Pages

Tuesday, November 22, 2016

MSANII WA WIKI - RITHA KOMBA


RITHA KOMBA KATIKA MSANII WA WIKI
Ritha Komba 
Ni wiki nyingine tena tunakutana katika “Msanii wa Wiki” na leo tuko na Mwimbaji mwingine wa nyimbo za Injili anayechipukia, si mwingine bali ni Ritha Komba

Kuna mengi usiyoyajua kumhusu, lakini leo nafasi ni yako kufahamu angalau machache zaidi kumhusu yeye. Tujumuike pamoja katika safari hii fupi ya kufahamu Ritha Komba, msanii wetu wa wiki hii

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Wapi unaabudu?

Ritha: Nimeokoka, naabudu katika Kanisa la  Kiinjili la  Kilutheri

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, yaani ulianzaje na wapi ulianzia?

Ritha Komba
Ritha: Mimi nilianza kuimba mwaka Jana pale mtumishi wa  Mungu aliponiambia nianzishe pambio kanisani. jumapili iliyofuata nilienda nyumbani nikasema sijawahi kuanzisha pambio wala kuimba kanisani, je  itakuwaje? Nikasema hapana, sitaimba wimbo wa mtu, natunga mwenyewe. Nikatunga wimbo mfupi tu na siku ilipowadia nilipoitwa kuimba nikaimba wimbo wangu binafsi na ukapendwa. Tokea hapo nikawa napewa nafasi ya kuimba na mpaka hivi sasa nimekua muimbaji

Rejoice Blog: Katika kuimba kwako, je, umeshatoa albamu yoyote? Jina ya albamu?

Ritha: Nimeshatoa  album audio na video, nasubiri kuizindua tarehe 18 Disemba pale Shalom Eloi Center, Kigamboni Kisiwani ndipo nianze kuisambaza

Rejoice Blog: Albamu yako inaitwaje?

Ritha: Albamu yangu inaitwa 'Mungu wa  Ajabu' na video hii inapatikana YouTube

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya nyimbo zako ni upi?

Ritha: Katika album yangu napenda nyimbo zote, ila unaonibariki sana ni  wimbo wa  Usifiwe

Ritha Komba
Rejoice Blog: Ni kwa sababu gani unaupenda wimbo huo zaidi?

Ritha: Ni  wimbo ambao unagusa moyo wangu sana kwa matendo ambayo Mungu ameyatenda kwangu pasipo mimi kutenda jema  lolote

Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako?

Ritha: Mpaka sasa bado sijapata msambazaji, nipo kwenye mchakato huo wa kutafuta msambazaji wa kazi zangu

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia zaidi na unapenda kufuatilia kazi zake?

Ritha: Navutiwa sana na waimbaji wengi wa  Nyimbo za Injili; naweza kusema Angel Bernard, Jessica Honore BM na Beatrice Mwaipaja. Huwa napenda sana kufuatilia kazi za hawa waimbaji

Rejoice Blog: Kuna mafanikio yoyote umeyapata katika uimbaji wako?

Ritha: Mafanikio niliyoyapata ni kuwa msomaji mzuri wa  Neno la  Mungu na kujikuta nakuwa mwenye upendo, furaha na amani. Lakini pia najuana na watu wengi zaidi tofauti na hapo awali

Ritha Komba
Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Ritha: Changamoto ni  nyingi hasa  kwa sisi ambao tunachipukia, vitu vingi tunakua hatuvifahamu. Lakini pia suala la  uchumi ni  changamoto kubwa sana, kurekodi kunahitaji hela, kutengeneza video nako kunahitaji hela, matangazo ili kazi iwafikie wengi pia inahitajika hela. Hizo ni  changamoto kubwa nilizoziona

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania?

Ritha: Muziki wa Injili umekua kwa kasi kikubwa sana, sio kama ule wa zama hizo; mambo yamebadilika. Umekuwa ni  muziki wenye ushindani mkubwa. Kwa hiyo hapo ni  kujitoa kwa dhati kuifanya kazi ya Bwana bila kukata tamaa

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Ritha: Wito  ninaotoa mimi ni  huu; kama tumejitoa kwa nia ya dhati kuifanya kazi  ya Mungu kupitia uimbaji na iwe  hivyo, tusitengeneze makwazo kwa Muumba wetu

Ritha Komba
Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Ritha: Mimi ni  mjasiriamali, nasomea journalism and media

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Ndoa na watoto vipi?

Ritha: Nimeolewa sina mtoto bado

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Ritha: Ujumbe kwa waimbaji wenzangu, tufanye kazi  ya Mungu kwa moyo na tupendane sisi kwa sisi bila kujali nani  anaimba vizuri, nani haimbi vizuri. Tuinuane maana kwa Mungu hakutaangaliwa sauti yako ilikuaje au umaarufu, bali Mungu ataangalia tulijitoaje katika kumtumikia yeye

Rejoice Blog: Kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Ritha Komba
Ritha: Napenda kuiambia jamii kuwa; Neno la  Mungu huwa halipunguzwi wala kuongezwa. Wasikilize nyimbo zote za waimbaji bila kubagua ili wapate ujumbe  mzuri. Wajiandae kupokea nyimbo zangu zitawabariki, kuwafariji na kuwasogeza karibu zaidi na Mungu

Rejoice Blog: Ahsante sana Ritha kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Ritha: Ameen!



Unaweza kuendelea kumfuatilia Ritha Komba katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Facebook, Instagram, YouTube na Twitter

Unaweza pia kuwasiliana naye kwa simu  namba 0712496727


~~~ Huyo ndiye Ritha Komba, usikose wiki ijayo tena, tunakutana kumfahamu zaidi msanii mwingine. Ubarikiwe! ~~~

No comments:

Post a Comment