Wednesday, August 6, 2014

Uchumba hadi Ndoa: Usifikiri utaweza kubadilisha tabia ya mwenzi wako baada ya kuolewa naye au Kumuoa

 

Bwana Asifiwe watu wazuri wa Mungu, namshukuru Mungu kwa siku hii nzuri aliyonipa maana kwakweli muda nao umekuwa mali.

Natamani sana kila wiki niendeleze Makala haya lakini mara nyingine tunabanwa na muda lakini pia Mungu ana makusudi kwa kila jambo.

Leo naomba tuzungumze jambo hili muhimu sana katika mahusiano, linalohusu pale mtu anapokuwa na matarajio kwamba mwenzi wake atakuja kubadilika tabia yake mbaya au isiyombariki baada ya kuingia kwenye Ndoa

Hii inakuwa hivi inawezekana watu wamekaa katika uchumba wanavyoendelea kuna tabia unaziona kwa mwenzi wako ambazo unaona kwamba ni ngumu yaani hazibebeki, lakini unaamua kwamba utaendelea maana unajua kwamba ukimuoa au akikuoa utakuwa na Mamlaka ya Kuweza Kumbadilisha au Kukomesha hiyo tabia.

Sisemi kwamba watu wenye udhaifu fulani hawawezi kubadilika,HAPANA mtu yoyote yule anaweza kubadilika ila Mabadiliko yatatokea tu pale mtu ANAAMUA kubadilika na sio kung`ang`anizwa kubadilishwa.

Hakuna aina ya ubabe ambao wewe mke au mume unaweza kutumiakwenye Ndoa ili kubadilisha tabia yake, sio pesa, sio chochote kitakachoweza kubadilisha mtu

Unaweza kuwa na mchumba ambaye ana mahusiano mengi mengi, leo umemkuta na meseji za Joyce, Kesho za Jane,mara umesikia jana alikuwa na mwingine sijui KFC au Steers pale, wengine tena wanakutumia labda meseji za kejeli au wengine wanakupigia simu kwamba huyo ni cha Wote, lakini wewe unang`ang`na kwamba eti huyu mtu wangu atabadilika pale tu Nitakapomuoa….

Kuna kisa nilikisikia hivi karibuni kaka alikuwa mchumba, kumbe huyo dada alikuwa anaendeleza mahusiano ya zamani kisirisiri, sasa kibaya sana siku mbili kabla ya harusi kuna mtu alimuona huyu mwanadada akiwa ametoka kwa yule mtu wake wa zamani, huyu kaka aliambiwa lakini akasema huyo mimi nikimuoa nitamkomesha hataweza kutoka hata ndani nitamfungia, NITAMBADILISHA.

Je Ndugu yangu unafikiri kweli kwa tabia hii huyo dada yetu ataacha mahusiano hayo, kama kweli anashindwa kuheshimu ndoa yake kabla hajaingia maana hapo hata huyo mume hajamjua vizuri je akishaishi naye kweli ndio ataiheshimu hiyo Ndoa. Hebu tafakari hili mpendwa wangu....

Neno katika Mathayo 6: 24“Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. Maana atamchukia mmoja na kumpenda huyo wa pili; au ataambatana na mmoja na kumdharau huyo mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja.”

Ukisoma Maneno ya Mungu hapo juu neno liko wazi Kabisa kwamba mtu huwezi kutumikia mabwana wawili yaani huwezi kushika mambo mawili lazima kuna moja utalidharau na kuzingatia lingine.
Kwa upande wa mahusiano kama mtu anakuwa na mahusiano mengi mengi ina maana hatakuwa na upendo wa kweli, atamchukia mmoja na kumpenda huyo wa pili, pia dharau itaibuka kwasababu atakuwa anajua ana plan B, hiyo ndoa itakuwa imejawa na uchungu mkubwa kila siku watu wakikimbizana, mashitaka, vilio, kwasababu tu mmoja alifikiri kwamba ataweza kumbadilisha mwenzake wakishafunga Ndoa, asijue kwamba Mabadiliko ya kweli huja tu pale mtu ANAPOAMUA mwenyewe kwa dhati.

Nakushauri ewe ndugu mpendwa wangu, dada, kaka, mdogo wangu ambaye bado hujaingia kwenye ndoa na uko kwenye mahusiano ambayo kwakweli tabia za mwenzi wako ni kwazo , hazibebeki, unaona kabisa hakupendi, anafanya vitu vinavyokuonyesha wewe si wa thamani kwake, anakubeza, kila siku wewe una kazi ya kumfumania labda, unatumiwa tu meseji za vitisho na watu wengine ambao ana mahusiano nao na umepeleka hilo swala kwa watumishi, washauri, wazazi lakini hajabadilika na wewe unaendelea kugugumia hivyohivyo na kung`ang`nia kuingia katika Ndoa hiyo hebu mpendwa wangu TAFAKARI tena, hayo ni maisha yako.

Unapaswa kujua Ndoa za Kikristo hazivunjiki jiulize maswali haya kabla hujaendelea na mipango ya Ndoa hiyo;

  • Nitaweza kuvumilia tabia na manyanyaso haya siku zote za NDOA yetu?
  • Hivi Mungu hawezi kunipa mtu mwingine atakayenithamini
  • Je maisha yangu hayatahadhirika
  • Je Mungu akinibariki na watoto nitakuwa na cha kuwafundisha juu ya Ndoa kitakachowajenga
  • Ndoa hii ninayoiendea na tabia hizi itanipa mlango kweli ya kufanya lile kusudi Mungu aliloweka Ndani yangu, au ndio kila siku itakuwa vita, vilio na magomvi?

Ukipata Jibu mpendwa wangu hebu amua haraka iwezekanavyo ili usimpotezee mwenzako muda wake na wa kwako pia usipotee, Amen!

Kama sasa umeshaingia kwenye mahusiano ukiwa na mtazamo huo na sasa uko kwenye KILIO ufanye nini;

1. Muombe Mungu na Kuamua Kubadilika

2 Mambo ya Nyakati 6: 30 -39

Ukisoma Maneno ya Mungu hapo juu inaonyesha kwamba kama mtu ataamua kwa moyo wake wote na nia yake yote kumuomba Mungu, Mungu atasikia maombi yao na atawasamehe na ubaya wao wote

2. Ongea na watumishi wa Mungu

3. Tafuta Washauri wa mambo ya Ndoa na Mahusiano wenye misingi ya Kikristo

4. Amini kwamba Mungu anaweza kumdalisha

Mungu akusaidie sana unapokwenda kufanya maamuzi makubwa ya kuingia kwenye Ndoa, au kumchagua mwenzi wako wa Maisha

Kama nilivyokwisha kusema zamani bora mahusiano yavunjike hata kama umeshafanyiwa send off Kuliko kuingia kwenye Ndoa yenye mateso wakati uliona Kabisa dalili hatari

Mungu akutembelee wewe ambaye umejikuta katika Kilio kwa Maamuzi hayo uliyoyafanya, yeye bado ni Mungu anayo nafasi nyingine ya kufanya, anaweza Kabisa kuibadilisha Ndoa yako, hebu chukua hatua leo ya kumtafuta kwa dhati nawe utaona wema wake, Haleluyaaaa

Endelea kutembelea Rejoice and Rejoice Blog mambo mazuri yanakuja

 

No comments:

Post a Comment