SALAAM ZA MAASKOFU WA KKKT KWA
WATANZANIA WOTE KUHUSIANA NA MATUKIO YA KUCHOMA MOTO MAKANISA YA KIKRISTO ENEO
LA MBAGALA – DSM.
Wapendwa Katika
Bwana,
Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla.
Neema na Iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba na
Bwana wetu Yesu Kristo, Amina.
Sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), tumepokea kwa
mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa katika eneo hili la
Mbagala. Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran Mission Cooperation
(LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya Kimissioni vya Ulaya na Marekani.
Tumelazimika kukatisha mkutano huo ili kufika hapa Mbagala. Tumekuja kwa
madhumuni makubwa matatu:
1.
Tumekuja kuwapa pole na kusimama pamoja nanyi
katika uchungu mkubwa mlio nao. Machozi yenu ni machozi yetu. Machozi yetu ni
machozi ya Kristo mwenyewe aliye Bwana wa kanisa linaloteswa. Jipeni moyo kwa kuwa yeye
aliushinda ulimwengu (Yohana 16:33).
2.
Tumekuja kuonyesha majonzi yetu makubwa kwa vitendo vya uvunjifu wa
amani, kuporomoka kwa umoja na mshikamano wa watanzania. Huu ni msiba mkubwa,
na wenye msiba ni watanzania wote, wenye dini na wasio na dini.
3. Tumekuja
kushiriki pamoja nanyi kupokea matumaini ya Tanzania mpya. Katika majivu haya yaliyotokana na
kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa. Majivu haya na
machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya itakayojali upendo, uvumilivu,
ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa kuabudu na dola isiyo na dini.
Katika ujio huu wa maaskofu hapa Mbagala, hatukuja hapa
kufanya haya yafuatayo:
1. Hatukuja
kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaokashifu dini za wenzao, wawe na
ruhusa kutoka mamlaka zilizo juu au kama wanajituma wenyewe.
2. Hatukuja
kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaodhalilisha misahafu ya dini; wawe
wametumwa, kutegeshewa na mamlaka zozote au kwa misukumo ya utashi wao binafsi
ili kupata kisingizo cha kugombanisha madhehebu ya dini.
3. Hatukuja
kuwahukumu hata kama hatukubaliani na wanaochoma makanisa na kuiba mali za
makanisa kwa kisingizio cha kumtetea Mungu. Kisasi cha dhambi hiyo tunamwachia
Mungu mwenyewe aliyedhihakiwa na walionajisi madhabahu yake.
Wapendwa wana KKKT na watukuka sana, wana na mabinti wa
Tanzania ya Julius Kambarage Nyerere; kilichotokea Mbagala katika wiki ya
kuadhimisha siku ya Baba wa Taifa, ni kebehi si kwa Baba wa Taifa bali ni
kebehi kwetu sisi wenyewe tunaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa. Yeye
amelala baada ya kazi njema. Apumzike kwa amani na tunu zake zifufuke katika
majivu haya yaliyotokana na kuchomwa kwa amani na mshikamano wa Tanzania
aliyoijenga.
Kilichotokea Mbagala ni mateso ya kimbari, yaani mateso
ya Kanisa (Persecution). Mateso haya ni matokeo ya mbegu ya magugu iliyopandwa
katika bustani njema na sasa magugu hayo yanazaa matunda machungu. Dalili za
mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya kanisa; zilianza kitambo na
hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa Taifa. Dalili hizo ni kama hizi zifuatazo:
·
Uchochezi wa wazi kuwa taifa hili linaendeshwa na unaoitwa “mfumo
Kristo”, na kuwa Baba wa Taifa alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa hili.
·
Ubishi usio na tija juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali hapa
nchini na hata kudiriki kushawishi na kugomea zoezi la sensa ya watanzania.
Lengo la ubishi huu ni mbegu inayoweza kuratibisha na kurasmisha mateso ya
kimbari na mateso ya kanisa.
·
Matumizi mabaya ya baadhi vyombo vya habari, vyenye lengo la
kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko ya kidini miongoni mwa watanzania
·
Ukimya wa vyombo vya dola juu ya vitendo vya uvunjaji wa sheria ya
matumizi ya vyombo vya habari. Kwa vyovyote vile, uvumilivu wa dola hauna
maslahi mapana kwa mustakabali wa taifa letu na ni mateso ya kimbari, mateso
kwa kanisa, na kwa wantanzania wote; wawe wengi dhidi ya wachache au wachache
dhidi ya wengi.
·
Madai yasiyo ya kawaida na ya mara kwa mara kwa serikali inayodaiwa
kutokuwa na dini. Madai hayo ni kama:
·
1.
Kulazimisha uvaaji wa alama za kidini katika taasisi za umma ili
kurahisisha na kuratibisha tofauti za watanzania. Tunajiuliza: Likitokea la
Mbagala katika mashule yetu na vyuo vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa
wangapi?
2.
Madai yanayojirudiarudia kutaka balozi za nchi fulani kufungwa hapa
nchini. Madai haya yanaashiria kutaka balozi za nchi fulani tu ndiyo ziwe hapa
nchini.
3.
Madai na mashinikizo ya Uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa
nchini
4.
Mashinikizo ya kidini yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na
kisheria.
5.
Mashinikizo ya kidini juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa
serikali na katika ofisi za umma,
6.
Kuhoji na kupotosha juu ya ushirikiano wa serikali na mashirika ya
dini katika utoaji wa huduma za kijamii hususan afya na elimu hapa nchini
Wapendwa wana KKKT na Wapendwa watanzania wote. Hata kama
wanaofanya mambo haya ya kusikitisha wametunukiwa hadhi ya kuitwa kuwa ni “wana
harakati”, tofauti na wanaharakati wanaotambuliwa na watanzania walio wengi,
tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote kuwa uana harakati wao usitumike kuvunja
nchi na sheria za nchi. Tanzania yenye amani na mshikamano ni tunda la dini
zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na hali zote za kiuchumi.
Hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii.
Kwa macho na masikio yetu, tumeendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa
huko Zanzibar, Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa
Mbagala. Wakati wote uvumilivu wa wakristo huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge
na woga. Ikumbukwe kuwa hata wanyonge na waoga, hufika wakati wakasema “sasa
basi” pale wanapodhalilishwa kupita kiasi. Hatuombei wakristo wafikishwe hapo.
Tumeshuhudia wizara zetu zikivamiwa mchana kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa
watuhumiwa wa uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto; mahakama
zikilazimishwa kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa, uhai wa viongozi wa
dini ukitishiwa hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa vibao hadharani kwa
sababu ya zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia kuhoji, watu hawa wavamie
nini ndipo hatua zichukuliwe? Wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya
kulinda mali na uhai washtuke? Wamwue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni
tishio kwa usalama wa taifa letu?
Sisi tulioitwa kwa njia ya nadhiri na viapo vitakatifu, tunawasihi sana waumini
wa dini zetu na watanzania kwa ujumla, wenye wajibu wa kututii na wasiolazimika
kututii, kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda taifa hili na watu wake.
Kamwe hawezi kuliacha liangamie.
Kwa Wakristo wote, huu ni wakati wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya
amani ya taifa hili. Mkristo wa kweli ni yule aliye tayari kuteswa kwa ajili ya
Kristo na kanisa. Wakristo hatuko tayari kuua, kutesa, kulipiza kisasi ili
kumtetea Kristo. Mungu wetu hatetewi kwa kuua wengine na kuchoma madhabahu ya
dini nyingine.
Katika mateso haya, kanisa litaimarika zaidi; na katika majivu haya ya Mbagala,
Tanzania mpya itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana. Tunawataka wakiristo
wote kusamehe na kuendelea kuwa raia wema. Kushiriki kikamilifu katika kuleta
mabadiliko ya kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa. Wakati wengine
wanaweka mikakati ya kuchoma madhabahu, wakiristo tuweke mikakati ya kuomba na
kushiriki vema katika haki zetu za uraia. Pamoja na kuwa wapole kama njiwa,
imetupasa pia kuwa na busara kama nyoka (Mathayo 10:16).
Daima tukumbuke kuwa, “KUSHINDANA
KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA
WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO”
(Waefeso 6: 12).
Ni sisi Maaskofu
wenu kwa Neema ya Mungu,
1.
Askofu Dr. Alex G. Malasusa – Mkuu, KKKT na D/Mashariki na Pwani
2.
Askofu Dr. Stephen Munga –Mkuu, D/Kaskazini Mashariki
3.
Askofu Dr. Martin Shao – Mkuu, D/Kaskazini
4.
Askofu Dr. Thomas Laizer – Mkuu- D/Kaskazini Kati
5.
Askofu Dr. Benson Bagonza- Mkuu, D/Karagwe
6. Askofu
Isaya J. Mengele – Mkuu, D/Kusini
7. Askofu
Levis Sanga – Mkuu- D/Kusini Kati
8. Askofu
Elisa Buberwa – Mkuu –D/Kaskazini Magharibi
9. Askofu
Andrew Gulle – Mkuu, D/Mashariki ya Ziwa Victoria
10. Askofu
Michael Adam –Mkuu, D/Mkoani Mara
11. Askofu
Renard Mtenji – Mkuu, D/Ulanga-Kilombero
12. Askofu
Dr. Israel-Peter Mwakyolile – Mkuu, D/Konde
13. Askofu
Job Mbwilo – Mkuu, D/Kusini Magharibi
14. Askofu
Dr. Owdenburg Mdegella- Mkuu, D/Iringa
15. Askofu
Jacob Ole Mameo- Mkuu, D/Morogoro
16. Askofu
Zebedayo Daudi – Mkuu, D/Mbulu
17. Askofu
Paulo Akyoo – Mkuu, D/Meru
18.
Askofu Charles Mjema – Mkuu, D/Pare
19.
Askofu Mteule Amon Kinyunyu- Mkuu, D/Dodoma
20.
Askofu Mteule Dr. Alex Mkumbo- Mkuu, D/Kati
Mbagala, DSM, 18 Oktoba 2012