini duniani, au unaipendaje dunia, au dunia inakupendaje. Si kitu unawapendaje watu wa dunia na vitu vya dunia lakini nataka ujue, na siyo utani kabisa kwamba hapa DUNIANI SIYO KWETU.

Waebrania 13:13-14 imeandikwa hivi;

13 Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake. 14 Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.


Kwa mujibu wa mistari hiyo hapo juu, unaweza kuona mambo ambayo yanaweza kutupa msisitizo wa kuelewa nini ninachomaanisha ninaposema ya kwamba hapa duniani siyo kwetu, na maandiko yanathibitisha hilo, kuna watu huwa wanaamini baada ya kuhukumiwa kwa ulimwengu, Shetani na wenye dhambi basi dunia hii ilivyo vivi hivi tutakuja Kuirithi wale walioamini na kukaa milele na milele, Hapana! Si dunia hii, kabisa, si dunia hii, ambayo tutairithi, dunia hii si kwetu.

Katika mistari hiyo ya Waebrania 13:13-14 kuna maneno nataka tuyatazame kwa jicho la kutuonesha kuwa Duniani siyo kwetu, mstari wa 13 kuna maneno haya… Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi,…. Hiyo inatupa mwanga kwamba kuna Hatua za kusogea au kutembea kuelekea upande fulani au mahali Fulani kutoka hapo ulipo.Halafu katika mstari wa 14 kuna maneno haya…… Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao…… ikiwa inatupa sasa hoja ya msingi kabisa ninayokuandikia katika sehemu hii, anaposema “Maana hapa (Duniani) hatuna mji udumuo”. Hiyo inatuonyesha hata kama kuna mambo gani umewekeza au unayatumainia hapa duniani hayatabadilisha maana kwamba hapa duniani siyo kwetu.

Hebu tuunganishe hiyo mistari ya hapo huu katika sehemu zake ili nikufundishe jambo, tunapounganisha mstari huo wa 13 na 14 kwenye sehemu tunapata maneno haya………”13 Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi………14 Maana hapa hatuna mji udumuo,……”

Sasa unaweza kuona maana tunayoipata katika mistari hiyo hapo juu ya kwamba….TUTOKE TUMWENDEE NJE YA KAMBI (Dunia)………MAANA HAPA HATUNA MJI UDUMUO……….

Katika sehemu ya pili ya mstari wa 14 tunapata maneno haya, “….. bali twautafuta ule ujao.”, sehemu hii inatupa uhakika kuwa Duniani sio kwetu; na hivyo tunapata mtiririko mzuri sana katika maneno hayo ambao tunaweza kuuweka hivi;

Kwa maana……TUNAHITAJIKA KUTOKA…………..

Kwanini……….HAPA HATUNA MJI UDUMUO………..

Bali/Lakini………TWAUTAFUTA ULE UJAO……………….

Hivyo basi kwa maana hiyo inatupa uhakika wa kujua ya kwamba hapa duniani siyo kwetu na ya kwamba katika uhalisia mwanadamu awaye yote katika vyote na yote hawezi kuishi hapa duniani milele, kuna

wakati wakati wa kurudi alikotoka na atahitaji kuwa na uhakika wa mahali anapokwenda, ndiyo maana KUOKOKA NI MUHIMU SANA maana unakuwa na uhakika wa mahali unapokwenda, ndio!, UKIOKOKA UNAKUWA NA UHAKIKA WA MAHALI UNAPOKWENDA, hivyo basi Hongera sana kwa wewe uliyeamua Kuokoka maana tangu sasa unapata uhakika wa mahali uendapo.

Mhubiri 12: 7 inasema imeandikwa hivi;

Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.

Mstari huu unathibitisha kile ninachokuambia kuwa “Duniani sio Kwetu” ambapo pia kimeandikwa katika kitabu cha Waebrania ya kwamba hapa “hapa hatuna mji Udumuo bali twautafuta ule ujao” na Suleimani mwana wa Daudi katika kitabu cha Mhubiri anasema “Mavumbi (Mwili wako) huirudia nchi, nayo roho (yaani Wewe) humrudia Mungu aliyeitoa”

Twautafuta Ule

“Ujao”

Tuliposoma Waebrania 13:13-14, katika ule mstari wa 14 tulipata maneno haya “………….bali twautafuta ule ujao”, nami natiwa Nguvu kusema nawe mtu uliyeokoka ya kwamba pamoja “Duniani siyo kwetu”, na ya kuwa “Hapa hatuna mji Udumuo” lakini kitendo cha kukubali KUOKOKA na kumpa Yesu maisha yako kama kiongozi na “Mfalme” wako basi wewe umeanza safari ya “KUUTAFUTA ULE (MJI) UJAO”, naam!, nan i safari muhimu sana katika maisha yako na inahitaji maandalizi ya muhimu maana UNARUDI NYUMBANI ambapo Yesu alikwenda kukuandalia “Makao” na huko kwenye hayo makao yako ambayo Yesu anakuandalia ndiko “Nyumbani Kwetu”.

2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari,……. (Ufunuo 21:2), mstari huu unatupa tumaini ya kwamba upo mji mwingine unaondaliwa kwa ajili ya watu waliookoka, naam!, kwa ajili yako, pale tu ulipoamua Kuokoka basi nawe unayo nafasi ya kuwepo katika mji huu unaondaliwa kwa ajili ya wale waliompokea Bwana Yesu kama mwokozi wa maisha yao na kuomba msaada na kujitoa maisha yao yawe yenye hofu ya Mungu kila siku na kila wakati.

Lakini kabla hujafika katika mstari huo wa 2 katika kitabu cha Ufunuo 21, upo mstari unaotangulia ambao unasema hivi; “1Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita,…………..”. (Ufunuo 21:1)

Nilitaka utazame maneno haya…… Mbingu MPYA na Nchi MPYA……………halafu maneno yanayofuata yanasema………. kwa maana Mbingu za KWANZA na Nchi ya KWANZA zimekwisha kupita………… sasa unaweza kuona zaidi jinsi maneno haya yanavyothibitisha kwamba “DUNIANI SIO KWETU”, naam maana kuna “Mbingu Mpya na Nchi Mpya” na hizi zinakuja kwa kuwa “Mbingu za Kwanza na Nchi ya Kwanza zimekwisha Kupita”

Nchi ya kwanza na miji hii itakwenda wapi?

2 Petro3:7 inasema hivi;

Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

Umeona? Labda soma tena huo mstari, imeandikwa hivi…..”LAKINI MBINGU ZA SASA NA NCHI ZIMEWEKWA AKIBA KWA MOTO, KWA NENO LILO HILO, ZIKILINDWA HATA SIKU YA HUKUMU, NA YA KUANGAMIA KWAO WANADAMU WASIOMCHA MUNGU”, hivyo ndivyo imeandikwa, hivyo basi uzidi kuwa na uhakika zaidi na zaidi kuwa ‘Duniani sio Kwetu”.

Naam! Na hii ndio inatupa maana halisi ya Ufunuo 21:1 ambapo imeandikwa ………. kwa maana Mbingu za KWANZA na Nchi ya KWANZA zimekwisha kupita…………, kumbe basi kila kilichopo sasa, unachokiona ni “Akiba kwa ajili ya Moto”, naam!, Masoko, Viwanja vya Ndege, Bandai, Magari, Majengo ya Thamani na kila ukijuacho kwa jina na kila kitega uchumi ambacho kinategemewa na mwanadamu na kila kisichotegemewa au kisichokubalika vyote ni kwa ajili ya moto, oooh!, ni jinsi gani inashangaza. Maana cha ajabu hadi wanadamu ambao HAWAJAOKOKA au ambao HAWATAOKOKA nao ni “Akiba kwa ajili ya Moto”.

Naam, KWA AJILI YA MOTO……………………..
 
Tutaendelea wiki ijayo, Karibu sana Rejoice and Rejoice blog

No comments:

Post a Comment