Pages

Tuesday, December 20, 2016

MSANII WA WIKI - SIXBERT MUBILIGI

NDANI YA MSANII WA WIKI HII.... 

Sixbert Mubiligi
Katika Msanii wa Wiki leo tunaye Sixbert Mubiligi kutoka Morogoro

Rejoice Blog: Tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Sixbert: Majina yangu ni Sixbert Eldard Mubiligi, kwenye huduma natumia zaidi Sixbert Mubiligi.

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Sixbert: Mimi nimeokoka kweli kweli; ninaabudu kanisa la TAG - nikiwa Morogoro kwangu ninaabudu TAG Bethel Mwembesongo linaloongozwa na Askofu Mkuu Barnabas Mtokambali. Nikiwa Mtwara naabudu kanisa la TAG Shangani Miracle Temple chini ya Askofu George Musa.

Sixbert Mubiligi katika moja ya Mikutano ya Injili
Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, ulianzaje na wapi ulianzia?

Sixbert: Nimeanza tangu nikiwa mdogo Sunday School Basanza Uvinza Kigoma, na nilipofika umri wa kutosha kuimba na watu wazima niliimba kwaya ya kwanza ya Neema iliyopo Basanza Uvinza, ni kwaya ya kanisa la Anglican. Baadaye nikaja Urambo Tabora na nikaimba kwaya ya ESSACU pale wilayani Urambo. Nilipokuja kwa baba yangu Morogoro nimeimba kwaya ya Safina pale Anglican Magereza Kihonda. Baadae nilipoanza kidato cha kwanza ndipo nilipokutana na wapendwa tukatengeneza bendi iliyoitwa SGS hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa kuingia studio hapo ilikuwa 2005 nikiwa kidato cha tatu na tulifanya kazi kama Maisha bora

Rejoice Blog: Safi sana. Una historia ndefu kwa kweli katika muziki wa Injili. Katika kuimba kwako, je, umeshatoa album yoyote?

Sixbert: Yesu umenipa Heshima  na mwaka 2009 nikiwa kidato cha Sita nilifanikiwa kurekodi albamu yangu iliyoitwa BWANA ATASIMAMA.
Na sasa ninaandaa albamu mpya iitwayo YESU HASHINDWI na albamu ya pamoja kati yangu na rafiki yangu ambae tumeanza nae huduma hii tangu tukiwa sekondari, anaitwa ALFRED MWAKASASA.

Sixbert akiwa na mwimbaji Joshua Silomba
 Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako?

Sixbert: Kazi zangu nasambaza mwenyewe sijapeleka kwa wasambazaji, lakini hizi kazi mbili itabidi nitafute msambazaji. Kwa upande wa usimamizi bado natafuta mtu atakayesimamia au hata kampuni ambayo nitafanya nayo kazi.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Sixbert: Mwimbaji ninavutiwa naya ni Ambwene Mwasongwe na huwa nasikia tu kumfuatilia kazi zake. Kwa kifupi ndiye Fanuel Sedekia wa wakati huu maana anayatunza mafuta ya madhabahu katika uimbaji

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Sixbert: Mafanikio ni mengi cha kwanza uimbaji umenipa digrii Udom  na mengine mengi maana kumtumikia Mungu kuna faida, lakini kubwa zaidi nimepata watu wengi sana ambao ni wa familia ya Yesu Kristo

Sixbert akiwa na waimbaji wengine studio
Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Sixbert: Waoh! Changamoto kubwa ni fedha ambapo huduma hii inahitaji pesa kuliko vile watu wanavyofikiria. Changamoto nyingine ni baadhi ya watumishi utakuta anakuita kwenye huduma wewe binafsi alikuambia mtumishi hali ni ngumu lakini ukifika kwenye mkutano au semina unakutana na muimbaji kutoka Dar ambae anaondoka na bahasha ya laki saba wewe hata mafuta ya gari hupati. Hii kwangu huwa inaumiza hata ungekuwa wewe mwandishi ungeumia

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina unayoimba wewe?

Sixbert: Muziki wa tanzania unakuwa kila siku, na tasnia inang'aa kwa kweli

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Sixbert: Kama umeamua kumtumikia Mungu unatakiwa uwa halisi hapo Mungu atayaachilia mafuta yake juu yako.

Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Sixbert: Mbali na huduma, mimi ni mwalimu wa sekondari Manispaa ya Mtwara pia mjasiriamali 

Sixbert akiwa na mkewe Joyce
Rejoice Blog: Je, umeoa na una watoto?

Sixbert: Yeah mimi ni mume wa mke mzuri Joyce Sixbert. Pia Bwana Yesu katuzawadia Mtoto wa kike  anayeitwa Prettyn.

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Sixbert: Niwaombe watumishi ambao Bwana kawapa kibali cha kuonekana mbele za jamii jitahidini kutamani kuwawezesha wengine ili familia ya wana wa Asafu ikue maana binafsi napenda waimbaji waongezeke kila siku. Na pia tuache ukabila kwenye huduma.

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Sixbert: Ujumbe wangu kwa jamii watusapoti, huduma hii inawahitaji wao ili isonge mbele. Amen

Rejoice Blog: Ahsante sana Sixbert kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Sixbert: Amen, ahsante

Huyo ndiye Sixbert Mubiligi, kijana aliyeanza kumtumikia Mungukwa muda mrefu kupitia uimbaji. Naamini umepata kumfahamu zaidi kwa angalau hatua moja mbele

Kwa mawasiliano na Sixbert kwa habari ya huduma unaweza kumpata kupitia namba 0716552795 au barua pepe mubiligis@yahoo.com


~~~ UBARIKIWE ~~~

No comments:

Post a Comment