Wednesday, February 4, 2015

MAOMBI YA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO -1 na Mchungaji Florian Katunzi



Mchungaji Florian Katunzi

Karibu katika mfufulilizo wa somo hili jipya linalofundishwa na Mchungaji Florian Katunzi wa EAGT City Centre, ambalo naamini ukilifuatilia kwa makini hautatoka kama ulivyo. Pia napenda kukwambia ya kuwa jiandae kukipokea kitabu hiki ambacho bado kipo jikoni na kitakuwepo mtaani hivi punde.
 
Leo tunaanza na Sehemu ya Kwanza
 
Zipo aina nyingi za maombi yanayotajwa kwenye Biblia takatifu, na yenye matokeo dhahiri yenye kudhihirisha uweza wa ki-Mungu wenye nguvu za kuangusha ngome zote za giza.  Katika kitabu hiki nitafundisha aina ya maombi ya kufungua  malango na milango.

 

KUOMBA maana yake ni Kumwita Mungu. “Katika shida yangu nalimwita BWANA, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake.” Zaburi  18:6

 

Ndani mwa maombi haya  BWANA  atakufungulia milango, na hakuna malango yatakayofungwa mbele yako tena. Neno la Mungu linatuambia:

 

 “Haya ndiyo BWANA amwambiayo Koreshi, masihi wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake, nami nitalegeza viuno vya wafame; ili kufungua milango mbele yake, hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.”  (Isaya 45:1-3)

 

Kipindi hiki wana wa Israeli walikuwa uhamishoni Babeli, kumbuka walitekwa na kuchuliwa uteka mpaka nchi ya Babeli na Jemadari Nebukadreza, mnamo mwaka 605 KK, baada ya kuwashinda wamisri  katika vita ya Karkameshi. Wakati huo kulikuwa na makundi mawili yaliyopelekwa uhamishoni Babeli, kundi la pili lilikuwa ni lile lililochukuliwa mwaka 586 KK.

 

Huyu Nebukadneza, ni mtoto wa kiume wa Nabopolasa, aliyemridhi baba yake kuwa mtawala wa dola ya Wakaldayo mwaka 605 KK. Hii ni kwa mujibu wa kitabu cha  The Cambridge Acient history  III Uk. 212.  Nebukadireza alikuwa  jemadari kijana aliyekuwa ana misuli ya vita na tena shujaa na mwerevu wa mapigano, hivyo alikuwa na sifa zote za kurithi kiti cha baba yake.

 

Wachambuzi wa mambo ya kale wanamuelezea kuwa alikuwa ni askari na mwanasiasa aliye heshimiwa sana kutokana na uwezo wake wa kuongoza mapigano na kujenga hoja katika uwanja wa kisiasa.

 

Baada ya kutwaa madaraka, mfalme huyu mpya alihusika kujenga  vyema himaya na alama za Babeli katika maeneo mbali mbali ya dunia, tena alijiongezea sifa kwa kumuoa Malkia wa Media  Amyhiya, binti wa Cyaxareas, aliyekuwa na utawala wa Kaskazini.

 

Neno la Mungu katika kitabu cha Daniel 2:36-43, linatuonyesha kuwa baada ya Nebukadreza aliyekuwa kiongozi wa dola yenye nguvu sana ya Ukaldayo kiasi cha  ufalme wake unafananishwa na kichwa cha dhahabu kwa  thamani yake, hata hivyo, alipojiinua kiasi cha kutaka kuabudiwa, ufalme wake, ulikomeshwa na Dola ya Ukaldayo iliingia hatua ya mwisho pamoja na kuchaguliwa kwa Nabondus mnamo mwaka 556 KK.

 

Baada ya kufa kwa Nebukadreza kinafuata kipindi kifupi cha kupinduana na kuchinjana kwa watawala na mwisho kabisa utawala wa Dola ya Ukaldayo unafutika kabisa na unaibuka utawala wa Wamedio, Umedi na Uajemi (Medionapersia) chini ya Mfalme Koreshi Mwajemi na Dario wa wamedi, walioungana pamoja na kuangusha Dola ya Ukaldayo mwaka 538. Utawala wa wabanabe ulidumu kwa kipindi cha miakamia mbili (200), mpaka 331 KK.  Ndani ya kipindi hiki cha utawala wa Wamedi na Wajemi, tunamuona Koreshi, tuliyemsoma katika andiko letu la msingi akitimiza unabii uliotolewa kwa kinywa cha Nabii Isaya miaka mia moja hamsini (150) kabla ya kutimizwa kwake  katika mwaka 538.

 

Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya wakaldayo. Katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Daniel, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka ambayo Neno la BWANA lilimjia Yeremia Nabii, kutimiza ukiwa wa Yerusalem, yaani, miaka sabini. nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwake maombi na dua, pamoja na kufunga na kuvaa nguo za magunia na majivu.” (Daniel 9:1-3).


 

Mungu anamuita Koreshi Masihi (mpakwa mafuta), kabla ya kuzaliwa kwake, kwani alizaliwa kwa makusudi ya Mungu, japo hakuwa akimwabudu (Mungu) wala hakuwa mwana wa Israeli, lakini anatumiwa na Mungu kuyatimiza mapenzi yake, kwa kuwaweka huru  Wayahudi kutoka uhamishoni Babeli.

 

Koreshi na mshirika wake Dario walianzisha dola ya Wamedi na Wajemi iliyodumu kwa karne mbili yaani miaka mia mbili, kama Neno la Mungu linavyosema:

 

“Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi Mfalme wa Uajemi, ili kwamba Neno la Bwana alilosema kwa kinywa cha Nabii Yeremia lipate kutimizwa, BWANA akamwamsha roho yake Koreshi, Mfalme wa Waajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaandika pia akisema Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; BWANA, Mungu wa mbingu, amenipa falme zote duniani; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi, kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, BWANA, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akajenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli, (Yeye ndiye Mungu, aliyoko Yerusalemu).  Na mtu awaye ye yote aliyesalia mahali popote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali,  na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiayari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu.” Ezra 1:1-4

 

Kudhihirisha upekee wa Koreshi, anatoa vyombo vya meza ya BWANA ambavyo Nebukadreza alivitwaa na kuvitia kwenye himaya ya miungu yake. “Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya BWANA, alivyokuwa amevileta Nebukadreza toka Yerusalemu na kuvitia katika nyumba haya miungu yake” Ezra 1:7

 

Itaendeleaa………

No comments:

Post a Comment