Showing posts with label Msanii wa Wiki. Show all posts
Showing posts with label Msanii wa Wiki. Show all posts

Tuesday, January 10, 2017

MWIMBAJI WA WIKI - JOSHUA SILOMBA

LEO TUKO NA MCHUNGAJI JOSHUA SILOMBA
Mchungaji Joshua Silomba
Rejoice Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Joshua Silomba: Naitwa Joshua Silomba wakati mwingine huwa naitwa Pastor Joshua kutokana na huduma yangu ya kichungaji.

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Joshua Silomba: Nimeokoka, ninaabudu kanisa la T.A.G Toangoma na pia ninatumika kama Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo (Mchungaji wa Vijana/Sifa na Kuabudu).

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, yaani ulianzaje na wapi ulianzia?

Joshua Silomba: Nakumbuka nilianza kuimba nikiwa mtoto kabisa kule nyumbani Vwawa, Mbozi. Baba yangu alikuwa Mchungaji na familia kwa ujumla ni ya Kikristo hivyo muda mwingi tulikuwa tukiimba nyumbani na kanisani pia hasa kwenye Sunday School. Nilikigundua zaidi kipaji changu cha kuimba nilipoanza kusoma Shule ya Sekondari miaka ya 2000, nilipofika kidato cha pili niliendelea zaidi kugundua uwezo wangu wa kuongoza ibada (kuimbisha), kupiga muziki na pia kutunga nyimbo. Mwaka 2003 nilikabidhiwa rasmi jukumu la kufundisha kwaya ya kanisa la TAG Mji Mkuu nikiwa Morogoro na tangu hapo nimeendelea kumtumikia Mungu katika maeneo yote niliyoyataja hapo juu (Kuongoza ibada, kupiga muziki, kutunga nyimbo zangu binafsi na kwaya na pia kufundisha kwaya na timu za kusifu na kuabudu).

Joshua akiiongoza ibada na sifa kanisani
Rejoice Blog: Katika kuimba kwako, je, umeshatoa albumu yoyote? Majina ya albamu?

Joshua Silomba: Nimewahi kutoa albumu mwaka 2010 iliyoitwa MUNGU WETU HASHINDWI (audio) na kwa sasa nina albumu nyinginei itwayo JAMBO JIPYA (audio) ambayo niliitoa rasmi tarehe 04.12.2016.

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya nyimbo zako ni upi?

Joshua Silomba: Kwa kweli napenda nyimbo zangu zote kwa kuwa kila wimbo umebeba ujumbe maalumu na pia sababu maalumu ya kutungwa kwake. Hivyo, kila wimbo una mguso wa kipekee napozisikiliza na kuziimba pia.

Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je, anakusaidia vizuri?


Joshua Silomba: Kwa sasa sina msambazaji wala mtu anayesimamia kazi zangu, labda kwa hapo baadaye.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Joshua Silomba:    Kwa Tanzania ni wengi wanaonivutia katika muziki wa Injili hususani wanaoimba nyimbo za sifa na ibada. Kwa nje ya nchi kwa sas anapenda sana kumsikiliza na kumfuatilia William McDowell.

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Joshua Silomba: Mafanikio ninayoyaona kwa sasa ni kupanuliwa zaidi kwa wigo wa kihuduma, watu wengi zaidi wanaendelea kunifahamu na kufuatilia ninachofanya katika huduma yangu. Pia naendelea kuwafahamu na kukutana na wadau mbalimbali wa muziki wa Injili kama vile wazalisha muziki (producers), waongoza video (video directors) na waimbaji ambao wananipa changamoto ya kufanya kazi katika ubora na viwango vya hali ya juu.

Joshua Silomba
Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Joshua Silomba: Changamoto ni nyingi ila kwa uchache, nimepata sana changamoto ya kifedha katika kufanikisha malengo yangu ya kihuduma hivyo kufanya kazi zisizona viwango ninavyovitaka, ucheleweshwaji wa kazi studio au kupoteza kabisa (nimewahi kurekodi nyimbo ambazo hadi sasa sijazipata kwa miaka zaidi ya miwili, pia nimewahi kurekodi video ambazo sijawahi kuziona pasipo maelezo yanayojitosheleza). Changamoto nyingine ni kutopata ushirikiano kwa waimbaji wengi waliotangulia kwenye huduma hii ya uimbaji na mwisho, mfumo wa vyombo vya habari wa Tanzania (Redio, TV, nk) hautii sana moyo hasa kwa waimbaji wanaoanza huduma hivyo ziko nyakati ambazo nilikatishwa sana tamaa na mfumo huu.

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina unayoimba wewe?

Joshua Silomba: Muziki wa Injili Tanzania unazidi kukua na changamoto inazidi kuwa kubwa hasa kwa upande wa ubora na viwango. Lakini pia kwa upande mwingine, muziki wetu umeingiliwa sana na mamluki, hivyo kusababisha waimbaji wengi hata wasio na shida kuonekana ni wababaishaji.

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Joshua Silomba: Nashauri waimbaji wanaojisahau na kujichanganya na mambo ya kidunia wajitambue na kurejea kwenye misingi ya Neno la Mungu ambalo linatuongoza kupita katika njia za haki na utakatifu. Zaidi wanatakiwa kutubu na kusimama kwenye kweli ili utumishi wao usiwe bure.

Joshua akiiongoza ibada na sifa kanisani
Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Joshua Silomba: Kama nilivyosema hapo awali, mimi ni Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la TAG Toangoma na nina wajibika zaidi kama Mchungaji wa Vijana na Sifa na Kuabudu (Youth/Worship Pastor). Najishughulisha pia na kilimo, ufugaji na biashara. Pia ni MC kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kikanisa.

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Ndoa na watoto vipi?

Joshua Silomba: Ninaishi Toangoma, Dar Es Salaam. Nina mke (Bertha) na mtoto mmoja (Doreen).

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Joshua Silomba: Tupendane, tuwe na umoja na pia tuishi maisha halisi ambayo yatamtukuza Mungu.

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Joshua Silomba: Waendelee kututia moyo na kutupa ushirikiano tunapotoa nyimbo.

Rejoice Blog: Ahsante sana Joshua Silomba kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Joshua Silomba: Amina! Nawashukuru pia Rejoice Blog kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuibua na kutangaza vipaji vya waimbaji wa nyimbo za Injili. Mungu awainue zaidi ili muwafikie watu wengi.


Kupata zaidi habari za huduma yangu kwa sasa natumia Facebook, page yangu natumia jina Joshua Silomba. Msomaji anaweza ku-like na ku-share na wengine ili waweze kujua habari mbalimbali zinazohusu huduma yangu. Pia YouTube kwa sasa nimeweka wimbo (audio) unaoitwa Jambo Jipya wanaweza kuusikiliza kwa kubofya link HAPA

Mawasilianoi zaidi piga: +255717387212/+255754773512

Mwisho kabisa napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa msomaji kutoa muda wake kufuatilia habari za muziki wa Injili kupitia Rejoice Blog.



~~~ UBARIKIWE ~~~


Tuesday, December 20, 2016

MSANII WA WIKI - SIXBERT MUBILIGI

NDANI YA MSANII WA WIKI HII.... 

Sixbert Mubiligi
Katika Msanii wa Wiki leo tunaye Sixbert Mubiligi kutoka Morogoro

Rejoice Blog: Tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Sixbert: Majina yangu ni Sixbert Eldard Mubiligi, kwenye huduma natumia zaidi Sixbert Mubiligi.

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Sixbert: Mimi nimeokoka kweli kweli; ninaabudu kanisa la TAG - nikiwa Morogoro kwangu ninaabudu TAG Bethel Mwembesongo linaloongozwa na Askofu Mkuu Barnabas Mtokambali. Nikiwa Mtwara naabudu kanisa la TAG Shangani Miracle Temple chini ya Askofu George Musa.

Sixbert Mubiligi katika moja ya Mikutano ya Injili
Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, ulianzaje na wapi ulianzia?

Sixbert: Nimeanza tangu nikiwa mdogo Sunday School Basanza Uvinza Kigoma, na nilipofika umri wa kutosha kuimba na watu wazima niliimba kwaya ya kwanza ya Neema iliyopo Basanza Uvinza, ni kwaya ya kanisa la Anglican. Baadaye nikaja Urambo Tabora na nikaimba kwaya ya ESSACU pale wilayani Urambo. Nilipokuja kwa baba yangu Morogoro nimeimba kwaya ya Safina pale Anglican Magereza Kihonda. Baadae nilipoanza kidato cha kwanza ndipo nilipokutana na wapendwa tukatengeneza bendi iliyoitwa SGS hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa kuingia studio hapo ilikuwa 2005 nikiwa kidato cha tatu na tulifanya kazi kama Maisha bora

Rejoice Blog: Safi sana. Una historia ndefu kwa kweli katika muziki wa Injili. Katika kuimba kwako, je, umeshatoa album yoyote?

Sixbert: Yesu umenipa Heshima  na mwaka 2009 nikiwa kidato cha Sita nilifanikiwa kurekodi albamu yangu iliyoitwa BWANA ATASIMAMA.
Na sasa ninaandaa albamu mpya iitwayo YESU HASHINDWI na albamu ya pamoja kati yangu na rafiki yangu ambae tumeanza nae huduma hii tangu tukiwa sekondari, anaitwa ALFRED MWAKASASA.

Sixbert akiwa na mwimbaji Joshua Silomba
 Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako?

Sixbert: Kazi zangu nasambaza mwenyewe sijapeleka kwa wasambazaji, lakini hizi kazi mbili itabidi nitafute msambazaji. Kwa upande wa usimamizi bado natafuta mtu atakayesimamia au hata kampuni ambayo nitafanya nayo kazi.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Sixbert: Mwimbaji ninavutiwa naya ni Ambwene Mwasongwe na huwa nasikia tu kumfuatilia kazi zake. Kwa kifupi ndiye Fanuel Sedekia wa wakati huu maana anayatunza mafuta ya madhabahu katika uimbaji

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Sixbert: Mafanikio ni mengi cha kwanza uimbaji umenipa digrii Udom  na mengine mengi maana kumtumikia Mungu kuna faida, lakini kubwa zaidi nimepata watu wengi sana ambao ni wa familia ya Yesu Kristo

Sixbert akiwa na waimbaji wengine studio
Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Sixbert: Waoh! Changamoto kubwa ni fedha ambapo huduma hii inahitaji pesa kuliko vile watu wanavyofikiria. Changamoto nyingine ni baadhi ya watumishi utakuta anakuita kwenye huduma wewe binafsi alikuambia mtumishi hali ni ngumu lakini ukifika kwenye mkutano au semina unakutana na muimbaji kutoka Dar ambae anaondoka na bahasha ya laki saba wewe hata mafuta ya gari hupati. Hii kwangu huwa inaumiza hata ungekuwa wewe mwandishi ungeumia

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina unayoimba wewe?

Sixbert: Muziki wa tanzania unakuwa kila siku, na tasnia inang'aa kwa kweli

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Sixbert: Kama umeamua kumtumikia Mungu unatakiwa uwa halisi hapo Mungu atayaachilia mafuta yake juu yako.

Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Sixbert: Mbali na huduma, mimi ni mwalimu wa sekondari Manispaa ya Mtwara pia mjasiriamali 

Sixbert akiwa na mkewe Joyce
Rejoice Blog: Je, umeoa na una watoto?

Sixbert: Yeah mimi ni mume wa mke mzuri Joyce Sixbert. Pia Bwana Yesu katuzawadia Mtoto wa kike  anayeitwa Prettyn.

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Sixbert: Niwaombe watumishi ambao Bwana kawapa kibali cha kuonekana mbele za jamii jitahidini kutamani kuwawezesha wengine ili familia ya wana wa Asafu ikue maana binafsi napenda waimbaji waongezeke kila siku. Na pia tuache ukabila kwenye huduma.

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Sixbert: Ujumbe wangu kwa jamii watusapoti, huduma hii inawahitaji wao ili isonge mbele. Amen

Rejoice Blog: Ahsante sana Sixbert kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Sixbert: Amen, ahsante

Huyo ndiye Sixbert Mubiligi, kijana aliyeanza kumtumikia Mungukwa muda mrefu kupitia uimbaji. Naamini umepata kumfahamu zaidi kwa angalau hatua moja mbele

Kwa mawasiliano na Sixbert kwa habari ya huduma unaweza kumpata kupitia namba 0716552795 au barua pepe mubiligis@yahoo.com


~~~ UBARIKIWE ~~~

Tuesday, December 6, 2016

ELANDRE - MSANII WA WIKI

LEO TUNAYE ELANDRE NA GOSPEL HIP-HOP


Leo katika Msanii wa Wiki tuko wa Gospel Hip Hop ajulikanae kwa jina la ELANDRE. Ni muziki wa aina ya kipekee sana kwenye tasnia ya Muziki wa Injili

Tayari kuna baadhi wanamfahamu kwa kazi zake na wengine hata wamehudumu naye pamoja katika huduma mbalimbali.

Tumebahatika kupata nafasi ya kumfahamu zaidi leo na kujua zaidi kuhusu huduma yake ya Muziki wa Injili kwa namna ya kipekee na pia kuhusu maisha yake binafsi.

Rejoice Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Elandre: Majina yangu kamili ni Emmanuel Andrew Mkumbwa. Kwenye mziki ndo natumia jina Elandre.

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Elandre: Nimeokoka. Na ninaabudu katika kanisa liitwalo Bread of Life ambalo lipo chini ya King’s Touch Ministries. Mchungaji wangu anaitwa Fred Okello, na pia ninahudumu pale kama kiongozi msaidizi wa sifa [kusifu na kuabudu].

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, ulianzaje na wapi ulianzia?

Elandre: Nikiwa kidato cha tano, tulikua na kikundi cha maombi ambapo tulikua tukishiriki kila Jumamosi. Kuna siku mtumishi kutoka Uganda akaja akaibua vipawa vilivyokua vimelala ndani yetu kwa neno la unabii. Haikuchukua mda nikaanza kuandika mashairi, maana alitoa mfano hai kabisa wa hiki kipaji/kipawa na nlikua nakipenda sana kitabu cha Zaburi. Ndipo nilipoitolea wimbo wangu wa kwanza uitwayo Praise The Lord [Psalm 150]. J 

Rejoice Blog: Sawasawa. Katika kuimba kwako, je, umeshatoa album yoyote?

Elandre: Nimetoa album moja inayoenda kwa jina PROJEKT THREE6TEEN inayopatikana pia mtandaoni kwenye soundcloud hapa na pia reverb nation hapa.

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya nyimbo zako ni upi?

Elandre: "Elijah" ambao nimemshirikisha mwanadada kutoka Zambia aitwae Tasila Mwale.

Rejoice Blog: Ni kwa sababu gani unaupenda wimbo huo zaidi?

Elandre: Wimbo huu una miondoko ya ki-Afro pop ukichanganywa na rap. Nilitumia mda mfupi sana kuundika na kwa uhai ulionao, huwagusa wengi wanaousikia na kuisikiliza meseji iliyomo ndani. Nahisi pia naupenda kwa sababu unachezeka.

Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je, anakusaidia vizuri?

Elandre: Hamna anayesambaza kazi zangu. Natafuta sana mtu atakaenisaidia kuifanya hii kazi.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Elandre: Lecrae ambae ni msanii kutoka Marekani, nahisi ndio the most successful Christian Rapper kwa sasa. Ana bidii sana katika kuifanya kazi ya Mungu kupitia kipaji alichopewa.

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Elandre: Tangu mwaka 2007 nilipotoa singo yangu ya kwanza mpaka sasa mafanikio nliyoyapata katika kuimba nyimbo za injili ni pamoja na kutengeneza connections na wasanii wengine kutoka nje ya Tanzania, baraka za afya tele na uhai, na mpaka sasa tunaendelea vizuri. Najua mafanikio ya kifedha yanakuja hivi punde.

Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Elandre: Kupenya katika hili soko letu la Tanzania ndo imekua ni changamoto kubwa sana kwangu, pia kwa watenda kazi wenzangu tunaofanya nao muziki kama huu. Vyombo vya habari haviukubali na kuuchukulia huu mziki kama fursa. Maana naamini kwamba sisi sio wasanii tu, ni zaidi ya wasanii na miziki yetu ina uhai na nguvu za kiMungu maana Mungu anaishi ndani yetu. Pia changamoto nyingine imekua kumpata msimamizi wa kazi zangu, nimekua nikifanya karibia kila kitu peke yangu. Bado najifunza mengi na nitaendelea mpaka kieleweke maana huwezi jua labda nimeitwa kua msimamizi wa wengine wanaokuja nyuma yetu.

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina unayoimba wewe?

Elandre: Bado tunakua. Bado njia haijawa wazi. Bado wasanii wengi hawajielewi na kwa sababu hiyo huenenda katika njia za wasanii wengine wasio wakristo/wa nuruni. Kujitambua kumekua ni changamoto kubwa sana, nahisi pia ni kwa sababu wengi hawajatulia na kuketi chini ya mchungaji mmoja atakaekuza, na kukiendeleza kile kilichomo ndani yao. Muziki huu bado unakua, kwa nionavyo mimi bado uko katika steji za utotoni, unahitaji maziwa na malezi zaidi ili kukua. Lakini ukikua utaleta mabadiliko makubwa sana katika miziki ya Injili hapa nchini. 

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Elandre: Warudi kundini. Mafanikio yako ndani ya Kristo Yesu pekee. Shida kubwa ni kutolitii Neno la Mungu, na kuwa na ushirika na Roho Mtakatifu. Lakini tungekua waaminifu katika hili, tusingetoka nje kwa nia ya kutafuta hela au maisha. Sisi ndo tungekua tunafuatwa na waduniani kujua nini wafanye ili wafanikiwe. Nimeji-include na mimi katika hili swala la uaminifu maana nahisi ndo “key factor” katika hili suala.

Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Elandre: Tofauti na mziki mimi ni Graphic Designer.

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Ndoa na watoto vipi?

Elandre: Bado bachela. Ndoa bado. Mungu akipenda mtasikia shangwe hivi karibuni. J

Rejoice Blog: Safi sana. Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Elandre: Tuutafute uso wa Mungu. Hapo ndipo mafanikio yalipo. Pia tupendane jamani, tuombeane badala ya kupigana mawe. Sisi ni familia moja, inabidi dunia itutazame sisi kama mifano hai. Hamna alie mkamilifu kwa hiyo tuinuane pale mmoja wetu anapoanguka.

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Elandre: Wazidi kutuombea sana.

Rejoice Blog: Ahsante sana Elandre kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Elandre: Asante sana hata kwa hii fursa mlinipa na kuniheshimu. Much love kwenu na nnawatakia mafanikio makubwa katika mwaka ujao, muwe the top blog hapa Tanzania na chombo chenu kizidi kukua mje kukamilisha ndoto zenu pia.

Rejoice Blog: Ameen

Unaweza kuwasiliana na kumpata Elandre kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, na pia kumwalika kuhudumu kwenye shughuli mbalimbali za kumtukuza na kumwinua Mungu... vilevile kushirikiana naye katika kukuza kazi za sanaa katika Injili hapa nchini na duniani kote

Elandre: Social media handle yangu ni @iamelandre yaani hii inatumika kote Facebook, Twitter, Instagram na Youtube [Ukitaka kuona video zangu]

Album yangu iko kwenye link hizi: www.soundcloud.com/iamelandre au www.soundcloud.com/projekt316
www.reverbnation.com/iamelandre

Huo ndiyo mwanzo wa kufahamu zaidi kuhusu Elandre, kuna mengi mengine kuhusu kazi zake za Injili kupitia muziki wa HipHop na shughuli zake nyingine. Usikose kuendelea kufuatilia kipengele hiki cha Msanii wa Wiki kila wiki siku ya jumanne kupata kuwafahamu zaidi wasanii wanaomtukuza Mungu kupitia kazi mbalimbali za sanaa, hususani Muziki wa Injili hasa hapa nchini Tanzania.

Ikiwa unapenda tufanye mahojiano na Msanii fulani wa Injili hapa nchini Tanzania,au ikiwa wewe ni msanii wa muziki au sanaa yoyote katika Injli na ungependa kutambulisha zaidi kazi zako, basi usisite kuwasiliana nasi kwa njia ya simu (call, text, whatsapp) kupitia namba 0714484504 (Alex). Ubarikiwe sana!

 ~~~ TUKUTANE WIKI IJAYO! ~~~

Tuesday, November 29, 2016

MSANII WA WIKI - LEMBO JR

LEO KATIKA MSANII WA WIKI - EMMANUEL LEMBO JR

Rejoice Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Lembo Jr: Jina langu ni Emmanuel Stephen Lembo, ila katika huduma nafahamika kama Lembo Junior
Lembo Jr

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Lembo Jr: Nimeokoka nampenda Yesu, kwa sasa naabudu NAIYOTH CHURCH - GEITA

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, yaani ulianzaje na wapi ulianzia?

Lembo Jr: Naweza sema,nilianzia utotoni sundayschool kids choir...ila kuingia rasmi kwenye tasnia hii mpaka kuanza kusikika kwa medias ni 2007-2008 nikiwa UDOM

Rejoice Blog: Katika kuimba kwako, je, umeshatoa album yoyote? Majina ya albamu?

Lembo Jr: Mpaka sasa niko na 4 albums ila tatu ndizo zajulikana 1.TUTEMBELEE. 2 USIFIE JANGWANI. 3.UWE KILA KITU. 4.WINGU LIMESIMAMA WAPI

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya nyimbo zako ni upi?

Lembo Jr: mmmmmmh ni almost nyimbo zote nazipenda maana kila wimbo najua Mungu alinipaje ILA UWE KILA KITU, TUTEMBELEE NA USIFIE JANGWANI ni zaidi

Lembo Jr
Rejoice Blog: Ni kwa sababu gani unaupenda wimbo huo zaidi?

Lembo Jr: Nyimbo zina ushuhuda mkubwa sana sikuzipewa hivi hivi, nilipitishwa sana sanaaaaa

Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je, anakusaidia vizuri?

Lembo Jr: Kwa sasa niko na Madam Gisela Malisa, yuko vyema

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Lembo Jr: Sipho Makhabane, Emmanuel Mgogo

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Lembo Jr: Yako mengi sana kiroho na kimwili. Kiroho; nimekua nikipokea shuhuda nyingi sana namna nyimbo zangu zimeokoa, zimeponya na kuganga NAFSI zilizokia zimejeruhiwa.  Kimwili kuna kupata kipato ingawa si kikubwa, ila MUNGU ni mwema. Na pia nimepata EXPOSURE kubwa sana ndani na nje ya mipaka ya Afrika
Lembo Jr

Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Lembo Jr: Changamoto ni nyingi sanaaaa kiroho na kimwili pia kimwili zaidi ni PESA, nitatizo kikubwa, kiroho vita ni KUBWA sana

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina unayoimba wewe?

Lembo Jr: Muziki huu naona kwa upande wangu uko vyema maana haujaniangusha

Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?

Lembo Jr: Kikubwa ni kurudi kwenye kusudi la MUNGU na kulitumikia Shauri la Bwana

Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Lembo Jr: Kitaaluma nina Bachelor Degree ya Public Administration (Shahada ya Sanaa katika Utawala wa Umma), ingawa sijaajiriwa, ninafanya biashara zangu ndogo ndogo

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Ndoa na watoto vipi?

Lembo Jr: Naishi na familia yangu Geita, niko na mtoto mmoja tu

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Lembo Jr: Ujumbe TUIFANYE KAZI YA MUNGU KWA UNYENYEKEVU MKUU SANA

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Lembo Jr: Waendelee kutusapoti kwa hali, mali na maombi.

Rejoice Blog: Ahsante sana Lembo Jr kwa muda wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Lembo Jr: Nami NIWASHUKURU SANA SANA KWA MUDA WENU NA KUJALI KWENU MUNGU AWABARIKI SANAAAA

Huyo ndiye Emmanuel Stephen Lembo a.k.a Lembo Junior ambaye umepata kumfahamu zaidi kupitia Msanii wetu wa Wiki. Ukitaka kuendelea kufuatilia habari zake na kazi yake ya huduma, mpate kwa njia zifuatazo:

Emmanuel Lembo Jr:
Instagram: @lembojr
Facebook: Lembo Jr Emmanuel

~~~ UMEBARIKIWA! ~~~