Pages

Monday, November 21, 2016

MAOMBI YA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO - SEHEMU YA 2

Na Mchungaji Florian Katunzi


Bwana asifiwe mtu wa Mungu, bado naendelea na mtiririko wa somo hili ambalo ninaamini litafanyika msaada kwako na hata kwa jirani yako. Pia napenda kukumbusha ya kuwa kitabu hiki kitatoka siku chache zijazo hivyo jiandae kukipokea.

Wiki jana tuliangalia utangulizi wa somo hili ambapo nilikufundisha juu ya habari za Mfalme Nebukadreza aliyekuwa kiongozi wa dola yenye nguvu sana ya Ukaldayo na pia alikuwa muabudu miungu. Mara  baada ya kifo chake Mungu alimuinua Mfalme Koreshi ambaye alikuwa mpakwa mafut wa BWANA na alifanya makusudi yote ambayo Mungu aliyaweka.

Leo tutakwenda kuangalia juu ya aina tano za funguo za kufungua malango na milango.  Endelea…………

AINA TANO ZA FUNGUO ZA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO;

UFUNGUO WA KWANZA

1: NENO LA MUNGU
    Neno ni kauli ya Mungu yenye Mamlaka, Uweza na Nguvu za ki-Mungu zenye kuleta mageuzi ya kiroho na kimwili.

Yesu Kristo alithibitisha yakuwa Neno la Mungu lina mamlaka na nguvu pale alipolitumia kufungua mafungo yaliyofunga watu wa Mungu sawasawa na injili ya Luka 4:36 “Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, ni Neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka.”

Tunajifunza pia kwa Neno vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana viliumbwa maana Mungu aliziumba mbingu na nchi kwa Neno lake. Alisema iwe na ikawa.

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Yohana 1:1-5 

Tukitaka kufungua malango na milango iliyofungwambele yetu sharti kwanza tuwe na ufunguo wa Neno la Mungu. Maana Neno ni taa na nuru ya maisha yetu. Aliye na Neno haendi gizani kwa sababu kwa Neno la Mungu hakuna lisilowezekana.
“Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” Luka 1:37

Neno la Mungu kamwe halipiti hivyo tukilishika Neno kila lango na malango hakika yatafunguka. “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe” Mathayo 24:35
Neno lake husimama katika kweli daima. Neno la Mungu huja kwetu likiwa hai, likifungulia imani yetu.
“Ndipo BWANA akaniambia… naliangalia neno langu, ili nilitimize” Yeremia 1:12


UFUNGUO WA PILI

IMANI
Imani sikuzote imekuwa ndiyo alama ya wanafunzi wa Yesu. Wanafunzi wa kwanza walijulikana kama WAAMINI. Yesu alisema “… Yote yawezekana kwake aaminiye” Mark 9:23

Imani humaanisha kumtegemea Mungu kwa hali zote. Wakati Adamu alipofanya dhambi, alijitoa katika kumtegemea Mungu na kujitegemea (ambako ni kutokuamini). Hii ndiyo sababu Mungu ameweka kipaumbele kwenye imani. Imani ni njia ya kuturudishia uhusiano na Mungu (kumtegemea Mungu). “Basi Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Warumi 10:17 

Tunajifunza yakuwa pasipo Neno la Mungu hakuna imani ya ki-Mungu. Maana yake ufunguo wa kwanza ndiyo unaotupeleka kwenye ufunguo wa pili.

Kumtegemea Mungu ndiko kunakoitwa imani. Kwa imani unatoka kwenye kutokuweza hadi kuweza. Kwa imani hakuna lisilowezekana.

A: IMANI NI NINI?
    Imani ni tendo la utii katika kuitikia kile Mungu alichokisema katika Neno lake.
Imani ya kweli inaelezewa katika Utii na Kutenda kulingana na  Neno la Mungu.
“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” Waebrania 11:1
Hivyo pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu; kwa maana kila mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, naye huwapa thawabu wale wamtafutao sawasawa na Neno lake. Ni lazima tumtafute Mungu kwa juhudi na kutamani kwa bidii uwepo wa neema yake.
Imani na utii haviwezi kutengana kama vile ambavyo kutokuamini na kutokutii kusivyoweza kutengana. “Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; hawakuigopa amri ya mfalme. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabiwa ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. Kwa  imani akatoka Misri asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”  Waebrania 11:23-27

B: KWELI TATU ZA IMANI
     Msingi wa kuwa na imani kwa Mungu uko katika kweli tatu muhimu:

Asili ya Mungu;
  
a.     Hawezi Kubadilika.
“Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu..” Malaki 3:6

b.     Hawezi Kushindwa
“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na yakuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika” Ayubu 42:2

c.      Hawezi Kudanganywa
“Mungu si mtu, aseme uongo; wala si mwanadamu ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?” Hesabu 23:19   
Kristo amefanyika chanzo cha imani yetu kwa Mungu. Ukweli kuhusu kifo chake na ufufuko hutoa msingi wa kuamini kwetu.
“Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi” 1Wakorintho 1:30

Ili imani itende kazi ya kufungua malango na milango katika maisha yetu, ni lazima kutii Neno la Mungu. Imani HUTENDA KAZI pale mtu aliyeamini anapofanya sehemu yake kwa imani, hiyo humfanya Mungu naye kutenda sawasawa na kuamini kwa mtu. Angalia mfano wa mwanamke aliyekuwa na msiba wa kutokwa damu muda wa miaka kumi na miwili, aliposikia Neno la uponyaji kupitia Kristo Yesu aliamini na kuadhimia moyoni mwake kumwendea Yesu Kristo kwa imani ili apate kufunguliwa. “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi namiwili alikuja kwa nyuma, akagusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.” Mathayo 9:20-21

Matokeo ya imani sikuzote mwisho wake ni ushindi kwake yeye aaminiye na kumletea utukufu wa Mungu katika maisha yake ya kiroho na kimwili. “… kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu” 1Yohana 5:4


Itaendelea……………………..

No comments:

Post a Comment