Tuesday, February 12, 2013

MAOMBI YA KUANGUSHA NGOME by Rev Florian Katunzi



KARIBU katika makala haya yanayoandaliwa na Mchungaji Florian J. Katunzi, wa Kanisa la EAGT City Centre,lenye makao yake viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam. Somo la wiki hii ni Maombi ya kuangusha Ngome…

 “MINARA INAYOSHIKILIA MAFANIKIO YAKO ITAANGUSHWA.” Endelea….
Nianze makala yangu ya leo kwa kuwashukuru wasomaji wa makala hizi katika gazeti, wasikilizaji wa vipindi vyetu katika Redio WAPO FM, ya Dar es Salaam, Redio Ushindi FM, Mbeya, Redio na wale wa Mwanza.


Nimepata shuhuda nyingi za wale waliofuatilia mahubiri haya na wakapata mabadiliko makubwa katika maisha yao.Ninataka kuwahakikishia kuwa ushindi wetu upo katika kudumu kwenye maombi, kusoma kwa bidii Neno la Mungu na kuishi maisha matakatifu.Ukishikilia mambo hayo hakika ngome ya adui haitasimama dhidi yako, utakuwa huru na utarithi Baraka zote ambazo Mungu alikukusudia.
Kama tulivyoanza mwaka mpya kwa maombi, pale PTA,ndivyo itakavyokuwa mwaka huu tumeazimia kuanza kwa maombi na tutakuwa katika maombi ya mfungo kwa siku mbili kila
wiki yaani Ijumaa na Jumamosi.
Baada ya shukrani hizo, sasa tuingie katika somo letu,jipya linaloanza wiki hii, ambalo ni MAOMBI YA KUANGUSHA NGOME.Ukisoma Bibilia katika kitabu cha 1Mambo ya Nyakati 16:11,Neno la Mungu linasema:“Mtakeni Bwana na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote.”
Katika maombi yetu ya kuangusha ngome zinazoshikili mafanikio yetu, hatuna budi kuutafuta uso wa Bwana na nguvu zake siku zote. Ngome haziwezi kuanguka tusipokuwa na nguvu za Bwana.
Tukichunguza maandiko ya Biblia tunaona jinsi wanadamu wanavyojaribu kujenga mnara kinyume na Mungu ili kutekeleza mapenzi yao badala ya mapenzi ya Mungu. Hata leo adui na mawakala wake wanajitahidi kujenga mnara dhidi ya watu wa Mungu ili kuzuia mafanikio yao.
“Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja.Ikawa watu waliposafiri pande za Mashariki, waliona nchi tambarare, katika nchi ya Shinari; wakakaa huko.Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome………..Haya na tujenge mji, na mnara na kilele chake kifike mbinguni, , tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote…..BWANA akashuka
ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu.BWANA akasema, Tazama,watu hawa ni taifa moja na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayowaza kufanya,wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya.Haya,natushuke huko tuwachafulie usemi wao ili
wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji.Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa babeli; maana hapo ndipo BWANA alipoichafua lugha ya dunia yote na kutoka huko BWANA akawatawanya waende usoni mwa nchi yote.” (Mwanzo 11:1-9) Watu wa Shinari, walikusudia kujenga mnara kinyume na mapenzi makamilifu ya Mungu, waligeuza utaratibu waMungu alioutoa wa kuijaza nchi na wao wakaamua kujenga mnara ili kuzuia mpango wa Mungu.
Kama watu hawa walivyofanya ndivyo mipango miovu inavyopangwa dhidi yako na minara inajengwa ili kuzuia mipango yako, lakini katika maombi haya ya kuangusha ngome
tunakwenda kuharibu mawasiliano yao na kuangusha minara iliyosimamishwa kinyume chako.Minara hii inayojengwa kinyume chetu ili iharibu mawasilianoyetu katika ndoa, katika kazi, katika biashara, na hata katika makusanyiko yetu, ni lazima tuiangushe ili tuishi kwa upendo na umoja.“Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili,bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)
tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka,kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote,kutii kwenu kutakapotimia.” (2Wakornto 10:3-6).
Ngome zinazotajwa hapo juu ni minara ya mawasiliano ambayo adui huitumia kutushambulia na tusiposimama imara kumpinga hatutatashinda.Tukimkumbuka Yakobo alipotoka Labani kwa mjomba wake,mkewe aliondoka na vijimiungu vya huko, vinyago hivi viligeuka kuwa minara ya kumzuilia mbele za Mungu hadi alipoviangamiza na kumjengea BWANA madhabahu nakumfanyia ibada.
Tukimtazama mfalme Ahabu, yeye aliamua kuijengea miungu ya baali madhabahu na kuitumikia, madhara yake yalikuwa makubwa. Huu ni wakati wetu kuondokana na minara
inayojengwa kinyume chetu, tukiiangamiza kama Yakobo alivyofanya na si kukumbatia miungu mingine kama ilivyokuwa kwa Ahabu.

 

Tutaendelea wiki ijiyo…………


No comments:

Post a Comment