Mtumishi Frank Philip |
“Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji
kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani
…Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza
nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika”
(Mithali 6:26 & 32,33).
Nimeona jambo hili, nami nikatafuta kujua kama kuna
hekima ndani yake “men’s hearts can be shared, but women’s hearts replaces”.
Maana yake: Moyo wa mwanaume ukipenda, waweza kupenda tena kwa wakati mmoja,
ila moyo wa manamke ukipenda, humwondoa wa kwanza na kumpenda mwingine.
Ukitaka kuona kwa njia ya urahisi, jiulize ni kwanini
mwanaume mmoja anaweza kuoa wake zaidi ya mmoja na maisha yakaenda? Na jiulize
tena, je! Mwanamke anaweza kuwa na mpenzi wa nje ampendaye sana, na maisha yake
ya ndoa/mahusiano yakawa sawa? Wote wawili: mwanamke na mwanaume, wana hatari
ya kuingiliwa mioyoni mwao, japo kwa madhara tofauti.
Hii hali sio rahisi kuikubali katika mahusiano ya
kawaida ambapo mtu anatoka nje ya ndoa/uhusiano kwa siri. Mara nyingi mtu
afanyaye mambo hayo, hudhani yuko sawa, kumbe ameathirika kabisa. Ukitaka kujua
ninachosema, angalia mambo ya kawaida kabisa ya kwenye ndoa/uhusiano kwa watu
ambao mmoja au wote wamenaswa nafsi na kahaba. Mambo ya kawaida kabisa kwenye
uhusiano/ndoa yanaanza kuwa kero, mzigo na ya kuchosha. Ukiona hii shida,
usipambane na mtu kwa jinsi ya mwilini, shughulika na nafsi kwa sababu hapo ndipo
penye shida.
Nitasema na wanawake sasa. Hii hali ya “replacement”,
huwa haianzi mara moja. Huenda kwa awamu, na hatua mbali mbali, kuanzia hisia,
matendo kisha ngono. Ndio maana mwanamke akitoka nje ya ndoa watu husema
“amefika mbali”. Mara zote huanza na “nafsi kunaswa” na kahaba. Kama kuna mtego
mbaya, ni kuacha nafsi yako inaswe. Kwenye nafsi ndiko kuliko na mawazo na
maamuzi. Kama nafsi imenaswa, mara ZOTE mtu ataanza kuwaza tofauti, na kisha
kufanya maamuzi mabaya. Ndio maana tunaonywa sana kwamba “Linda moyo wako
kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima” (Mithali
4:23). Ukitaka kuona uzima kwenye ndoa/uhusiano wako, linda sana moyo wako;
ukitaka kuona mauti kwenye ndoa/uhusiano wako, achilia moyo wako uingiliwe.