Na Mchungaji Florian Katunzi - EAGT City Center
Wiki jana
nilikufundisha juu ya aina za funguo za kufungua malango na milango, ambapo nilikwambia
zipo aina tano na nikakufundisha funguo mbili kati ya hizo. Funguo ya kwanza
ilikuwa ni Neno la Mungu na ya pili ilikuwa ni Imani.
Nilikwambia ya
kuwa neno la Mungu ni kauli ya Mungu yenye Mamlaka, Uweza na Nguvu za ki-Mungu
zenye kuleta mageuzi ya kiroho na kimwili. Pia nilikuonesha maandiko ambayo
yanathibitisha hilo.
Katika
kipengele cha imani ambacho ndicho tunachoendela nacho siku ya leo,
nilikufundisha maana halisi ya imani na nilisema Imani ni tendo la utii katika kuitikia kile
Mungu alichokisema katika Neno lake.
Nilizama
zaidi na kukuonesha msingi wa kuwa na
imani kwa Mungu ambao uko katika kweli tatu zilizobebwa na maana halisi ya
Asili ya Mungu wetu. Kweli hizo ni Hawezi Kubadilika, Hawezi Kushindwa na Hawezi Kudanganywa.
Endelea……….
Malango na
Milango ni sharti ifunguliwe kwa Imani; sawasawa na Neno la Mungu. Kwa Imani
tunalegeza viuno vya wafalme, Kwa Imani tunalegeza mafungo na vifungo
vilivyowafunga watu wa Mungu. Kwa Imani tunafungua Malango na Milango
iliyofungwa mbele yetu.
“Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na
nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Isaya
10:27
Kila mzigo
uliotwishwa katika nafsi yako unaondolewa begani mwako maana uwezo wake Kristo
Yesu sasa umedhihirishwa ili kazi zote za yule mwovu shetani zivunjwe ndani mwa
imani.
“Kwa maana
vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo, nao wameleta
habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama
kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.” Zekaria 10:2
Imani ni
Ufunguo wa kufungua Malango na Milango,
tunaona Senakeribu analeta majeshi yake akiwa ameazimia kupiga watu wa Mungu na
kuwatawala. Mfalme Hezekia akasema na
watu wake ili apate wakuwajenga Kiimani.
“Iweni hodari, na wa moyo mkuu, msiogope, wala msifadhaike kwa sababu
ya mfalme wa Ashuru, wala kwa majeshi yote walio pamoja naye; kwa maana yupo
mkuu pamoja nasi kuliko aliye pamoja naye, kwake upo mkono wa mwili, ila kwetu
yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu
wakayategemea maneno ya Hezekia mfalme wa Ashuru.” 2Mambo ya
Nyakati 32:7-8
Adui anakuja na
neno lenye kuogofya ili kuifisha Imani yako, Senekarabu anatuma watu wenye
kuhubiri hofu kwa kueleza historia ya Hezekia ya udhaifu.
Senekerebu
anatuma watu wake wageuze neno la Mfalme Hezekia ili apate kuifisha Imani yao
apate kuwapiga. Hezekia anataka kuonyesha waziwazi tofauti kati ya mkono wa
mfalme wa Ashuru na mkono wa BWANA.
Nasi kanisa
lazima tutambue ya kuwa kwetu upo mkono wa BWANA wenye nguvu ya Kuokoa na
Kuponya hivyo lazima tusimame kwa Imani ndipo tupate kufungua Malango na
Milango iliyofungwa mbele zetu, Maana pasipo IMANI haiwezekani kumpendeza
Mungu. Kwa imani yote yanawezekana katika Kristo.
Imani ni chanzo
kikuu cha kupokea kutoka kwa Mungu maana hakuna neno lolote lililo gumu la
kumshinda Mungu aliye hai.
Mwanamke huyu
aliteseka pamoja na kuteswa na mengi lakini kwa IMANI alipata kupokea Uponyaji
baada ya kusikia Neno la Yesu Kristo lenye nguvu ya Kuponya. Hivyo kwa imani
Wagonjwa wataponywa na kupata afya tena.
Wakati mwanamke
yule anashika pindo la vazi la Yesu Kristo, nguvu zilizomtoka Yesu Kristo,
ndizo zilizokwenda kufanya uponyaji kwa mwanamke huyu kwa Imani, hivyo ni
dhahiri pasipo Imani hakuna nguvu ya Mungu kuingia na kuponya. Unaweza kuguswa
na Watu au Watumishi wa Mungu na usipone lakini ukiamini kabisa na usione shaka
moyoni mwako hapo ndipo utakapo pokea.“Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako
ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu,
utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kkwa kinywa
hukiri hata kupata wokovu.” Warumi
10:9-10
Imani yetu
katika Yesu Kristo Yesu sharti ivuke mipaka iliyowekwa mbele yetu, maana kwa
Imani BWANA anasema,
“Nitakwenda
mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza, nitavunja vipande vipande
milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma.” Isaya 45:2
WATU WANAWEZA
KUKUCHEKA KWASABABU YA IMANI YAKO KATIKA MUNGU, usiogope vicheko vyao bali kaza
roho kwa Imani maana lipo Jibu kwa kuwa Mungu hufungua njia mahali pasipo kuwa
na njia. Angalia mfano huu wa ufunguo wa imani; “
“Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu
kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani
kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, aliposikia lile neno likinenwa,
akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane
naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa
yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo
makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana
hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote,
wakamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia
ndani alimokuwambo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha,
kumi, tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana,
akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa
mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile, akaamuru apewe chakula.” Marko 5:35-43
Katika msiba
Yesu anaangalia imani ya yule mkuu wa Sinagogi ili apate kutenda muujiza. Kwa
maana Imani ahitaji ushabiki wa watu bali Imani inahitaji mtu mwenye kujua Neno
la Mungu na kuliamini. Watu walimcheka Yesu Kristo pale aliposema mtoto hajafa
bali amelala, Yesu akamwamsha, akamwambia kijana amka naye akawa mzima. Vivyo
hivyo inawezekana upo kwenye ndoa miaka mingi hujapata mtoto, Kwa Imani tumbo
lako lifunguliwe milango yake na upate watoto wa kiume na wakike.
“Kwa Imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba,
alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa
mwaminifu.” Waebrania
11:11
SARA alipoambiwa
atabeba mimba na kuzaa aliona ni kichekesho kwake maana alikuwa mzee. Hali
halisi ya mwili wa Sara ilimfanya apoteze imani ya kuzaa. Wako watu wengi wa
Mungu wanaopishana na Baraka zao toka kwa BWANA kwa sababu ya kuhesabu miaka ya
mapito yao na kuona Mungu amechelewa na kinachozaliwa ni kukata tamaa kwa mfano
wa Sara. “Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara
alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni
mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA
akamwambia Ibrahimu, mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana,
nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake
nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.” Mwanzo
18:11-14
Katika mambo
yote Mungu hufanya kazi na wenye Imani ili apate kuwapatia Mema kwani ndio wale
walioitwa kwa kusudi lake, Sisi tu watoto wa Mungu basi sasa tu warithi wa
Baraka na Ustawi wa Kimungu, turithio kwa Imani pamoja na Kristo Yesu. Imani ni
kutarajia yasiyowezekana kutarajiwa.
SARA alimpokea
Isaka katika hali ya kutokutarajiwa kwani alikuwa mkongwe wa miaka mingi. Tangu
Mungu atamke Ahadi ya uzao wa Sara, miaka ishirini na tano ilipita. “Nami
nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani, na katika wewe jamaa zote
za dunia watabarikiwa. Basi Abrahamu akenda kama BWANA alivyomwamuru, Lutu
akaenda pamoja naye. Naye Abrahamu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano
alipotoka Harani.” Mwanzo 12:3-4
IBRAHIMU
alishakata tama juu ya ahadi ya Mungu ya kupata mtoto kupitia SARA, maana
kimwili Sara alikuwa ni mzee asingeweza tena kuzaa. (biologically)
“Mungu
akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake
litakuwa Sara. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam,
nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme za kabila za watu
watatoka kwake. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni,
je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa
miaka tisini atazaa? Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi
mbele yako.” Mwanzo 17:15-18
·
Kwa imani kila mlango uliofungwa utafunguliwa, hatuhitaji kuangalia
historia uliyopitia au hali ya mwili wako bali unachopaswa kuangalia ni Uweza na Nguvu za Mungu aliye
hai
ambaye yeye hashindwi na jambo lolote.
“…lakini mwenye haki ataishi kwa imani
yake.” Habakuki 2:4
“BWANA
ametukumbuka, naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki
mlango wa Haruni, Atawabariki wamchao BWANA, wadogo kwa wakubwa.” Zaburi
115:12-13
Ushindi wetu
katika ulimwengu wa Roho na mwili hutegemea Ufunguo wa Imani.
Itaendelea.....