Pages

Monday, December 26, 2016

MAOMBI YA FUNGUA MALANGO NA MILANGO - SEHEMU YA 7

Na Mchungaji Florian Katunzi -EAGT City Center

SILAHA NANE ZA KUFUNGUA MILANGO NA MALANGO YALIYOFUNGWA MBELE YAKO

Bwana apewe sifa. Bado naendela na mfululizo wa somo hili ambapo katika makala zilizopita nilikufundisha aina TANO za funguo za kufungua malango na milango. Nilizitaja funguo hizo ambazo ni Neno la Mungu, Toba, Imani, maombi na Nguvu za Roho za roho Mtakatifu. Kimsingi kama utazisoma na kuzielewa basi ni imani yangu ya kuwa utafika mbali kiimani sanjari na kujua ni kwa jinsi gani unatakiwa kupambana na adui shetani.

Leo nitahamia katika kipengele kingine cha silaha nane za kufungua milango na malango, Endelea….

Maombi yetu ya Kufungua Milango na Malango yaliyofungwa inahitaji Uhodari na Uthabiti katika Imani, hivyo lazima silaha hizi zitumike ndipo Milango na Malango yaliyofungwa yatafunguliwa. Kufungua kilichofungwa si kazi rahisi. Maandiko matakatifu yanasema; “Hatimaye mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani; kwa maana kushindana kwetu si juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa Roho, kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.” Waefeso  6:10-14
Maisha yetu ya Kristo yapo katika mgongano wa kiroho na shetani na huu mgongano unaitwa VITA VYA IMANI. Ambavyo vinaendelea hadi atakapokuja mara ya pili Yesu Kristo kuvikomesha. Lakini ushindi wa mtu wa Mungu umehakikishwa na Kristo mwenyewe kwa njia ya kifo chake pale msalabani. Alipokufa na kufufuka ametangaza ushindi kwa kila amwaminiye tangu wakati ule hata sasa tunashinda na zaidi ya kushinda. Palipo na neno “KUSHINDA” maana yake pana neno “KUSHINDANA”.
Maisha yetu ya imani ni ya kushindana na kushinda. Wengine kwa kutokujua, adui alipokuja kushindana nao wakaogopa, wakaona Mungu amewaacha na kujiuliza maswali mengi KWANINI BWANA AMEYARUHUSU HAYA? Kumbe maisha ya ukristo halisi ni vita sio lelemama ndiyo maana BWANA anasema tuwe hodari na moyo wa ushujaa. “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakaye warithisha watu hawa… uwe hodari tuu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote… usiache kwenda mkono wa kuume au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.” Yoshua 1:6-7
BWANA umtumia mtu hodari na mwenye moyo wa ujasiri sio mtu legelege na dhaifu. Ndiyo maana alimtumia Daudi kumpiga Goliati kwa sababu alikuwa na moyo wa uhodari na ujasiri mwingi. Daudi hakwenda vitani kubahatisha bali alikwenda ksuhindana na kushinda ndivyo ilivyotokea. Maandiko yanasema; “Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea na kuyagawanya mateka yake.” Luka 11:21-22

Yesu Kristo anahimiza kujifunga silaha zetu na kuyalinda Malango na Milango yetu. Pasipo kujifunga silaha hatuwezi kumshinda yule adui shetani. Lazima uzivae hizi silaha ndipo zitakazofanya Ushinde Falme za giza, Wakuu wa giza hili na kuyashinda Majeshi ya pepo wabaya. Maandiko yanasema; “Maana ingawa tunaenenda katika mwili hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili, maana silaha za vita vyetu si za mwili bali zinauwezo katika Mungu hata kuangusha ngome.” 2Wakorinto 10:3-4

Vita vyetu vya kiroho sharti vipiganwe kwa silaha za rohoni – pasipo kuvaa hizi silaha za kiroho hatuwezi kuziangusha ngome zilizojengwa kinyume na zenye kuhakikisha Malango hayafunguliwi.

SILAHA YA KWANZA
Zipo silaha nane za kiimani zenye nguvu za kufungua malango na milango iliyofungwa katika maisha yetu ya kiroho na kimwili. Silaha hizo ni:-

(i) KATAA
    Imani ni kuwa na hakika katika Mungu na mwenye haki ataishi kwa imani. Maandiko matakatifu yanaonyesha waziwazi ya kuwa msingi wa wokovu ni imani. Yatupasa kuyakataa yale tusiyoyaamini katika imani yetu, mfano wa Musa alivyokataa kuitwa mtoto wa binti Farao, japo kuitwa mtoto wa binti Farao kulikuwa na faida nyingi za kimwili lakini akachagua ufalme wa Mungu na haki yake kuliko ufalme wa Farao ambao mwisho wake ni kutupwa jehanamu ya moto. Hivyo Musa akatumia silaha hii ya kwanza ya KUKATAA matokeo yake BWANA akamtumia kama shujaa na mkombozi wa wana wa Israeli toka utumwani Misri. Maandiko matakatifu yanathibitisha; “Kwa Imani Musa alipozaliwa alifichwa miezi mitatu na wazazi wake kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri wala hawakuogopa amri ya mfalme KWA IMANI MUSA ALIPOKUWA MTU MZIMA ALIKATAA KUITWA MWANA WA BINTI FARAO. Akaona afadhali kupata mateso kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo akihesabu kushutumiwa kwake Kristo ni UTAJIRI MKUU kuliko hazina za Misri kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. Kwa Imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme, maana alistahimili kama amuonaye yeye asiyeonekana kwa Imani alifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu ili yule mwenye kuangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao” Waebrania 11:23-28

Musa alikataa kuitwa mtoto wa binti Farao, ukawa ndio mlango wa ukombozi wa wana wa Israel kutoka katika milango ya kuzimu ya Farao. Hii ni silaha kubwa sana ambayo lazima tuivae kabla ya mambo yote. Ni lazima kwa Moyo wako wote na Roho yako yote na kwa Akili zako zote Kataa hali uliyonayo katika ulimwengu wa Roho ama katika Mwili. Maandiko matakatifu yanasema; “Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.” Mithali 18:20-21
Ukiri katika ulimi una nguvu ya kuangusha malango na milango ya kuzimu hivyo ulimi wa imani ni mti wa uzima. Ni vema kutumia ndimi zetu kujitamkia mema sisi wenyewe, kutamka mema kwa watoto wetu na juu ya mali zetu maana BWANA Mungu alitamka iwe na ikawa. “Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu” Mithali 10:20

Dada mmoja pale Morogoro eneo la Forest aliokoka akiwa na miaka kumi na mitano (Miaka 15), siku moja akiwa anatoka shule pale Morogoro mjini, alikutana na mvulana mmoja kumbe ni mjumbe wa shetani (mtu jini) lakini yeye aliona ni mvulana, wakasalimiana, lakini kumbe huyu binti amevamiwa na nguvu za yule jinni kwa sababu alimwambia dada nimekupenda naye akasema asante kama utani lakini ndo ukiri wa kinywa. Baada ya hapo huyu binti alianza kuota ndoto mbaya, anafanya mapenzi; hiyo hali iliendelea kwa muda mrefu akiwa ndani ya wokovu. Huyu binti alipokuwa anakuja kwangu kuniona alikuwa na umri wa miaka thelathini na sita (Miaka 36) akiwa bado hajaolewa, hiyo ilikuwa mwaka 2012, akisema;“Mchungaji nimefunga na kuomba na nimetoa sadaka sana lakini sipati mpenyo, ee Mtu wa Mungu niombee.”

Wakati naanza kumpa ushauri ili nipate kumwombea, nikaitiisha ile nguvu iliyo mfunga kwa jina lenye nguvu la Yesu Kristo. Ndipo nguvu ya pepo jinni dume likapiga kelele likidai huyu binti ni mke wake, limemuoa akiwa na umri wa miaka kumi na mitano kule Morogoro. Nikaipinga ile nguvu ya pepo, nikasema huyu ameokoka, ninyi mnawezaje kukaa ndani yake? Nikahoji tena ni mlango  gani mliotumia kumfunga huyu binti; yule jini akasema waziwazi huyu binti ni mvumilivu na mwaminifu sana kwa huyo Mungu wenu, lakini mimi ninammiliki kwa sababu yeye mwenyewe hajawahi kunikataa na kuitengua ndoa yetu, kwani hujui imeandikwaje katika Warumi? “Kwasababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, Utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” Warumi 10:9-10

Yule kijana (Jini) alimwambia binti nakupenda naye akakubali lakini hawakuonana tena na ni miaka zaidi ya kumi na sita ndoa ipo katika ulimwengu wa roho. Ukiri una nguvu ya Uzima ama Mauti. Ni lazima ukatae  na utengue kila mkataba na maagano yote ya giza sawasawa na kuamini kwako. Ndiyo maana Musa alikataa kwanza kabla ya wito wake. Tendo la kukataa kuitwa binti Farao ndilo likamfanya Mungu amuite kwa kazi yake.

Wakristo wengi wanataka kufunguliwa Milango na Malango lakini bado hawajakataa kabisa Mizimu ya ukoo, Mizimu ya mababu na mabibi zao, maagano mbalimbali walioungamanishwa kwayo kabla ya wokovu. Usikiri Udhaifu juu yako, juu ya watoto wako, juu ya mume wako, juu ya mke wako, juu ya kazi yako, juu ya ndoa yako wala juu ya maisha yako.
         
 “Neno BWANA lilinijia, kusema, kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; Nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana Mungu! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. LAKINI BWANA akaniambia, USISEME, Mimi ni mtoto maana utakwenda kwa kila nitakayekutuma kwake, nawe UTASEMA KILA NENO NITAKALOKUAMURU. Usiogope kwasababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana” Yeremia 1:4-8

Usiseme kinyume na Neno la Mungu juu yako maana BWANA anakuwazia mema naye ulituma Neno kwako lipate kukuponya na kukufungulia milango na malango ya Baraka na Ustawi.
Angalia Musa pamoja na BWANA kumtumia katika kutenda maajabu na miujiza mingi, lakini Musa alikufa akiwa na  utasi (kigugumizi) kwa sababu hakuukataa udhaifu huo bali aliukubali kuwa sehemu ya maisha yake. Maandiko yanathibitisha;
“Musa akamwambia BWANA, Ee Bwana, mimi si msemaji tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. Akasema, Ee Bwana nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. HASIRA YA BWANA ikawaka juu ya Musa, akasema, je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki, naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara.” Kutoka 4:10-17

Mungu alimkasirikia Musa kwa kitendo cha kukataa Uponyaji wa kinywa chake. Matokeo yake mtumishi wa Mungu Musa mpaka anakufa, alikufa akiwa na utasi (kigugumizi).

Pia tunajifunza kwa YABESI; alikataa maisha ya huzuni, Bwana akageuza huzuni zake kuwa heshima. Kabla ya kupokea hicho unachotaka lazima uvae Silaha hii ya kukataa utaona mlango unafunguka mbele yako.“Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze, na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akasema, Ni kwasababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akasema, Lau kwamba ungenibarikia kwelikweli, na kunizidishia hozi yangu na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.” 1Nyakati 4:9-11

Pamoja na jina lake kuitwa huzuni, Yabesi alipomjua Mungu alikataa kuitwa huzuni, akakataa maisha ya huzuni. Ndani mwa Maombi haya ya Kufungua Milango na Malango ni lazima tukatae malango yote yaliyotupwa juu yetu au tumezaliwa nayo, maana katika ukiri wa Imani mna nguvu ya kufungua Milango na Malango.

Tunajifunza kwa AYUBU; Pamoja na mateso ya zaidi ya miaka kumi na saba (miaka 17), Kuugua, Kufilisika na Misiba, lakini bado mtumishi huyu wa Mungu alikataa kutamka kinyume cha Imani yake katika Mungu. Katika mambo yote Ayubu hakufanya dhambi wala kumuwazia Mungu kwa upumbavu. “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na yakuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada  ya ngozi yangu kuharibiwa hivi. Lakini, pasipokua na mwili wangu nitamuona Mungu; Nami nitamuona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine, Mtima wangu unazimia ndani yangu.” Ayubu 19:25-27

Haya maneno yalifungua Mlango na Milango ya Ayubu tena akainuliwa toka kwenye shimo la uharibifu.  Baada ya hayo yote, BWANA aligeuza uteka wa Ayubu.

 “Basi huyo BWANA akaubarikia mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake, naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia efu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume saba, binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume. Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, nae akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne. Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku.” Ayubu 42:12-16

Ayubu alikataa  Kukiri udhaifu, Kukiri misiba, Kukiri mateso japo alikua kwenye mateso. Alisema, nalitoka tumboni kwa mama yangu ni uchi nitarudi nikiwa uchi. Maandiko matakatifu yanasema; “Maana mwenye kuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna. Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadharika huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote.” Muhubiri 11:4-5

Kwa imani katika Kristo Yesu yatupasa kukataa yaliyokinyume na imani na tukiri yakuwa anaweza kufanya mambo yote;  Aweza Kufungua Milango na Malango yaliyofungwa. Bwana Yesu Kristo anamtumia mtu aliye tayari kutumika na si vinginevyo. Acha kujiua kwa maneno ya kinywa chako. Maana yeye Kristo Yesu ni mwaminifu. Vaa na ujifunge SILAHA yako itakusaidia. “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.” Waebrania 3:20

No comments:

Post a Comment