Friday, July 19, 2013

Vitu muhimu vya kuangalia au kufanya unapojiandaa kuoa au kuolewa….Sehemu ya 9





Hofu;
Leo nitaongelea juu ya jambo hili la hofu na nitazungumzia katika pande mbili;
1. Kwanza unapokuwa umeanza mahusiano usiwe na hofu kwamba uhusiano wako hautadumu au utavunjika mwamini Mungu.
Tusome neno hili la Mungu kutoka Wafilipi 4: 6-7 “ Msifadhaike juu ya jambo lo lote; lakini katika kila jambo mjulisheni Mungu haja zenu, kwa kusali na kuomba pamoja na kushu kuru 7 Na amani ya Mungu, ambayo inapita ufahamu wote, italinda mioyo yenu na nia zenu kwa Kristo Yesu.”
Neno la Mungu liko wazi kabisa usifadhaike kwa jambo lolote na mahusiano ni lolote mpendwa wajibu wetu ni kumjulisha Mungu haja zetu kwa njia ya maombi na shukrani,na baada ya hapo unatakiwa uishi kwa furaha na imani maana Mungu unakuwa na uhakika kwamba Mungu anashughulikia mambo yako, Mungu anashughulika na hayo mahusiano.
Ila tu usisahau misingi Mungu anashughulikia mahusiano kama umemwalika ndio maana katika masomo yaliyopita tumesisitiza san asana swala la kuanza mahusiano na Mungu.
Neno la Mungu katika Mathayo 6: 34 Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.
Usiwaze sanaa juu ya nini kitatokea kesho maana kesho inajitegemea yenyewe,usiwaze kwamba kesho huyo mwenzi ataamka na msimamo gani au wazazi wake au wako wataamka na msimamo gani kikubwa sana ni kumtegemea Mungu ambaye anajua mwanzo na mwisho kama yeye ndio mwanzilishi wa mahusiano hayo atasimamia yafike mwisho.
Inawezekana ulikuwa kwenye mahusiano na yalikuwa na picha nzuri sana kila mahali kwamba kuna mahali mnaelekea, na watu wakatamani kuwa kama nyie na mlijitambulisha pande zote mbili na labda na tarehe ya harusi mlipanga iwe mwezi fulani ghafla siku moja na siku moja huyo mkaka au mdada akaamka akasema ameshuhudiwa kwamba sio mpango wa Mungu nyie kuja kuwa pamoja, Pole mpendwa huo          sio mwisho wa safari, yeye sio Bwana Yesu ni mwanadamu kama wewe na ndio maana neno la Mungu katika Zaburi 118: 8 “Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu”
Pia katika Yeremia 17:5 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana” Inawezekana unampenda sana huyo mpendwa wako ambaye unategemea labda utamuoa au atakuoa lakini usije ukakosea ukamtegemea kuliko unavyomtegemea Mungu, mpende lakini ujue kwamba yeye ni mwanadamu kwamba muda wowote akiamua tofauti na mlivyokubaliana japo inauma sana sana jipe Moyo maana aliyeko ndani yako ndio mkuu zaidi,songa mbele na ujue kwamba Mungu atavusha na huo sio mwisho wa safari yako,Mungu atafanya jambo jipya Halleluyaa
Ngoja nikupe ushuhuda kidogo kuna mpendwa wangu mmoja alikuwa na mchumba na walitegemea kufunga ndoa,siku moja mchumba yule aliibuka ghafla na unabii kwamba Mungu amezungumza nae kwamba sio mpango wake hao wapendwa kuwa pamoja,yule dada aliumia akamtafuta mchungaji wake akapata ushauri na maombi, akaweza tena kuendelea mbele pia kwa kutiwa moyo na ndugu na marafiki siku, miaka ikapita yule dada alikuja kuolewa na mtu mwingine na huwa ananishuhudiaga kwamba hakung`ang`ania akamuheshimu Mungu na sasa anaishi maisha ya furaha maana alimtegemea Mungu. Inalipa sana kumtegemea Mungu mpendwa.
2.         Usiwe na hofu kwamba hutaoa au hutaolewa
Neno la Mungu katika Yeremia 29: 11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Mungu aliyekuumba kwa mkono wake anakuwazia mawazo mema ya amani, kama anajua kwamba kitakachokupa furaha ni kuwa na mwenzi basi atakupatia haijalishi umepita muda gani.
Usiangalie umri wako kabisa, kwa Mungu wewe ni kijana kabisa maana hata mahesabu yake ya siku ni tofauti ya ya dunia hii, nakushauri ubadili mtazamo wako kuanzia leo uishi maisha ya imani kwamba
Mungu anakwenda kukupa mtu aliyekusudia kuwa mwezi wako katika wakati ambao yeye anaona ndio sahihi kwako, maana Mungu anakujua.
Usije ukaona wadogo zako wanaolewa ukaumia roho muombe Mungu akusaidie uweze kushinda huo mtihani,na kitakachofunya ufaulu huo mtihani ni Imani yako kwa Mungu, mwamini kwamba atafanya, Amen.
Tena wala usijeukapata majaribu ya kufanya kitu ambacho kitamchukiza Mungu, kama umeamua kumtumaini Mungu basi mwachie yeye wala usimsadie ukaanza kuwaza basi tu kwasababu umri unakwenda niwe tu na mtoto maana sijui ikifika umri gani kupata mtoto sijui itakuwa kazi, jua kwamba maadamu wewe ni mtoto wa Mungu njia zako sio kama za dunia hii ni kaunzia kuishi maisha ya kawaida na hata umri wako wa kupata watoto sio kama wa watu wengine wewe ni mtu wa tofauti sana umeumbwa kwa jinsi ya ajabu.
Nimeona wakaka wa miaka 40 kwenda juu wakioa na wadada halikadhali wanaolewa,hebu kuwa na imani na chunga sana kinywa chako kinatamka nini juu ya hilo, usije ukasema kwamba unajua mimi wala hata huo mpango sina, sema Mungu ninahitaji naomba ufungue mlango nipate na mimi mwenzi wangu nitakayefunga nae ndoa na kuishi naye kwa furaha huku tukikutumikia.
Maana kuna ile tabia ya mtu kujifanya huna mpango kumbe ndio njia adui sasa anaitumia kuzidi kukufunga juu ya jambo hili uwe mkweli mbele za Mungu kwamba Mungu ninakuhitaji katika hili , na pia utafute prayer partner ambaye mnaelewana muombee kwa imani jambo hili.
Naomba kumalizia somo la leo na msitari huu ukutie Moyo, Isaya 41:10 “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
Usiogope kwamba hutapata mwenzi wa maisha Mungu yupo pamoja na wewe atakutia nguvu, atakusaidia na atakushika kwa mkono wake, Amen . Utapita maana Mungu yupo pamoja nawe.
 
 
Ubarikiwe sana na endelea kutembelea Rejoice and Rejoice vitu vingi vizuri vinakuja.

No comments:

Post a Comment