Monday, November 21, 2016

MAOMBI YA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO - SEHEMU YA 2

Na Mchungaji Florian Katunzi


Bwana asifiwe mtu wa Mungu, bado naendelea na mtiririko wa somo hili ambalo ninaamini litafanyika msaada kwako na hata kwa jirani yako. Pia napenda kukumbusha ya kuwa kitabu hiki kitatoka siku chache zijazo hivyo jiandae kukipokea.

Wiki jana tuliangalia utangulizi wa somo hili ambapo nilikufundisha juu ya habari za Mfalme Nebukadreza aliyekuwa kiongozi wa dola yenye nguvu sana ya Ukaldayo na pia alikuwa muabudu miungu. Mara  baada ya kifo chake Mungu alimuinua Mfalme Koreshi ambaye alikuwa mpakwa mafut wa BWANA na alifanya makusudi yote ambayo Mungu aliyaweka.

Leo tutakwenda kuangalia juu ya aina tano za funguo za kufungua malango na milango.  Endelea…………

AINA TANO ZA FUNGUO ZA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO;

UFUNGUO WA KWANZA

1: NENO LA MUNGU
    Neno ni kauli ya Mungu yenye Mamlaka, Uweza na Nguvu za ki-Mungu zenye kuleta mageuzi ya kiroho na kimwili.

Yesu Kristo alithibitisha yakuwa Neno la Mungu lina mamlaka na nguvu pale alipolitumia kufungua mafungo yaliyofunga watu wa Mungu sawasawa na injili ya Luka 4:36 “Mshangao ukawashika wote, wakasemezana wakisema, ni Neno gani hili, maana awaamuru pepo wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka.”

Tunajifunza pia kwa Neno vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana viliumbwa maana Mungu aliziumba mbingu na nchi kwa Neno lake. Alisema iwe na ikawa.

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Yohana 1:1-5 

Tukitaka kufungua malango na milango iliyofungwambele yetu sharti kwanza tuwe na ufunguo wa Neno la Mungu. Maana Neno ni taa na nuru ya maisha yetu. Aliye na Neno haendi gizani kwa sababu kwa Neno la Mungu hakuna lisilowezekana.
“Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” Luka 1:37

Neno la Mungu kamwe halipiti hivyo tukilishika Neno kila lango na malango hakika yatafunguka. “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe” Mathayo 24:35
Neno lake husimama katika kweli daima. Neno la Mungu huja kwetu likiwa hai, likifungulia imani yetu.
“Ndipo BWANA akaniambia… naliangalia neno langu, ili nilitimize” Yeremia 1:12


UFUNGUO WA PILI

IMANI
Imani sikuzote imekuwa ndiyo alama ya wanafunzi wa Yesu. Wanafunzi wa kwanza walijulikana kama WAAMINI. Yesu alisema “… Yote yawezekana kwake aaminiye” Mark 9:23

Imani humaanisha kumtegemea Mungu kwa hali zote. Wakati Adamu alipofanya dhambi, alijitoa katika kumtegemea Mungu na kujitegemea (ambako ni kutokuamini). Hii ndiyo sababu Mungu ameweka kipaumbele kwenye imani. Imani ni njia ya kuturudishia uhusiano na Mungu (kumtegemea Mungu). “Basi Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Warumi 10:17 

Tunajifunza yakuwa pasipo Neno la Mungu hakuna imani ya ki-Mungu. Maana yake ufunguo wa kwanza ndiyo unaotupeleka kwenye ufunguo wa pili.

Kumtegemea Mungu ndiko kunakoitwa imani. Kwa imani unatoka kwenye kutokuweza hadi kuweza. Kwa imani hakuna lisilowezekana.

A: IMANI NI NINI?
    Imani ni tendo la utii katika kuitikia kile Mungu alichokisema katika Neno lake.
Imani ya kweli inaelezewa katika Utii na Kutenda kulingana na  Neno la Mungu.
“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” Waebrania 11:1
Hivyo pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu; kwa maana kila mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, naye huwapa thawabu wale wamtafutao sawasawa na Neno lake. Ni lazima tumtafute Mungu kwa juhudi na kutamani kwa bidii uwepo wa neema yake.
Imani na utii haviwezi kutengana kama vile ambavyo kutokuamini na kutokutii kusivyoweza kutengana. “Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; hawakuigopa amri ya mfalme. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabiwa ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. Kwa  imani akatoka Misri asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”  Waebrania 11:23-27

B: KWELI TATU ZA IMANI
     Msingi wa kuwa na imani kwa Mungu uko katika kweli tatu muhimu:

Asili ya Mungu;
  
a.     Hawezi Kubadilika.
“Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu..” Malaki 3:6

b.     Hawezi Kushindwa
“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na yakuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika” Ayubu 42:2

c.      Hawezi Kudanganywa
“Mungu si mtu, aseme uongo; wala si mwanadamu ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?” Hesabu 23:19   
Kristo amefanyika chanzo cha imani yetu kwa Mungu. Ukweli kuhusu kifo chake na ufufuko hutoa msingi wa kuamini kwetu.
“Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi” 1Wakorintho 1:30

Ili imani itende kazi ya kufungua malango na milango katika maisha yetu, ni lazima kutii Neno la Mungu. Imani HUTENDA KAZI pale mtu aliyeamini anapofanya sehemu yake kwa imani, hiyo humfanya Mungu naye kutenda sawasawa na kuamini kwa mtu. Angalia mfano wa mwanamke aliyekuwa na msiba wa kutokwa damu muda wa miaka kumi na miwili, aliposikia Neno la uponyaji kupitia Kristo Yesu aliamini na kuadhimia moyoni mwake kumwendea Yesu Kristo kwa imani ili apate kufunguliwa. “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi namiwili alikuja kwa nyuma, akagusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.” Mathayo 9:20-21

Matokeo ya imani sikuzote mwisho wake ni ushindi kwake yeye aaminiye na kumletea utukufu wa Mungu katika maisha yake ya kiroho na kimwili. “… kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu” 1Yohana 5:4


Itaendelea……………………..

Wednesday, November 16, 2016

KUJAMIIANA, UASHERATI NA USAFI - MCHUNGAJI YARED DONDO, TAG CITY HARVEST CHURCH


Pastor Architect Yared Dondo - TAG City Harvest Church
 Upendo wa Kweli Hungoja – Waebrania. 13:4

Mpango wa Mungu kuhusu kujamiiana unahusisha mwanaume mmoja na mwanamke mmoja walio ndani ya uhusiano wa ndoa. Serikali na dunia kwa ujumla hutumia mamilioni ya fedha kwa kinaitwa “ngono salama”. Hakuna ngono salama zaidi ya iliyo ndani ya mpango wa Mungu!
Tafsiri ya kidunia kuhusu ngono salama haijaegemea kwenye maadili hata kidogo. Mawazo yao ni kuwa: “ikiwa hauwezi kuenenda vyema, basi kuwa mwangalifu”.
Tafsiri ya Mungu wa ngono salama ni kungoja mpaka ndoa.
1 Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho”

Maadili ya Kibiblia huchekwa, hudharauliwa husemwa ni ya kale na yamepitwa na wakati.
Ninashukuru kwa ajili ya viajana matineja wachache ambao leo wanasema, kuanzia leo na kuendelea, nitangojea mpaka wakati wa ndoa….. nitaishi sawa na mpango wa Mungu….. na watu wazima wanaojitoa tena kuwa wasafi na waaminifu. Tumeliruhusu neno ngono/kujamiiana kuwa neno chafu. Kilichopaswa kuwa taswira njema ya upendo, ndoa na maskani, kwa sasa kinahusishwa na upotovu/ukimwi/ukahaba/usagaji/ngono ya jinsia moja.
Jamii inajifunza kwamba kuna adhabu ya uasherati na uzinzi. Lakini badala ya kurejea kwenye viwango vya Mungu na kutii sheria za Mungu, jamii husema “wacha tuone tunachoweza kufanya kukwepa matokeo ya matendo yetu”
Hapa ndipo hatari iko: ikiwa utaingia kwenye uhusiano wa kimwili kabla ya ndoa:

Hatari 5 za ngono kabla ya ndoa:

1.             Pendo bandia
Mahusiano yaliyojengwa juu ya ngono hayadumu! Mkianza na mambo ya kimwili mtajikuta hata hamvutiani. Hamtakua pamoja kiakili, kihisia au kiroho!
Upo hapo ukiwa hauna kitu isipokuwa malai/krimu iliyochapika na inazeekana ambayo utaitupa pia! Lakini…ikiwa kujamiiana kutaanza baada ya ndoa, sehemu nyingine tatu zitaendelea kukua pia! Hivyo unakuwa na siyo tu mshirika wa kujamiiana, bali pia rafiki bora zaidi anayekupenda.
Upendo wa kweli huvumilia, ni halisi na hauna ubinafsi.
Wasichana, pale mwanaume anaposema “Siwezi kusubiri”, utajua kwamba hakupendi. Pale anaposema “Ikiwa wanipenda kweli, nithibitishie”, chukulia hilo kuwa tusi na umchape kibao cha nguvu kiasi cha ubongo wake kupiga kelele kama kengele za kanisa wakati wa asubuhi yenye baridi!

Hatari za upendo wa bandia..

2.             Madhara kihisia

Mabinti wadogo:
Tafiti zinaonyesha uhusiano wa moja kwa moja baina ya ngono kabla ya ndoa na matatizo binafsi ya kihisia… Kujihisi mkosaji/wasiwasi/kupoteza kujiheshimu
Kujihisi una hatia ndiyo hisia inayoweza kutuharibu zaidi.
Hukukosesha usingizi, amani, furaha, kujithamini na uhusiano wako na Mungu.
Hukuacha umevunjika vunjika, ukiwa hauna uhakika na kutoweza kuzalisha matunda.
Na kisha hupoteza ule “mng’ao” unaoambatana na usafi.
Sikieni haya mabinti, na nitawaambia namna wanaume hufikiri…
…..kuna fumbo fulani kuhusu yasiyojulikana. Kuna kitu fulani cha kuvutia sana kuhusu yasiyojulikana.
Mara tisa kati ya kumi, pale unapojifunua kwa mwanaume, baada ya fumbo kuondoka, naye pia huondoka….atakudondosha kama jiwe la moto! Na haitakuwa kama kuachana kwingine kokote, itakuwa kama kupewa talaka.

3.             Madhara ya Kimwili

Bado mshahara wa dhambi ni mauti!
Kuwa mchafu – uko katika hatari ya magonjwa yasiyo na tiba. Kuna magonjwa saba, nje na ukimwi ambayo hayana tiba na yote yamebeba madhara ya muda mrefu, na yote huenea na huhusiana na kundi la watu walio tayari kufanya ngono nje ya usalama wa ndoa!
Utasema yuko tayari kuwa nami pekee. Usijihakikishie hivyo! Ikiwa wako tayari kufanya ngono nawe, basi wako tayari pia kufanya na wengine, na huenda wamekwisha kufanya hivyo tayari.
Unapolala na mtu, unalala na historia nzima ya ngono ya mtu huyo na KILA MTU ambaye amepata kuwa naye.
Mshahara wa dhambi bado ni mauti.

Hatari ya upendo bandia, madhara ya kimwili na kihisia…

4.             Madhara katika ndoa

Nimewashauri watu ambao wamekuwa wakisema “ni swa kwetu kufanya ngono kwani tunajua tutaoana”. Hapana, si sawa…. Kwa nini?
Kwa kuwa Mungu amesema si sawa…. Nani atakaye kubadili sheria yake? Inawezekana usionane naye!
Kwa wastani, kijana tineja hupenda takribani mara 10 kabla ya kuingia katika ndoa
Hivyo, hata ikiwa umeonana naye, umepunguza nafasi za kuwa na ndoa yenye furaha kwa kuwa umemegua msingi wa uaminifu. Kwenye akili yako, siku zote kutakuwa na lile wazo kuwa mtu uliyeoana naye anauwezo wa kuwa mdanganyifu. Waliweza kufanya dhambi nawe kabla ya ndoa, wanaweza kufanya dhambi dhidi yako sasa baada ya kuoana.

Kisha kuna…

5.             Madhara ya kiroho

Lakini Mchungaji, hauamini kuwa Mungu husamehe? NDIYO, NINAAMINI!
Lakini msamaha na madhara ni mambo mawili tofauti. Huwa tunadhani mambo yote mawili yanaishi kwenye mstari mmoja, kuwa tunapousogolea zaidi msamaha ndivyo tunakuwa mbali na madhara… siyo hivyo!
Daudi alifanya dhambi na Bathsheba na kisha akafanya amauaji…na katika vifungu viwili vya ajabu vya Biblia tunaona msamaha wa hali ya juu ambao Daudi aliomba na kupokea – lakini ngoja niulize, madhara hayakuendelea kuwepo?
Ndiyo. Mungu akasema, “Daudi, utaishi katika bonde la machozi maisha yako yote. Upanga hautaondoka nyumbani mwako”
Alimzika mwanae aliyefariki. Kisha mwanaye mmoja akambaka bintiye. Na Mungu akasema ni matokeo ya moja kwa moja ya dhambi zake.

Namna gani ubakie safi?
1.             Linda ufahamu wako
Mlango wa macho na mlango wa masikio ni muhimu sana…. Ni barabara kuu ya ufahamu.
2 Petro 2:14 “macho yaliyojaa uzinzi”
Wanaume, lindeni macho yenu. Biblia inasema (Zaburi 101:3) “Sitaweka mbele ya macho yangu neno la uovu”. Dai mstari huo
Ayubu alisema “Nilifanya agano na macho yangu, basi nawezaje kumwangalia msichana kwa kumtamani?” jiweke mbali na muziki ambao maudhui yake ni tamaa ya kingono.

2.             Usiatamie dhambi

Ikiwa huwezi kuingia duka la videa na kusalia msafi, usiingie kabisa!
Ikiwa huwezi kuperezi kwenye vituo vya televisheni pasipo kutazama kitu kichafu, basi zima kabisa. Ikiwa hamwezi kuwa peke yenu kwenye gari, basi msikae peke yenu.
“Usiupe mwili nafasi”

3.             Azimia kabla

Fanya maamuzi ya awali kubakia msafi, na kuwa hutaingia kamwe kwenye uhusiano na mtu ambaye hajafanya maazimio kama hayo.
Maneno ya mpumbavu: “Atabadilika mara tutakapooana”
Wewe unasema: “Nimechelewa mno mchungaji” (Tayari nimeshatoa)
Habari njema! Siku moja mwanamke aliletwa kwa Yesu, akiwa ameshikwa akifanya uzinzi. Alitarajia kuhukumiwa, lakini Yesu akamwambia, Sikuhukumu, enenda zako na usifanye dhambi tena!


Huwezi kubadili yaliyopita, lakini mustakabali wako waweza kuwa bila madoa!

Tuesday, November 15, 2016

MSANII WA WIKI - FRIDA FELIX

LEO TUPO NA....
Frida Felix

Leo katika Msanii wa Wiki tuko na binti anayechipukia katika Muziki wa Injili, Frida Felix.

Tayari kuna baadhi wanamfahamu kwa kazi zake za utambulisho na wengine hata wamehudumu naye pamoja katika huduma mbalimbali.

Leo tumebahatika kupata nafasi ya kumfahamu zaidi na kujua zaidi kuhusu huduma yake ya Muziki wa Injili na kuhusu maisha yake binafsi.

Frida Felix
Rejoice Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Frida: Jina langu ni Frida Felix na situmii jina lolote tofauti kwenye muziki

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Frida: Ndiyo nimeokoka, na ninaabudu katika kanisa la TAG City Harvest

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, yaani ulianzaje na wapi ulianzia?
Frida: Nilianzia Sunday School nikiwa bado mdogo. Nilianza nikiwa Songea kanisa liitwalo Redeemed Assemblies of God; nilikuwa nikiabudu hapo na kuimba kwaya ya watoto.


Rejoice Blog: Katika kuimba kwako, je, umeshatoa album yoyote?

Frida: Nimetoa single mbili mpaka sasa, albamu bado kidogo. Single ya kwanza inaitwa “Neno” na ya pili inaitwa “Watawala”

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya hizo mbili ni upi?

Frida: Naupenda zaidi “Neno”

Rejoice Blog: Ni kwa sababu gani unaupenda wimbo huo zaidi?

Frida: Kwa sababu huu ni wimbo ambao namuomba Mungu anifundishe njia zake na aniongoze kwa Neno lake ambalo ni msingi wa maisha yangu kama mwamini.

Frida Felix
Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je, anakusaidia vizuri?

Frida: Sijaanza mambo ya usambazaji kwa kuwa sijatoa albamu. Pia kwa sasa najisimamia mwenyewe. Nilipotoa singles nilipeleka redioni na pia watu walizipata kupitia mitandao kwenye SoundCloud, Mkito na Mdundo.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Frida: Napenda sana kundi la Joyous Celebration la Afrika ya Kusini, pia Mary Mary na Tasha Cobbs.

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Frida: Kuimba nyimbo za Injili kumeimarisha sana uhusiano wangu na Mungu kwa sababu najihisi karibu zaidi na Mungu ninapomwimbia. Kama mwimbaji wa nyimbo za Injili inabidi usome sana Neno la Mungu na kuomba sana.

Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Frida: Changamoto nilizokutana nazo hasa ni za kiuchumi. Kwa sababu kuingia studio nzuri na kurekodi nyimbo kunahitaji fedha, kufanya video, promo ya nyimbo pia kunahitaji fedha.

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania?

Frida: Kwa kweli unakua siku hadi siku, na unabadilika kwa sababu kila siku Mungu anaibua waimbaji wapya na wazuri.


Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mamba ya dunia hii?

Frida: Mungu hadhihakiwi. Apandacho mtu ndicho atakachovuna!


Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Frida: Mimi ni Legal Officer, kitaaluma ni mwanasheria, kwa hiyo najihusisha na na mambo ya sheria ambayo ndiyo taaluma niliyoisomea

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Umeolewa au bado?
Frida: Bado sijaolewa na sina watoto

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Frida: Wautafute uso wa Mungu, maana jukumu letu kubwa ni kuokoa roho za watu waliopotea kupitia huduma zetu

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Frida: Waendelee kusikiliza nyimbo za Injili maana kuna uwepo wa Mungu katika nyimbo hizo.


Rejoice Blog: Ahsante sana Frida Felix kwa muda wako na kwa ushirikiano wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Frida: Amen. Ahsante sana. 

Frida Felix
Huyo ndiye mwanamuziki wa Nyimbo za Injili Frida Felix tuliyenaye kwa siku ya leo katika segment ya "Msanii wa Wiki" ambaye kwa sasa nina imani utakuwa umemfahamu hatua moja zaidi.

Fridah pia ni mwimbaji wa kundi la Kusifu na Kuabudu la kanisani kwake, liitwalo The City Shakers.

Unaweza kutazama wimbo wake wa “Neno” YouTube hapa na “Watawala” hapa

Waweza kupata pia nyimbo zake katika audio katika mitandao kwenye SoundCloud, Mkito na Mdundo

Kwa mawasiliano ya moja kwa moja na Frida Felix, mpate katika Social Networks za Instagram, Twitter, Facebook kwa @fridafelixofficial na pia waweza kumpata kwa simu namba 0712 093 696

Mungu akubariki msomaji wangu, tukutane wiki ijayo ili kumfahamu msanii mwingine wa muziki wa Injili. Ahsante

GLOBAL FAMILY GATHERINGS BRINGS TO YOU "UNLIMITED BREAKTHROUGH" - ARUSHA 18TH DECEMBER

A life transforming and changing encounter this Friday at Corridor Springs in Arusha with Servants of God, Apostle Shemeji Melayeki (Arusha) and Geofrey Kingu (Dar es Salaam)

Geofrey Kingu (Dar es Salaam)
Shemeji Melayeki (Arusha)