Pages

Tuesday, December 6, 2016

ELANDRE - MSANII WA WIKI

LEO TUNAYE ELANDRE NA GOSPEL HIP-HOP


Leo katika Msanii wa Wiki tuko wa Gospel Hip Hop ajulikanae kwa jina la ELANDRE. Ni muziki wa aina ya kipekee sana kwenye tasnia ya Muziki wa Injili

Tayari kuna baadhi wanamfahamu kwa kazi zake na wengine hata wamehudumu naye pamoja katika huduma mbalimbali.

Tumebahatika kupata nafasi ya kumfahamu zaidi leo na kujua zaidi kuhusu huduma yake ya Muziki wa Injili kwa namna ya kipekee na pia kuhusu maisha yake binafsi.

Rejoice Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Elandre: Majina yangu kamili ni Emmanuel Andrew Mkumbwa. Kwenye mziki ndo natumia jina Elandre.

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Elandre: Nimeokoka. Na ninaabudu katika kanisa liitwalo Bread of Life ambalo lipo chini ya King’s Touch Ministries. Mchungaji wangu anaitwa Fred Okello, na pia ninahudumu pale kama kiongozi msaidizi wa sifa [kusifu na kuabudu].

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, ulianzaje na wapi ulianzia?

Elandre: Nikiwa kidato cha tano, tulikua na kikundi cha maombi ambapo tulikua tukishiriki kila Jumamosi. Kuna siku mtumishi kutoka Uganda akaja akaibua vipawa vilivyokua vimelala ndani yetu kwa neno la unabii. Haikuchukua mda nikaanza kuandika mashairi, maana alitoa mfano hai kabisa wa hiki kipaji/kipawa na nlikua nakipenda sana kitabu cha Zaburi. Ndipo nilipoitolea wimbo wangu wa kwanza uitwayo Praise The Lord [Psalm 150]. J 

Rejoice Blog: Sawasawa. Katika kuimba kwako, je, umeshatoa album yoyote?

Elandre: Nimetoa album moja inayoenda kwa jina PROJEKT THREE6TEEN inayopatikana pia mtandaoni kwenye soundcloud hapa na pia reverb nation hapa.

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya nyimbo zako ni upi?

Elandre: "Elijah" ambao nimemshirikisha mwanadada kutoka Zambia aitwae Tasila Mwale.

Rejoice Blog: Ni kwa sababu gani unaupenda wimbo huo zaidi?

Elandre: Wimbo huu una miondoko ya ki-Afro pop ukichanganywa na rap. Nilitumia mda mfupi sana kuundika na kwa uhai ulionao, huwagusa wengi wanaousikia na kuisikiliza meseji iliyomo ndani. Nahisi pia naupenda kwa sababu unachezeka.

Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je, anakusaidia vizuri?

Elandre: Hamna anayesambaza kazi zangu. Natafuta sana mtu atakaenisaidia kuifanya hii kazi.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Elandre: Lecrae ambae ni msanii kutoka Marekani, nahisi ndio the most successful Christian Rapper kwa sasa. Ana bidii sana katika kuifanya kazi ya Mungu kupitia kipaji alichopewa.

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Elandre: Tangu mwaka 2007 nilipotoa singo yangu ya kwanza mpaka sasa mafanikio nliyoyapata katika kuimba nyimbo za injili ni pamoja na kutengeneza connections na wasanii wengine kutoka nje ya Tanzania, baraka za afya tele na uhai, na mpaka sasa tunaendelea vizuri. Najua mafanikio ya kifedha yanakuja hivi punde.

Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Elandre: Kupenya katika hili soko letu la Tanzania ndo imekua ni changamoto kubwa sana kwangu, pia kwa watenda kazi wenzangu tunaofanya nao muziki kama huu. Vyombo vya habari haviukubali na kuuchukulia huu mziki kama fursa. Maana naamini kwamba sisi sio wasanii tu, ni zaidi ya wasanii na miziki yetu ina uhai na nguvu za kiMungu maana Mungu anaishi ndani yetu. Pia changamoto nyingine imekua kumpata msimamizi wa kazi zangu, nimekua nikifanya karibia kila kitu peke yangu. Bado najifunza mengi na nitaendelea mpaka kieleweke maana huwezi jua labda nimeitwa kua msimamizi wa wengine wanaokuja nyuma yetu.

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina unayoimba wewe?

Elandre: Bado tunakua. Bado njia haijawa wazi. Bado wasanii wengi hawajielewi na kwa sababu hiyo huenenda katika njia za wasanii wengine wasio wakristo/wa nuruni. Kujitambua kumekua ni changamoto kubwa sana, nahisi pia ni kwa sababu wengi hawajatulia na kuketi chini ya mchungaji mmoja atakaekuza, na kukiendeleza kile kilichomo ndani yao. Muziki huu bado unakua, kwa nionavyo mimi bado uko katika steji za utotoni, unahitaji maziwa na malezi zaidi ili kukua. Lakini ukikua utaleta mabadiliko makubwa sana katika miziki ya Injili hapa nchini. 

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Elandre: Warudi kundini. Mafanikio yako ndani ya Kristo Yesu pekee. Shida kubwa ni kutolitii Neno la Mungu, na kuwa na ushirika na Roho Mtakatifu. Lakini tungekua waaminifu katika hili, tusingetoka nje kwa nia ya kutafuta hela au maisha. Sisi ndo tungekua tunafuatwa na waduniani kujua nini wafanye ili wafanikiwe. Nimeji-include na mimi katika hili swala la uaminifu maana nahisi ndo “key factor” katika hili suala.

Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Elandre: Tofauti na mziki mimi ni Graphic Designer.

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Ndoa na watoto vipi?

Elandre: Bado bachela. Ndoa bado. Mungu akipenda mtasikia shangwe hivi karibuni. J

Rejoice Blog: Safi sana. Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Elandre: Tuutafute uso wa Mungu. Hapo ndipo mafanikio yalipo. Pia tupendane jamani, tuombeane badala ya kupigana mawe. Sisi ni familia moja, inabidi dunia itutazame sisi kama mifano hai. Hamna alie mkamilifu kwa hiyo tuinuane pale mmoja wetu anapoanguka.

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Elandre: Wazidi kutuombea sana.

Rejoice Blog: Ahsante sana Elandre kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Elandre: Asante sana hata kwa hii fursa mlinipa na kuniheshimu. Much love kwenu na nnawatakia mafanikio makubwa katika mwaka ujao, muwe the top blog hapa Tanzania na chombo chenu kizidi kukua mje kukamilisha ndoto zenu pia.

Rejoice Blog: Ameen

Unaweza kuwasiliana na kumpata Elandre kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, na pia kumwalika kuhudumu kwenye shughuli mbalimbali za kumtukuza na kumwinua Mungu... vilevile kushirikiana naye katika kukuza kazi za sanaa katika Injili hapa nchini na duniani kote

Elandre: Social media handle yangu ni @iamelandre yaani hii inatumika kote Facebook, Twitter, Instagram na Youtube [Ukitaka kuona video zangu]

Album yangu iko kwenye link hizi: www.soundcloud.com/iamelandre au www.soundcloud.com/projekt316
www.reverbnation.com/iamelandre

Huo ndiyo mwanzo wa kufahamu zaidi kuhusu Elandre, kuna mengi mengine kuhusu kazi zake za Injili kupitia muziki wa HipHop na shughuli zake nyingine. Usikose kuendelea kufuatilia kipengele hiki cha Msanii wa Wiki kila wiki siku ya jumanne kupata kuwafahamu zaidi wasanii wanaomtukuza Mungu kupitia kazi mbalimbali za sanaa, hususani Muziki wa Injili hasa hapa nchini Tanzania.

Ikiwa unapenda tufanye mahojiano na Msanii fulani wa Injili hapa nchini Tanzania,au ikiwa wewe ni msanii wa muziki au sanaa yoyote katika Injli na ungependa kutambulisha zaidi kazi zako, basi usisite kuwasiliana nasi kwa njia ya simu (call, text, whatsapp) kupitia namba 0714484504 (Alex). Ubarikiwe sana!

 ~~~ TUKUTANE WIKI IJAYO! ~~~

No comments:

Post a Comment