Neno la Mungu katika Luka 16:15 “ Hapo akawaambia,
Ninyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana
kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka.”
Leo nimesukumwa niongee juu ya jambo hili linalotusumbua sisi Wakirsto na jamii kwa ujumla. Imekuwa kama kawaida siku hizi watu kuishi maisha ya unafiki.
Unafiki ni hali ya kutukuwa na maisha ya ukweli kwa
kuwa na maisha ambayo hayana picha halisi ya kile kilichoko ndani ya moyo ya
mtu.
Mtu mnafiki anafanya hivyo ili kupata sifa kwa watu
wanamzunguka kama vile wachungaji,mabosi ofisini,marafiki na ndugu.
Mara nyingi lengo la mnafiki ni kuweka picha nzuri yake
kwa watu huku akihakikisha kwa njia yoyote ile wengine wanaonekana wabaya.
Sio rahisi sana kumjua mnafiki maana anaweza kujifanya
rafiki yako ili uwe wazi kwake apate nafasi ya kujua mtazamo wako ili aende
kueleza kwa watu wengine kwa njia ya tofauti ambayo inakufanya uonekane mbaya.
Kama neno linavyosema hapo juu katika Luka 16:15 Mungu
anajua mioyo ya wanafiki kwamba wanajifanya wema mbele za watu lakini hawako
hivyo.
Pia katika Mathayo 6: 1“Angalieni msifanye wema wenu
machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya hivyo, hampati
thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.”
Neno linatuasa kabisa kutojifanya kwamba ni wema mbele za watu ili hali
ndani ya mioyo yetu hatuna upendo nao,Mungu hatatupa thawabu kama tuna tabia
hiyo.