Bishop Nickodemus Shaboka Jr |
Leo katika Hoja yangu tutakuwa na mtumishi wa Mungu Bishop Nickodemus Shaboka Jr,karibu tujifunze.....
Mafanikio ni jambo
ambalo limeshika hatamu katika ubongo wa kila mtanzania leo, awe kanisani au
nje ya kanisa, katika kila eneo la maisha watu wanataka, wanapambana na
kupigania mafanikio. Tafsiri nyepesi ya neno mafanikio ni kuongezeka au
kubadilika kutoka ngazi moja kwenda nyingine au kutoka hali mbaya kwenda nzuri.
Hili ni jambo ambalo
kanisa la leo kila upande utasikia semina za mafanikio, maombezi ya mafanikio
na mambo kama hayo, na kwa kweli watu wanajitoa kuhudhuria hata kama ni kwa
wiki mbili kujifunza namna ya kufanikiwa.Leo nataka tuangalie habari ya
mafanikio katika kanisa hasa makanisa ya kipentekoste “kiroho” ambayo kwa karne
hii ya 21 ishirini na moja yameonekana kuchukua nafasi zaidi katika jamii yetu.
Miaka ya 90’s kurudi
nyuma, haikuwa rahisi kukuta hapa Nchini kanisa la kipentekoste linawashirika
zaidi ya 300, lakini leo makanisa ya kiroho hapa hapa Tanzania yana washirika
mpaka 10,000 elfu kumi na zaidi. Naweza kusema tumefanikiwa kwa mtazamo wa
kuhama hatua moja kwenda nyingine.
Mtu mwnye akili timamu
au anayeitwa kakamilika kiakili ni yule ambaye anaangalia alipotoka, alipo na
anapoelekea, na ilikujua unakotoka, ni muhimu kujua msingi wako ni upi, ili kuangalia
misingi uliosimamia au unaojenga juu yake kwa sasa kama unamizizi sawa na ile
uliyoanza nayo au unayopaswa kuendelea nayo.
Msingi wetu kama kanisa
ni Kristo, na ndiye tunayejifunza kutoka kwake. Yaani kwa maana rahisi
tunatakiwa kupima mafanikio yetu kwa kuangalia tumejenga namna gani au kama
kanisa tunaenenda namna gani juu ya kile alichokianzaisha Bwana wetu Yesu
Kristo aliye jiwe kuu la pembeni na nguzo ya kanisa.
Kwakuwa Yesu ndiye
nguzo yetu, yeye alifanyaje katika huduma yake na sisi tunafanyaje leo? Je
tunadumsha kile alichoanzisha au tumegeukia mambo yetu wenyewe? Hicho ndicho
kipimo halisi cha mafanikio ya kanisa.
Maana ninaavyoelewa
mimi, kanisa ni mwili wa kristo na Yesu ndiye kichwa, hii inamaana kanisa
halina matakwa yake lenyewe, bali lipo kutimiza yale anayotaka Yesu juu ya
kanisa lake.
Katika huduma ya Yesu
kwa miaka mitatu na nusu hapa duniani, ukisoma maandiko, alijihusisha sana na
mambo mawili, kwanza alitoa huduma ya Kiroho na pili huduma ya kimwili ambayo ilileta
uwiano. Muujiza wa kwanza aliofanya kabla ya muujiza wowote ambao Biblia
imerekodi ni ule wa kugeuza maji kuwa divai na kuokoa jahazi katika harusi ya
Kana ya Galilaya. (Yohana 2:1-11)
Swali linakuja, je sisi
kama kanisa yaani wafuasi wa Yesu, watu wa uamsho, tunauwiano katika huduma?
Tunaigusa vipi kimwili jamii inayotuzunguka? Tunasifa gani ya kuhudumia
wanajamii?
Mwanafunzi mzuri, au
mfuasi aliyefaulu,ni yule ambaye anamtazama mwalimu wake na kuigiza kila kitu
anachokifanya mwalimu wake. Sisi kama kanisa tunafanya yote aliyofanya Bwana
wetu Yesu?
Tukiangalia wenzetu wa
upande wa pili, kila wanapojenga nyumba ya ibada kwa asilimia kubwa wanatoa na
huduma za maji aidha ya kisima au ya bomba kwa jamii inayowazunguka. Sisi
makanisa yetu yanafanya nini mbali kuongeza maspika kuwapigia makelele ya
nyimbo wanajamii?
Sikatai kwamba tunaihudumia
jamii kiroho kwa kutoa mapepo na kuwafungua vifungo mbali mbali, lakini hata
Yakobo anasema imani bila matendo imekufa. Yesu aliwahubiria na kuwapa mikate
ili waendelee kumsikiliza.
Mkazo tulio nao katika
kukusanya pesa za sadaka, fungu la kumi na michango mbali mbali, kwanini
tusiutumie pia kuangalia tunaigusa vipi kimwili jamii inayotuzunguka? Badala ya
kutumia milioni nne kuandaa mkutano wa nje “Crusade” tutumie pesa hiyo
kukodisha hata magari ya maji safi tukanywesha bure maeneo yasiyo na maji, huku
tukitumia fursa hiyo kuwahubiria injili. Je hatutafaulu?
Ni jambo lisilopingika
kwamba ulimwengu umebadilika, hata Tanzania imeingia kwenye mfumo wa digitali,
mbona kanisa bado limeng’ang’ania mifumo ya analogia. Mimi naamini kuwa Mungu
ndio “up to date” wakisasa kuliko hata wanadamu.
Ndio maana anamwambia
Musa “Nami nilijulikana kwa Ibrahimu na Isaka, na Yakobo kama Mungu Mwenyezi,
bali kwa jina langu Yehova, sikujulikana kwao.”(Kutoka 6:2-3) Kama Mungu wetu
anavipindi vya mabadiliko, iweje sisi tubaki pale pale tulipokuwa miaka nenda
rudi.
Hebu tuamke kama
kanisa, Yesu ametuambia,” Mtu akinipenda atazishika amri zangu” basi na tushike
amri zake kwa kufanya alichokifanya kiongozi wetu. Japo hata mara moja kwa
mwaka basi kwenye karenda ya makanisa yetu ya kiroho, badala ya kuweka mikutano
mitatu ya nje, tuweke angalau siku ya huduma kwa jamii.
Tukifikia mahali pa
kuweka uwiano kati ya huduma za kiroho na kimwili, hapo tunaweza kusema
tumefanikiwa. Wenzetu ngozi nyeupe walipotuletea injili, walifanikiwa kirahisi
kwani waligusa huduma kwa jamii pia. Imani pasipo matendo imekufa.
Wamisionari wengi, ndio
waliojenga mashule, vyuo mbali mbali, zahanati hadi hospitali kuu, na makanisa,
na huo ndio msingi wa Ukristo. Lazima tutofautiane na wanasiasa. Hata wahenga
walisema “Maneno matupu, hayavunji mfupa.”
Kwa
maoni na ushauri tuma bishopshaboka@gmail.com au 0784 310 587.
Bwana Yesu apewe sifa,
ReplyDeleteMtumishi Mungu akubariki kwa kutukumbusha majukumu yetu kama Wakristo na kama kanisa. Ni kweli yatupasa tutazame yale Kiongozi wetu Yesu Kristo alitenda nasi tutende na zaidi ya yale. Kwa njia hiyo, injili ikihubiriwa itapokelewa kwa urahisi zaidi, na Mungu atusaidie.
In faith of the Lord Jesus Christ, Martha Macha Msale
Amina mtumishi Martha,ni kweli kabisa Kama Kanisa la Kiristo tumekumbushwa wajibu wetu katika makala haya
ReplyDelete