Karibu atika mifululizo yote ya somo hili kutoka mwanzo mpaka sasa
imekuwa ni suala la kuangalia ni kwa jinsi gani nafsi zetu zinahusika sana
katika Uhai wa Kanisa. Sehemu ya mwisho nitasema nawe kwa kifupi sana kuhusu
Uhusiano wa nafsi ya Kanisa.
Karibu tujifunze pamoja…..
Luka 12:15 inasema hivi;
Akawaambia, Angalieni,
jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo
navyo.
Ni heri kila mmoja akahakikisha ya kwamba Nafsi yake iko na
furaha kila wakati, kwa ajili ya uhai wa kanisa lako, lakini pia kwa ajili ya
uhai wa nyumba yako kama msingi wa kanisa, kwa ajili ya ofisi yako, kwa ajili
ya ukoo wako.
Lakini pia ni vema kila mmoja akahakikisha anafanya bidii kumfurahisha
mwingine na kuifanya nafsi ya mwingine isiwe na jeraha hata moja, kuifanya
nafsi ya mwingine isitende dhambi, kila mmoja acheze karibu na mwenzake, kama
kucheza basi tucheze peke yetu, hakikisha unamlinda mwenzake asipate shida wala
asipotee.
1 Wakorintho 8:12 tunasoma hivi;
Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri
iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo
Kuna Uhusiano Mkubwa kati ya Usalama na
Ubora wa Nafsi yako na Uhai wa Kanisa
Sasa labda tutazame kwa nafasi nyingine uhusiano wa Nafsi
yako ikiwa na Usalama na ubora wa nafsi yako na Uhai wa Kanisa ikiwa ni la
nyumbani au ni mahali unapoabudu au ofisini kwako au hata shuleni kwako
unakosoma.
Labda niweke jambo hili la msingi, tunapozungumzia kanisa ni
lazima tukajua ya kwamba si suala la dhehebu moja tu au suala la watu wanaosali
kwa pamoja lakini suala la Kanisa ni jambo linalohusu watu wote waliookoka na
wanaomkubali BWANA YESU kuwa ni mwokozi wa maisha yao na Mfalme wa Ulimwengu
wote.
Sasa kuna shida ambayo ni muhimu tukaishughulikia vizuri
kidogo ili tusipate shida tunapoangalia utekelezaji wa Somo hili, na jambo
lenyewe ni lazima akili zetu na fahamu zetu zifunguke tukajua mambo kadhaa ili
tuone Umuhimu wa kuona Nafsi ya kila mmoja inakuwa salama na bora ili Kanisa
liweze kuwa Hai.
1 Wakorintho 3:16-17 tunasoma hivi;
Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa
Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu
atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Sasa kuna jambo la msingi hapo natamani tulitazame kwa
makini sana sana, maana kama tusipolitazama kwa makini tunaweza tusielewe
vizuri, na hilo jambo linatuonesha Uhusiano uliopo kati ya Usalama na Ubora wa
Nafsi yako inavyohusiana na Uhai wa Kanisa la Tanzania, Kanisa la Ulimwengu
mzima lakini pia kuanzia na Kanisa la Nyumbani kwako na mahali unapoabudu.
Basi tuutazame huo mstari kwa makini sana sana, kuna maneno
kadhaa ya huo mstari natamani tuyatazame kwa makini …..Hamjui ya kuwa NINYI
mmekuwa hekalu la Mungu….. na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani YENU?.......
Kama MTU akiliharibu hekalu la Mungu,… Mungu atamharibu MTU huyo….. Kwa maana
hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo NINYI.
Maneno niliyoyaweka kwa herufi kubwa yana maana kubwa sana,
Paulo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu anawaandikia Wakorintho akitaka kuwaonesha ni
jinsi gani Uhusiano wa Kanisa unavyotengenezwa na unavyotegemea mtu mmoja
mmoja. Anapozungumzia Hekalu la Mungu anasema ni NINYI au ndilo SISI kama
tukijiweka kwenye nafasi ya Wakorintho na ambayo ni nafasi muhimu lazima
tujiweke hapo ili hiyo nafasi tuichukue kwa Umuhimu mkubwa sana.
Jambo amabalo ni la kulitazama kwa makini kwenye mistari
hiyo ni kwamba inapozungumziwa kanisa basi tunatazama kama Muunganiko wa watu,.
Maana HEKALU LA MUNGU (moja) linajengwa na NINYI (wengi), lakini pia
inawezekana hilo Hekalu la Mungu ambalo ni watu wengi likaharibiwa na MTU yaani
mmoja. Sasa basi kuna jambo la kulitazama tena hapo kwa makini Zaidi, kwamba kama
Hekalu la Mungu linalojengwa na SISI linaweza kuharibu na YULE au WEWE basi pia
linaweza kujengwa na WEWE- Nitalielezea hilo baadae kwa undani.