Friday, September 27, 2013

There is No Glory without Story,Hakuna Taji ya Utukufu pasipo Taji ya Mwiba by Frida Blessings James


 

UNAPITIA KIPINDI GANI KATIKA MAISHA YAKO???

TAMBUA JINSI YA KUISHINDA SAA YA MAMLAKA YA GIZA!

Hakuna mwanadamu asiyepitia kipindi hiki, usipoishinda saa hii itakushinda! Usipoiharibu itakuharibu Luka 22:52-53. Mamlaka hii ya giza inaweza kujifunua kazini, kwenye jamii/familia-nyumbani hata katika huduma au katika nchi.

Ninamaanisha nini nikisema saa ya mamlaka ya giza? Ni wakati unapopitia kipindi kigumu maishani kiasi cha kutamani kujikimbia/ kujiua au kukataa tamaa na wale uliowategemea wakakukimbia na kukaa mbali na wakati huo unaweza kuona pia Mungu amekuacha kwani atakaa kimya ili kuipima imani yako je unamwangalia yeye au tatizo.

Mamlaka hii ina majira yake na ndio maana inaitwa saa ya mamlaka ya giza.Inatumika na mtu au watu. Pia inatabia ya kukutenga na watu ili ikupate na ikumalize kwani hata uliowategemea watakaa pembeni. Ila lazima ujue hata kama wote watakimbia lazima Simon wa Kirene atokee atakuja mtu usiyemtegemea atakayeletwa na Mungu. Mfano halisi wakati ule wa Yesu , Saa ya mamlaka ya giza ilipofika kwa Yesu aliitambua. Petro alikaa pembeni akasema simfahamu mtu huyu, Yuda alimsaliti. Pia wale Mitume waliposhindwa kuomba Mungu aligusa watu, kuna wakina mama waliokuwa wakilia na kuomboleza, walimfuata Yesu na kumywesha maji.

Kumbuka saa hiyo ni saa ya kudhalilishwa, ni saa ya matusi. Kutakuwa na kusalitiwa unaweza kugeukwa na mtu uliyemtegemea sana,anaweza kuwa ndugu, mke, mume, mtoto, mzazi, rafiki,mpendwa hata mtumishi mwenzako n.k. Saa hiyo ikifika watasema unajifanya unajua kuomba na kuombea watu, watasema eti anajidai Mungu anamtumia embu fanya muujiza tuone. Watakukejeli. Watasema anajifanya ana uwezo, ni mzuri sana maneno kama hayo hayakosekani. Saa hii ilipotokea kwa Yusuph mpaka ndugu walimuuza lakini aliposimama na Mungu alifanikiwa na utukufu wa Mungu ukamfunika. Shetani alimletea majaribu mengi ili amuangushe lakini alijitambua akamshinda.Hakuna taji ya utukufu pasipo taji ya mwiba! Yusuph alipitia mateso mengi sana lakini alipoweka tumaini lake kwa Bwana alishinda.

Saa hii ilipofika kwa Ayubu ilimwacha hoi sio eti inatokea kwa kuwa unadhambi hapana, ni lazima ije na kama hujapitia itakuja hata wakati wa siku zako za mwisho za kuishi. Saa hiyo Mungu anakaa pembeni kukupima je unaangalia tatizo au unamwangalia yeye.Utafikiri Mungu amekuzira, hakuoni unaweza hata kukufuru. Na ukitaka kujua Mungu amekuacha au yupo na wewe unaanza kuangalia tatizo na kuliona kubwa kuliko Mungu, unaanza kukata tamaa na hapo lazima utashindwa na kuangamizwa, lakini ukimwangalia Mungu na kumtegemea yeye pekee utashinda! Na utakapovuka MUNGU ATAWEKA HESHIMA KUBWA JUU YAKO.

Saa hii itakushawishi uingie mwilini ili ikupate na utakuwa umeshindwa (Petro alitumia upanga akakata sikio lakini Yesu akasema hapana Petro akarudishia lile sikio ina maana inatufundisha hatupigani kimwili) Tunatakiwa kuomba mara kwa mara na kumtegemea Mungu kwani saa hiyo ikifika hautaweza kuomba ni kama upo msalabani/umesulubishwa. Vita vyetu sio vya nyama na damu kitakachokuokoa ni haki. Kaza imani yako kumtafuta Bwana elekeza macho yako kwa Bwana kwani utakapoacha kumwangalia Bwana utakata tamaa na kuangalia tatizo.

Wana wa Israel walipokuwa wanaelekea Kanan walipomnungunikia Mungu alileta nyoka lakini Bwana aliporidhia na kuwaletea Yule nyoka wa shaba waliambiwa wasiangalie wale nyoka wenye sumu bali yule nyoka wa shaba. Iliwapasa kuangalia juu hata kama nyoka alikuwa shingoni walielekeza macho yao kwenye nyoka wa shaba ndiyo ilikuwa salama yao. Nasi tunapopita katika jaribu ni kumwangalia Yesu na sio shida tuliyonayo. Katikati ya shida tunatakiwa kumwangalia BWANA wa MABWANA kwani ukiangalia tatizo utavunjika moyo.

Saa ya mamlaka ya giza kwa Yohana mbatizaji, hata Yesu mwenyewe hakwenda kumwangalia gerezani, unapomwangalia Bwana unapata nguvu mpya Matendo 4:23-26.( mfano unapokuwa katika saa hiyo ukaonyeshwa unapaa kwenda juu inamaanisha utashinda)

Elia alipopita ile saa alimwomba Mungu afe, omba upite sio ufe. Angalia neno la Mungu na maagizo ya Bwana usije ukakosea. Saa hiyo ikikukuta dhaifu inakupeleka—Nguzo ni maombi na Neno, kama kuna mahali umekosea omba rehema na neema ya Mungu ikufunike ili uweze kuvuka. Kutoka 14:15 -16

Saa hii unaweza kurudi Misri, shetani atataka kukurudisha nyuma , Musa aliulizwa na Bwana mbona unanililia mimi? saa hiyo ni ya kusonga mbele sio kulia na ukitaka kujua Bwana yuko na wewe hautazama,hautakufa ninamaanisha matatizo hayatakushinda. Ni saa ya kutumia mamlaka ndio maana Musa alitumia ile fimbo sio kila mahali ni machozi mwenye mamlaka hatakiwi kulia ni saa ya kutamka,kuthibitisha mamlaka unayotembea nayo.

Maombi ya machozi yanalipa mbele za Mungu lakini sio wakati wote ni kulia, inapaswa kujitambua kama Mungu alishakupa silaha sio wakati wa kulia tena.

Paulo alipokutana na vita uso kwa uso (alipokutana na mchawi) fimbo ilikauka pale pale kuna vitu vipo ndani yako jitambulishe

Sisi ni miungu Zaburi 82:6 mauti na uzima vipo ndani ya Ulimi wetu. Kuvuka kwako kuko kwenye kinywa chako. Ila lazima tutambue ni mahali gani pa kuomba na ni mahali gani pakutamka. Katikati ya vita pita Mungu wako ataheshimika.Usirudi nyuma vita isikuchanganye, majaribu yasikuchanganye. Unaposonga mbele majaribu nayo yanaweza kuzidi ni mbele kwa mbele ukiweza mkumbushe Mungu ahadi zake, silaha yako kubwa iwe, maombi na kusoma neno la Mungu likae ndani yako kwa wingi.

Nenda faragha na Bwana kuwa na malengo, Kuwa hodari,shujaa, samehe, usibebe watu moyoni mwako, mbebe Yesu. Kuwa na mtumishi wa kukujenga kiroho ili saa ya mamlaka ya giza ikifika isikuweze. 2korinto 2:5-11. Nakumbuka mara ya kwanza nilipopitia kipindi hiki,niliposhinda niliponywa na kupata gari. Ila haikuwa rahisi, na ndipo nilipojifunza na kupata ujumbe huu.

Watu wote ni wazuri kabla shetani hajawavaa unapopambana na adui usimwangalie mtu,angalia ile roho iliyo ndani ya yule mtu inayotenda kazi ndani yake pambana kiroho sio kimwili unaposema una maadui sio mtu ni roho inayotenda kazi ndani ya hao watu.Mungu hutumia watu na shetani pia hutumia watu.

Acha ni waambie watu wa Mungu kila mtu ameitwa kivyake na kila mtu amejaliwa karama yake. Kanisa la leo imetupasa kujitambua, Waefeso 4:11-13 mchungaji asimame kwenye nafasi yake kama mchungaji achunge kondoo, Waalimu nao walishe kondoo/wafundishe, Wainjilist nao wahubirie watu waokoke, Mitume nao waweke msingi na Manabii nao wasimame kwenye nafasi zao, kukemea dhambi na kutuletea ujumbe kutoka kwa Mungu. Yesu alipenda wenye dhambi lakini alichukia dhambi tutamani kufanana na Yesu mwenyewe kwani yeye ndiye njia ya kwenda kwa Baba Yohana 14:6. Tuwe na upendo na umoja kama alivyosema Bwana wetu Yesu Kristo. Yesu aliishinda saa ya mamlaka ya giza na ndio maana tukilitaja Jina lake shetani anasalimu amri. Alishuka kuzimu akamnyang’anya shetani vilivyo vyetu na ku tukabidhi wale tunaomwamini na kumkiri kama Bwana na Mwokozi na huo ndio utukufu tulionao katika Yesu Kristo.Shetani hana nguvu kwa wale tulio ndani ya Yesu Kristo, anatuweza tu pale tunapokuwa kwenye himaya yake Yohana 15:4-8.

Nakumbuka nimewahi kumwona Yesu akiwa na kitabu kilichombeba yeye mwenyewe, kilichofanana naye, alikuwa mweupe kama sufi….nywele, sura, mavazi kila kitu kiasi kwamba sikuweza kumwona sawasawa. Kitabu kile kilifanana na y eye mwenyewe na alipoongea tu kilifunguka na aliponyamaza kilifunga. Kilikuwa kama maji au kioo kwani ndani ya hicho kitabu alionekana yeye mwenyewe hivyo nilipokuwa ninamwangalia na kuangalia kile kitabu ni kitu kimoja,hakukuwa na tofauti nikimwangalia yeye moja kwa moja au nikimwangalia kupitia kile kitabu, ni vigumu hata kuelezea.Hivyo niligundua Yeye ni neno. Tutamani kuwa wenyeji ktk bibilia.Maneno ya Mungu yakae ndani yetu kwa wingi.shetani anafunga ufahamu wetu tusipende kusoma neno la Mungu na hata tukisoma tusielewe hasa kitabu cha ufunuo, kama haujawahi kusoma kitabu cha ufunuo mpinge kwa kukisoma kuanzia sasa.

SIKU ZOTE TUKUMBUKE HAKUNA TAJI YA UTUKUFU PASIPO TAJI YA MWIBA! LAZIMA TUISHINDE SAA YA MAMLAKA YA GIZA WANA WA MUNGU!


Makala haya yameletwa kwenu na mtumishi wa Mungu Frida Blessing James kutoka ArushaEndelea kututembelea mambo mazuri yanakuja
 

 

No comments:

Post a Comment