Mchungaji Florian Katunzi |
Karibu katika mfufulilizo wa somo hili jipya linalofundishwa na Mchungaji Florian Katunzi wa EAGT City Centre, ambalo naamini ukilifuatilia
kwa makini hautatoka kama ulivyo. Pia napenda kukwambia ya kuwa jiandae
kukipokea kitabu hiki ambacho bado kipo jikoni na kitakuwepo mtaani hivi punde.
Leo tunaanza na Sehemu ya Kwanza
KUOMBA maana
yake ni Kumwita Mungu. “Katika shida yangu nalimwita BWANA, Na
kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu
kikaingia masikioni mwake.” Zaburi
18:6
Ndani mwa
maombi haya BWANA atakufungulia milango, na hakuna malango
yatakayofungwa mbele yako tena. Neno la Mungu linatuambia:
“Haya ndiyo BWANA amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika
mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya
wafame; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Nitakwenda
mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande
milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za
gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni
BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.” (Isaya 45:1-3)
Kipindi hiki
wana wa Israeli walikuwa uhamishoni Babeli, kumbuka walitekwa na kuchuliwa
uteka mpaka nchi ya Babeli na Jemadari Nebukadreza, mnamo mwaka 605 KK, baada
ya kuwashinda wamisri katika vita ya Karkameshi. Wakati huo kulikuwa na
makundi mawili yaliyopelekwa uhamishoni Babeli, kundi la pili lilikuwa ni lile
lililochukuliwa mwaka 586 KK.
Huyu
Nebukadneza, ni mtoto wa kiume wa Nabopolasa, aliyemridhi baba yake kuwa
mtawala wa dola ya Wakaldayo mwaka 605 KK. Hii ni kwa mujibu wa kitabu cha The Cambridge Acient history III Uk. 212.
Nebukadireza alikuwa jemadari
kijana aliyekuwa ana misuli ya vita na tena shujaa na mwerevu wa mapigano, hivyo
alikuwa na sifa zote za kurithi kiti cha baba yake.
Wachambuzi wa
mambo ya kale wanamuelezea kuwa alikuwa ni askari na mwanasiasa aliye heshimiwa
sana kutokana na uwezo wake wa kuongoza mapigano na kujenga hoja katika uwanja
wa kisiasa.
Baada ya kutwaa madaraka, mfalme huyu mpya alihusika kujenga vyema himaya na alama za Babeli katika maeneo
mbali mbali ya dunia, tena alijiongezea sifa kwa kumuoa Malkia wa Media Amyhiya, binti wa Cyaxareas, aliyekuwa na
utawala wa Kaskazini.
Neno la Mungu
katika kitabu cha Daniel 2:36-43, linatuonyesha kuwa baada ya Nebukadreza
aliyekuwa kiongozi wa dola yenye nguvu sana ya Ukaldayo kiasi cha ufalme wake unafananishwa na kichwa cha
dhahabu kwa thamani yake, hata hivyo,
alipojiinua kiasi cha kutaka kuabudiwa, ufalme wake, ulikomeshwa na Dola ya
Ukaldayo iliingia hatua ya mwisho pamoja na kuchaguliwa kwa Nabondus mnamo
mwaka 556 KK.
Baada ya kufa
kwa Nebukadreza kinafuata kipindi kifupi cha kupinduana na kuchinjana kwa
watawala na mwisho kabisa utawala wa Dola ya Ukaldayo unafutika kabisa na
unaibuka utawala wa Wamedio, Umedi na Uajemi (Medionapersia) chini ya Mfalme
Koreshi Mwajemi na Dario wa wamedi, walioungana pamoja na kuangusha Dola ya
Ukaldayo mwaka 538. Utawala wa wabanabe ulidumu kwa kipindi cha miakamia mbili
(200), mpaka 331 KK. Ndani ya kipindi
hiki cha utawala wa Wamedi na Wajemi, tunamuona Koreshi, tuliyemsoma katika
andiko letu la msingi akitimiza unabii uliotolewa kwa kinywa cha Nabii Isaya
miaka mia moja hamsini (150) kabla ya kutimizwa kwake katika mwaka 538.
“Katika mwaka wa kwanza wa
Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya
milki ya wakaldayo. Katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Daniel, kwa
kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka ambayo Neno la BWANA lilimjia
Yeremia Nabii, kutimiza ukiwa wa Yerusalem, yaani, miaka sabini. nikamwelekezea
Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwake maombi na dua, pamoja na kufunga na
kuvaa nguo za magunia na majivu.” (Daniel 9:1-3).