Wednesday, November 27, 2013

Uchumba hadi Ndoa: Je unaweza Kusamehe



Karibu tena katika masomo haya ya uchumba hadi Ndoa,tunaendelea na mtiririko wa Vitu muhimu vya kufanya au kuangalia kabla hujaoa au kuolewa.

Somo letu la leo tutaangalia upande wetu wenyewe tukiangalia kama wewe mwenyewe unayetegemea kuoa au kuolewa Je Unaweza Kusamehe?

Najua utaniuliza sasa mimi nitajuaje kama naweza kusamehe au Lah, Kwani nimeolewa au kuoa?

Ni Kweli hujaolewa bado au hujaoa lakini maisha unayoishi sasa iwe ni na ndugu zako, na rafiki, wanafunzi wenzako,majirani zako, wafanyakazi wenzako,wanakwaya wenzako n.k yanatoa picha kubwa kwamba wewe ni mtu unayeweza kusamehe au lah.

Kama wewe pale nyumbani mdogo wako akikukosea wewe ni mtu wa kushika bango kubwa kutaki kabisa kusamehe mpaka ukoo ukae chini kuwapatanisha inaonyesha kabisa wewe si mtu wa Kusamehe kwa urahisi na tabia hii utaipeleka kwa urahisi sana kwenye ndoa.

Au wewe pale shule au Chuoni ni mtu ambaye huwezi kusamehe kabisa kwasababu labda mwanachuo mwenzako amekukwaza akakuomba msamaha lakini wewe hukumsamehe na hadi mmemaliza chuo au shule umeuendeleza ule uadui , hiyo ni dalili kubwa kwamba siku huyo mwenzako akija kukukosea kuna uwezekano mkubwa sana wa kutomsaheme.

Kuna mtu nakumbuka alikuwa shuleni akagombana na mwenzake yaani huo ugomvi haukuisha na hakuna hata mmoja aliyetaka kusamehe kwahiyo mpaka leo Zaidi ya miaka kumi hao watu wameendelea kuwa maadui na kitu kilichowafanya wagombane kilikuwa kidogo sana.

Sasa hao watu unategemea kwamba kwenye ndoa kama mwenzao atawakwaza watasamehe kweli kama sio msaada wa Kristo Yesu tu.

Watu wengine wameokoka kabisa lakini utasikia anasema yaani I am so delicate mimi ukinigusa nakaa mbali na wewe hiyo ina maana huwezi kusamehe au kuchukuliana na mwenzako.

Unatakiwa kujua kwamba vitabia fulani ulivyo navyo ambavyo ama kwa kujua kutokujua hutaki kuvishughulikia vina madhara makubwa sana katika ndoa maana vitakuja tu kujitokeza hasa pale ambapo mtakuwa mmeshazoeana na mwenzako, tena ndio vitakuwa dhahiri kabisaaaa.


Neno la Mungu katika Mathayo 6: 14 – 15 Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.”


Kwahiyo nakushauri amua leo kujifunza kusamehe kwanza maana kama umeokoka au ni Mkiristo na husamehi na wewe Mungu hatakusamehe makosa yako. Kwahiyo utakuwa Mkristo Jina.

Ndugu zangu Msamaha sio Rahisi, lakini hatuna Budi Kumuomba Mungu kutupa neema na uwezo wa kusamehe hata kama mtu ametukosea mara nyinge kiasi gani.

Ninaposema sio Rahisi naamanisha Kabisa maana kuna kipindi ilinichukua miaka kuwasamehe watu fulani fulani lakini nilikuwa Napata shida nikiwa mbele za Mungu maana nilikuwa naona wamesimama mbele yangu na hata huduma yangu ikawa ngumu kutokana na kubeba wao moyoni mwangu, lakini nilipoamua kwamba jamani enhee NINASAMEHE ndipo nilimuona Mungu akinitumia kwa Njia ya ajabu. Na nilijisikia Vizuri sana na Huru na kufurahia maisha yangu ya Wokovu.

 
Hii Tabia ya kutokusamehe unaweza ukawa nayo kama ulikutana na maisha fulani yenye changamoto watu wakakunyanyasa labda kwamfano ulikaa kwa ndugu ambaye alikunyanyasa, au kuwa katika mahusiano ambayo yamekuumiza, sasa wewe ukaona kwamba kutowasamehe au watu ndio unapata relief lakini nataka nikuambie Leo mtu wa Mungu, kutokusamehe kunachelewesha Muujiza wako hebu amua leo kuchua hatua maana kama umeamua kumfuata Yesu heshimu na Neno lake, yaani SAMEHE ili USAMEHE mwaka huu Mchungaji wa Kimataifa TD Jakes alitoa kitabu kilichopendwa sana Forgive so that you can Be Forgiven kwakweli hicho kitabu kinaelezea umuhimu kwa kuwa Mkristo mwenye maisha ya Kusamehe, na hata yeye TD Jakes anatoa ushuhuda alivyoweza kumsamehe mtu ambaye aliyetaka kubomoa huduma yake.


Swala la kutosamehe limevunja mahusiano mengi hasa ya ndoa, na mimi naangalia kwa mtazamo huu kwamba hili swala mtu haendi kulianzia kwenye Ndoa, analianzia katika maisha yake ya kabla ya ndoa amezoea hivyo ,labda katika ukoo wao ni jambo la kawaida kutosamehe, utakuta mtu alikua akiona jinsi wazazi wake walivyokuwa hawajawasamehe majirani au ndugu mbalimbali, au ambavyo hawakusameheana labda na ndoa kuvunjika. Mtu kama huyo anaweza kuona ni kawaida na ndio njia ya kujifariji, maana mwingine anasema nataka Amani, Mpendwa huwezi kupata Amani kama kuna mtu unambeba moyoni, bali ukiwa mtu wa msamaha.

 

Je Utafanyaje ili uweze Kusamehe;

·         Nitakuambia nilichofanya mimi ilikuwa kuomba na kusoma neno na kuhudhuria semina mbalimbali na makongomano, katika hizo utasikia shuhuda na mafundisho ya watu walioweza kusamehe vitu vikubwa.

·         Jambo lingine ni kujifunza kuwa mtu wa Kusamehe, anza kusamehe wale ulio nao kwa Karibu usichukulie vitu serious sana na vigumu, Samehe tu mpendwa
 

·         Jitamkia kwamba wewe ni mtu unayesamehe, maana katika Ulimi kuna nguvu ya mauti na uzima, ukitamka uzima utaupata ukitamka mauti nayo utaipata, mauti yaweza kuwa katika hali yako ya kutosamehe,

maana nakumbuka kuna mtu aliniambia yaani mimi huwa siwezi kusamehe kabisaa nimejitahidi maombi ya aina yote,  sasa huyo atakuwa hivyo maana ndicho anachijitamkia. 

·         Samehe Kila kitu, mtu mwingine ana checklist, anasema hili na hili nitasamehe lakini hili mmh hapana sisamehi, hiyo si sawa Neno linasema SAMEHE

 
Kutokusamehe kuna madhara mengi sana, hayo nitayazungumzia katika Somo tofauti wiki Ijayo.

 
Leo nakushauri ndugu yangu anza kujifunza kusamehe, usipende kulalamika na kuona kwamba wewe unakosewa sana au hupendwi Samehe tuu, Na Mungu wangu wa Mbinguni akuwezeshe katika Hili Bila Nguvu yake haitakuwa Rahisi.

 

2 comments:

  1. My Life Coach, keep it up and keep them lessons flowing...

    ReplyDelete
  2. Amen my Coach, God Bless you abundantly

    ReplyDelete