Monday, May 13, 2013

MAOMBI YA ULINZI – Sehemu ya Pili na Mchungaji Florian Katunzi


Rev Florian Katunzi
*CHIMBUA KIFUSI, NG’OA MAGUGU YOTE.

*Mwanzo 26:12 - 22, Hagai 2:6-9
Maisha ya ustawi wa watu wengi wa Mungu adui ameutupia kuufukia kwa kifusi.

*Mathayo 13 : 24-28               
“ Bwana Yesu Kristo akawatolea mfano mwingine akisema, ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika bonde lake lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano akaenda zake, baadaye majani ya ngano yalipoanza kuzaa yakaonekana na magugu, watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia Bwana hukupanda mbegu njema katika bonde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawambia adui ndiye aliye tenda”

Katika maisha yetu ya wokovu, ni maisha kamili yenye mamlaka kamili ya kimungu. Hivyo lazima maisha yetu ya kiroho yastawi sambamba na maisha yetu kimwili. Yesu Kristo anatoa mfano wa mkulima aliyelima bonde akapanda ngano(mbegu ya ngano) alipolala(hakulinda shamba) akaja adui akapanda magugu katikati ya ngano.

Hivyo katika bonde moja kukawepo mbegu za aina mbili, mbegu ya ngano na mbegu ya magugu na vyote vikaota vikamea vikatoa matunda sawa sawa na mbegu yake, mbegu ya ngano ikazaa ngano na mbegu ya magugu ikazaa magugu.

Katika somo hili nataka tujifunzi juu ya kazi ya Yesu Kristo.

*Wakolosai 1:13

“Naye alituokoa toka nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza ufalme wamwana wa pendo lake”.

Kristo Yesu anafanya mambo matatu makuu pale anapoingia ndani ya mtu.

(A)  Anamwokoa toka nguvu za giza, nguvu za mauti na kuzimu.

(B)  Anatuhamisha  toka katika ufalme wa shetani.

(C)  Anatuingiza katika ufalme wa Mungu.

Baadaye ya hatua hizi Yesu anatupa mamlaka za kifalme wa mbinguni.

*Luka 9:1 “Akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi”

*Mathayo 16: 18-19

“Juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu wala milango ya kuzimu haitalishinda ,Nami nakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni na lolote utalofunga duniania litakuwa limefungwa mbiguni na lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
FUNGUO ZA UFALME WA mbinguni tunazo katika Kristo Yesu, Yesu anasema watu walipolala adui akaja akapanda mbegu za magugu katikati ya mbegu njema za ngano.

Maombi ya ulinzi niya muhimu katika ustawi wa maisha ya kiroho na kimwili, mtu wa Mungu uliyeitwa kwa jina la Bwana wewe ni mlinzi wa maisha yako, watoto wako na mali zako.

Maisha yako lazima yawe yameunganishwa (connected) na madhabahu ya Mungu aliyehai, funguo za Baraka ,funguo za ustawi wako , funguo za mali ziko mikononi mwako sio nje yako.

Isaka alikuwa mbarikiwa wa Bwana, lakini baada ya kufa baba yake mzee Ibrahim, mali za Isaka zilipukutika zote matokeo yake akajikuta katika njaa nzito maana wafilisti walimwonea wivu wakamdhoofisha kwa kuvifukia visima vya maji wakajaza kifusi.

*Mathayo 26:15

“Na vile visima vyote walivyovichimba, watumwa  wa baba yake siku za ibrahimu babaye ,wafilisti walikuwa wamevifukia wakavijaza kifusi.”

Lakini Isaka baada ya kukaa Gerari miaka mingi , mwisho akamua kulima shamba pale Gerari Bwana akambariki na akamstawisha, watu wa Gerali wafilisti wakamwonea wivu tena.

*Mwanzo 26:14                                                                                       

“Akawa  na mali  ya kondoo na mali ya ngo’mbe na watumwa wengi”

Abimeleki mfalme wa wafilisti akamwambia Isaka utoke kwetu, maana una nguvu sana kuliko sisi, Isaka alipoinuka katika Mungu akafanya yampasayo kufanya mbele za Mungu na Baraka zilionekana tena kwake wale waliomdhalau kwanza, wakatambua Isaka anazo nguvu za tofauti kuliko za wafilisti. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyo vichimba siku za Ibrahimu babaye maana wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake ibrahimu.

-Katika Mungu , mtu wa  Mungu anapojisahau akalala, adui utumia mwanya huo kufukia Baraka zetu maana jukumu la kulinda(Kuomba) si la Mungu bali ni letu. Katika huduma yangu nimekutana na watu wengi wamefungwa na nguvu nzeto za shetani.

Dada mmoja akaja kwangu akasema, kila nikipata mchumba, uchumba unavunjika  sabababu zisizokojulikana mchumba anasema hasikii Amani, lakini baada ya kumwombea nguvu za majini zikajidhihirisha nguvu za giza na kudai huyu ni mke wetu tumemfunga sisi tunataka awe Muhuni tu sio kuolewa. Baada ya mapambano makali akafunguliwa nikamwambia sasa lazima utaolewa, lakini baada ya miezi kama sita akaja akaniletea taarifa amepata mchumba, nikamsihi kuendelea na maombi baada yakupata mchumba lakini hakufanya hivyo bali kwa furaha aliyokuwa nayo akaamua kuwashirikisha marafiki zake wawili akawapa mpango mzima wa uchumba wake na mipango ya harusi, marafiki wakamwonea wivu.

Rafiki wa kwanza(M.S) akachukua jina lake huyu binti na la mchumba wake akaenda kwa mganga mmoja pale tandale  anaitwa (Mohamed Mohamed ni mzanzibar) akamloga yule binti akamtupia jini nuksi akamfanya awe nuksi, akamfanya yule mchumba wa binti awe mzito awe mzito akamtupia jini farakana wakamfarakanisha  na huyu binti  na mchumba wake.

Rafiki wa Pili(L.K) akaenda kwa mganga pia pale Ilala anaitwa Aziz, huyu mganga akamtupia jini yule binti asionekane tena kwa mchumba wake,aonekane mwenye sura ya kizee.

Ndipo huyu binti anakuja ofisini tena, akaniambia mchungaji mambo yameharibika tena na analia kwa uchungu. Baada ya ushauri nikataka kujua kwanini mtu niliyemuombea akafunguliwa kafungwa tena, nikamwambia piga magoti nikamuita Yesu Kristo mwenye nguvu na ndipo pepo nuksi akapiga kelele akidai kwanini  nawafata fata  sana, nikamtiisha chini ya mamlaka kuu ya kimungu na pepo akasema yote ndipo nikamuuliza  mmerudi humu kwa kutumia mlango gani? Wakajibu yeye mwenyewe huyu binti haombi analala tu na anakaa na marafiki zake wa zamani( kupiga story) ana maongezi yasiyofaa, hivyo yeye tumemwingia kwa njia hiyo tu, huyu ameokoka sio mzinzi lakini dhaifu, ndipo nikayaamuru yatoke nikadhibatilisha nguvu zote nikachimbua na kung’oa magugu ya pepo nikaamuru na kumfungua mchumba wake yeye mwenyewe.

Kuokoka pasipo kudumu katika maombi utafungwa na nguvu za giza utafungikika, utaanza kuangaika kutafuta maombizi, mkristo usitegemee upako wa kununua, usitegemee upako wa mafuta na maji, usitegemee upako wa sabuni na chumvi hapana upako nje ya maombi, upako wa uweza wa Mungu unapatikana ndani mwa maombi tu.

*Luka 6:12-19

“Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba  Mungu.” Na makutano walikuwa wakitaka kumgusa kwasababu uweza ulikuwa ukimtoka kiponya wote.

Wako watu  wengi wakristo maisha yao yamejaa kifusi ba magugu, adui amefukia visima vyao vya Baraka, visima vyao vya utajiri na huduma. Bwana asema lazima tujifunge silaha zetu tupigane vita maana ingawa tunaenenda katika mwili hatufanyi vile kwa jinsi ya mwili. Wale waliofungwa katika madhabahu za kichawi sharti waje wasimame na familia zao na mali zao mbele za Bwana.

 * Ayubu 1:5 “ Ayubu  hutuma  kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote”

Ayubu aliomba kama mlinzi wa familia yake akatoa sadaka kwa ajili ya watoto wake. Unaposimama mbele za Bwana tambua wewe ni mlinzi wa taifa, watoto wako na mlinzi wa mali zako

*Mwanzo 19: 1 – 38

Ibrahimu alisimama akaomba ulinzi juu ya kifo kwa jamaa yake Lutu akamwombea ulinzi wakimungu.

*Mwanzo 19 : 29 “ Ikawa Mungu alipoharibu miji ya bondeni (Sodoma na Gomora) Mungu akamkumbuka I brahim akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo ya aliyootoka  Lutu.”

Lutu aliokolewa na Mungu si kwa haki yake bali Mungu aliyaangalia maombi ya mtumishi wake aliyesimama mchana na usiku mbele zake. Lutu na familia yake waliishi maisha ya vugu vugu hata baada ya kuokolewa, Lutu akawa mkulima na mlevi wa pombe , akanywa pombe na binti zake akazaa nao pia , uchafu mzito binti mkubwa akazaa nae mtoto akamwita Moabu na binti wa pili akazaa mtoto akamwita Benani ndiye  baba wa Amoni.

Maombi yako mama, baba, kijana yatainua uzao wako, jamaa zako, kazi zako, ndoa yako na ustawi wako pia. Tunakwenda kutikisa mkuu wa anga hili, mkuu wa nchi kavu na mkuu wa majini, watu wengi wamefunikwa kwa nguvu za mkuu wa anga hili yule kerubi afunikaye.

Nilioombea mama mmoja anasema tangu azaliwe maisha yake niya shida na misukosuko, katika kumwombea majini yanapiga kelele kwa kilio cha uchungu yakidai huyu ni mtu wetu usimfungue si ameokoka tu mwache usimfungue uchumi wake maana nyota yake ndiyo tunayotumia , huyu ni mtu mkuu sisi tumepewa na babu yake tangu akiwa mimba tuliingia kwa njia ya mtoli ambao shangazi yake alimpikia mama yake akiwa mjamzito alipokunywa tukaingia ndani.

Wakati wewe unasubiri mtoto azaliwe ndipo uombe mapepo yanaingia akiwa bado tumboni. Nguvu za giza nikapambana nazo kama masaa matatu, maana zilikuwa ni nguvu za kutisha  mno  maana walitaka huyu mama awe malkia wa anga, wakapinga  nisendelee kuomba wakidai  wewe unatuharibia kazi zetu, tumekubali watu waokoke  wasiende mbinguni, hubiri hivyo lakini usiwafungue uchumi wao.Nyota ya huyu mama nikubwa inatumiwa na kufanya biashara akiwemo na mjomba wake yuko Arusha tajiri,lakini sasa umeharibu  tulikuwa  tunataka ende Arusha akafanye zinaa na mjomba wake lakini sasa unatuchoma.

-Katika ulimwengu war oho kuna mambo mazito mno hata mengine hayasemeke, makafara  mazito yanatolewa, damu zinamwagwa shetani anakunywa damu za watu. Mwisho nikamfungua mama Yule kwa jina la Yesu Kristo

*Yeremia 1:5

“Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa nimekuweka kuwa nabii wa mataifa”

Usifanye mzaha adui yuko kazini kinyume na ustawi wetu, kinyume na taifa letu , imenilazimu sasa kuombea watoto wetu.

-Sasa wanauliza kwanini nimeitisha maombi ya kuombea Taifa, wanasema lazima tunywe damu za watanzania hapa ipo madhabahu yetu, unapinga vita mbona ni mapatano ya watu wetu waliokoka hapa na kule  ili damu ipatikane ili mambo yao yawanyokee. Nami nikasema lazima tung’oe madhabahu zote za kishetani ndani ya taifa letu.Tunaomba mbele za Mungu kwa maombi ya siku tatu yakung’oa madhabahu tutafunga na kuomba, tutamtolea Mungu sadaka na kujenga madhabahu ya ulinzi.

*Luka 11:21-22

“Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake alindapo nyumba yake,vitu vyake vi salama , lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea na kuyagawanya mateka yake.”

 

7 comments:

 1. Amina nimebarikiwa sana na hili somo Mungu azidi kutetea watenda kazi wake...

  ReplyDelete
 2. Mtumishi upo JUU. Mungu akutie nguvu, ni kweli wakristu wengi tunashindwa kutumia MAMLAKA na kusoma NENO. Endelea kuturushia zaidi na zaidi masomo mengi yanatujenga. Pia maombi ya vita na kupata upenyo binafsi ningefurahia sana. Barikiwa. Emma Dismas

  ReplyDelete
 3. Baba nimefurahi sana juu ya somo lako ni kweli kabisa wakristo wengi tunaamini ukiokoka tu ndiyo umemaliza kila kitu kumbe unahitaji kupambana siyo kidogo. asante sana mtumishi wa Mungu endelea kutoa masomo.

  Phillip Bugobora

  ReplyDelete
 4. Shalom! MUNGU akubariki kwa somo hili zuri, mara nyingi nimekuwa nikimlaum MUNGU, pasipo kujua, ninefunguka mno! Nitafanyia kazi maarifa haya ya neno la MUNGU .

  ReplyDelete
 5. Mtumish wa Mungu Mchungaji Katunzi Mungu aendelee kukuinua na kukutumia. tuko nyuma yako Baba

  ReplyDelete
 6. Mtumishi wa Mungu Mchungaji Katunzi Mungu aendelee kukutumia maana kazi yako si bure atakulipa taji. Tuko nyuma yako baba. Amina

  ReplyDelete
 7. Tudumu daima katika imani ya Mungu wa kweli, sala, maombi, na kujitakasa ili shetani asipate nafasi. Asante sana mtumishi wa Mungu hasa katika shuhuda. Mimi binafsi hizo shuhuda za watu ulizotueleza zimenifungua sana na zimeniongezea uchaji wa Kimungu zaidi.

  ReplyDelete