Karibu atika mifululizo yote ya somo hili kutoka mwanzo mpaka sasa
imekuwa ni suala la kuangalia ni kwa jinsi gani nafsi zetu zinahusika sana
katika Uhai wa Kanisa. Sehemu ya mwisho nitasema nawe kwa kifupi sana kuhusu
Uhusiano wa nafsi ya Kanisa.
Karibu tujifunze pamoja…..
Luka 12:15 inasema hivi;
Akawaambia, Angalieni,
jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo
navyo.
Ni heri kila mmoja akahakikisha ya kwamba Nafsi yake iko na
furaha kila wakati, kwa ajili ya uhai wa kanisa lako, lakini pia kwa ajili ya
uhai wa nyumba yako kama msingi wa kanisa, kwa ajili ya ofisi yako, kwa ajili
ya ukoo wako.
Lakini pia ni vema kila mmoja akahakikisha anafanya bidii kumfurahisha
mwingine na kuifanya nafsi ya mwingine isiwe na jeraha hata moja, kuifanya
nafsi ya mwingine isitende dhambi, kila mmoja acheze karibu na mwenzake, kama
kucheza basi tucheze peke yetu, hakikisha unamlinda mwenzake asipate shida wala
asipotee.
1 Wakorintho 8:12 tunasoma hivi;
Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri
iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo
Kuna Uhusiano Mkubwa kati ya Usalama na
Ubora wa Nafsi yako na Uhai wa Kanisa
Sasa labda tutazame kwa nafasi nyingine uhusiano wa Nafsi
yako ikiwa na Usalama na ubora wa nafsi yako na Uhai wa Kanisa ikiwa ni la
nyumbani au ni mahali unapoabudu au ofisini kwako au hata shuleni kwako
unakosoma.
Labda niweke jambo hili la msingi, tunapozungumzia kanisa ni
lazima tukajua ya kwamba si suala la dhehebu moja tu au suala la watu wanaosali
kwa pamoja lakini suala la Kanisa ni jambo linalohusu watu wote waliookoka na
wanaomkubali BWANA YESU kuwa ni mwokozi wa maisha yao na Mfalme wa Ulimwengu
wote.
Sasa kuna shida ambayo ni muhimu tukaishughulikia vizuri
kidogo ili tusipate shida tunapoangalia utekelezaji wa Somo hili, na jambo
lenyewe ni lazima akili zetu na fahamu zetu zifunguke tukajua mambo kadhaa ili
tuone Umuhimu wa kuona Nafsi ya kila mmoja inakuwa salama na bora ili Kanisa
liweze kuwa Hai.
1 Wakorintho 3:16-17 tunasoma hivi;
Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa
Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu
atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Sasa kuna jambo la msingi hapo natamani tulitazame kwa
makini sana sana, maana kama tusipolitazama kwa makini tunaweza tusielewe
vizuri, na hilo jambo linatuonesha Uhusiano uliopo kati ya Usalama na Ubora wa
Nafsi yako inavyohusiana na Uhai wa Kanisa la Tanzania, Kanisa la Ulimwengu
mzima lakini pia kuanzia na Kanisa la Nyumbani kwako na mahali unapoabudu.
Basi tuutazame huo mstari kwa makini sana sana, kuna maneno
kadhaa ya huo mstari natamani tuyatazame kwa makini …..Hamjui ya kuwa NINYI
mmekuwa hekalu la Mungu….. na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani YENU?.......
Kama MTU akiliharibu hekalu la Mungu,… Mungu atamharibu MTU huyo….. Kwa maana
hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo NINYI.
Maneno niliyoyaweka kwa herufi kubwa yana maana kubwa sana,
Paulo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu anawaandikia Wakorintho akitaka kuwaonesha ni
jinsi gani Uhusiano wa Kanisa unavyotengenezwa na unavyotegemea mtu mmoja
mmoja. Anapozungumzia Hekalu la Mungu anasema ni NINYI au ndilo SISI kama
tukijiweka kwenye nafasi ya Wakorintho na ambayo ni nafasi muhimu lazima
tujiweke hapo ili hiyo nafasi tuichukue kwa Umuhimu mkubwa sana.
Jambo amabalo ni la kulitazama kwa makini kwenye mistari
hiyo ni kwamba inapozungumziwa kanisa basi tunatazama kama Muunganiko wa watu,.
Maana HEKALU LA MUNGU (moja) linajengwa na NINYI (wengi), lakini pia
inawezekana hilo Hekalu la Mungu ambalo ni watu wengi likaharibiwa na MTU yaani
mmoja. Sasa basi kuna jambo la kulitazama tena hapo kwa makini Zaidi, kwamba kama
Hekalu la Mungu linalojengwa na SISI linaweza kuharibu na YULE au WEWE basi pia
linaweza kujengwa na WEWE- Nitalielezea hilo baadae kwa undani.
1Wakorintho 6:19 tunasoma hivi;
Au hamjui ya kuwa
mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu?
Wala ninyi si mali yenu wenyewe;
Nataka tutazame vizuri maneno mengine kwenye mstari huo
ambayo hayatofautiani sana maneno yaliyoelezwa kwenye mistari ile
tuliyotangulia kuitazama hapo juu (1Wakorintho 3:16-17), maana katika mstari
huo hapo anaeleza wingi wa waliookoka kama mtu mmoja na ambaye huyo mtu mmoja
anatengeneza Hekalu la Mungu, lakini cha ajabu Paulo anaandika kwa wengi kana
kwamba kwa mtu mmoja.
Tazama kwa makini maneno haya;
Au HAMJUI ya kuwa MWILI WENU ni hekalu la Roho Mtakatifu
aliye ndani YENU, MLIYEPEWA na Mungu? Wala NINYI si mali YENU wenyewe;
Anasema hivi
Au HAMJUI (wengi) ya kuwa MWILI WENU (mmoja) ni hekalu la
Roho Mtakatifu aliye ndani YENU MLIYEPEWA (wengi) na Mungu? Wala NINYI si mali
YENU wenyewe;
Katika yote nataka nikuoneshe ya kwamba haijalishi kwa
Ukubwa wake au kwa udogo wake, kwa umaarufu wake au kwa kutokujulikana kwake,
KANISA linaanza na Nafsi moja moja na haijalishi kwa wingi wake waliopo humo
ndaniau idadi ya waliookoka katika mji Fulani au nchi Fulani bado kanisa
litahesabika kama MTU MMOJA au MWILI MMOJA.
Mpaka hapo tujaribu kurudi kidogo kwenye ule mstari wa
1Wakorintho 3:17 unasema hivi;
Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu
huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Nataka tuone madhara yanayoweza kutokea mtu anapojaribu
kuliharibu Hekalu la Mungu yaani Kanisa ambalo ni Ninyi mlio wengi
mnaotengeneza Mtu au Kitu kimoja katika kumtukuza Kristo au kusimamisha Ufalme
wa Mungu. Maandiko yanasema mtu akiliharibu Hekalu MUNGU atamharibu mtu huyo.
Sasa tuondoe mawazo ya kuwafikiria watu kama wakina Sauli
ambao wanaliharibu Hekalu au Kanisa kwa sababu Hawajaokoka, au tusiwafikirie
Wakuu wa makuhani wanaokataza watu wasiseme tena wala kupoza Wagonjwa kwa Jina
la YESU, tukiangalia hivyo tutakosa maana ya msingi sana sana, hebu tuutazame
huo mstari kama unawaambia watu au unamuonya Mtu anayeliharibu Kanisa huku naye
ameokoka au yumo ndani ya Kanisa.
Na kulingana na maandiko inawezekana kabisa mtu akaliharibu
Kanisa wakati mwenyewe yumo humo ndani yake, haijalishi anajua kama analiharibu
Kanisa au la, lakini kuna uwezekano kabisa akawa analiharibu kanisa wakati na
yeye yumo ndani yake.
Matendo 20:28-30 tunasoma hivi;
Jitunzeni nafsi zenu,
na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi
ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake
mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali
wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu
wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.
Sasa kuanzia mstari wa 30 inaonesha kabisa ya kwamba si
kwamba mharibu anaweza kutoka nje ya kundi lakini kumbe anaweza kutoka ndani ya
kundi, hata kama ataonekana ni kama mtu anayekata tawi alilokalia mwenyewe
lakini hiyo si kitu lakini ndio anaharibu sasa. Na MUNGU hawezi kukaa kimya
anapomuona mtu anaharibu au
anapoleta au kuingiza kitu kinachoharibu kanisa hata kama
huyo mtu hajui lakini MUNGU hatamuacha, lazima atampa adhabu Kulingana na ule
mstari wa 1Wakorintho 3:17.
Lakini nataka niweke jambo Fulani ndani yako ya kwamba, kama
mtu alikuwa mpo naye pamoja kasha akaanza kutenda mambo tofauti na kuliharibu
kundi lazima mtapata shida, lakini pia MUNGU akimhadhibu mtu huyo bado kwa watu
wenye Uchungu na Kanisa watapata shida lazima maana wanajua Umuhimu wake, hivyo
hawatafurahia adhabu ya MUNGU aliyoipata, hivyo basi Nafsi moja ikiharibika
lazima kuna jambo linabadilika kwenye Kanisa.
Matendo 5:5-11 inasema hivi;
Anania aliposikia
maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia
haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje, wakamzika.
Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya hayo
yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo?
Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana
kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao
watakuchukua nje wewe nawe. Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana
wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe. Hofu
nyingi ikawapata kanisa lote na watu wote walioyasikia haya.
katika mistari hiyo natamani nikuoneshe kilichotokea kwa
Anania na Safira na Uhusiano na Kanisa, sasa ninawinda mstari ule wa 11 ambao
unatuonesha jambo Fulani lililotokea kwenye Kanisa na jambo lenyewe ni HOFU
iliyo ZIMISHA nafsi zao kwa ndani, sio hofu tu ya kusema MUNGU ni MKUU lakini
pia inakuwaje mtu akiwa na shida ya kuonana na Petro au mtume Fulani, na ndio
maana hawakuwa na Ujasiri wa kusema jambo lolote na waliona ni heri kutenda
dhambi ya kunung’unikakuliko kuonana na Mitume na kuwaambia shida zao.
Yote hiyo inatokana na nafsi ya mtu mmoja Anania
ilipoharibika ilikuwa haiku Salama iliyomshauri Mkewe Safira na wote wakatenda
jambo lililoharibu Kanisa kwa namna moja au nyingine, na halikuharibu kanisa
kwa mtindo ambao watu waliondoka, la hasha! Watu walikuwepo na walizidi
kuongezeka katika kanisa (MATENDO 4:14) lakini ndani yake kuna WOGA/HOFU ambayo
ilisababisha watu wawaogope mitume kuwaeleza shida zao wakaona ni vema tu
wakanung’unika (MATENDO 6:1)
Nataka niseme ya kwamba suala si tu kuona watu, lakini Nafsi
ya kila mmoja inatakiwa iwe Salama, maana nafsi Fulani ikiharibika basi ujue
hakuna Usalama hapo, na ujue kabisa kunahitajika kuhakikisha kila nafsi ndani
ya Kanisa iko Salama na iko Bora.
Waebrania 12:15 tunasoma;
Mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la
uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa
hilo.
Nimeweka huo mstari hapo ili tutazame jambo hilo kwa mtazamo
wa Upande wa pili ya kwamba kama mtu mmoja akipungukiwa na Neema ya Mungu
anaweza kuleta shina la Uchungu ambalo linawakwaza wengi, Je ikatokea mtu mmoja
akaongezewa Neema ya Mungu nini kitatokea?
NADHANI SHINA JEMA SHINA LA UTAMU, SHINA LA FURAHA, SHINA LA
KICHEKO, SHINA LA WEMA LINACHIPUKA NA KUWABARIKI WENGI.
Aaaaameen!!!
Umebarikiwa.
NURU Ministry:
mkumbosj@gmail.com
www.facebook.com/mwlsamwelmkumbo
+255 753 – 204 743
No comments:
Post a Comment