Wednesday, September 11, 2013

Umuhimu wa Mwamini kutambua nafasi aliyo nayo


Leo nimejifunza kitu cha Ajabu katika Lunch Hour Fellowship naona ni vizuri nikakushirikisha.

Umuhimu wa Mwamini kutambua nafasi aliyo nayo lililohubiriwa na Bishop Lubala.

Kuna tatizo kubwa sana la mwamini kutojua nafasi ambayo Mungu ametupa. Waamini tunashindwa kutumia kanuni za kuishi hapa duniani ambazo Mungu ametupa matokea yake waamini tunaishi kama watu wengine tu wasio mjua Mungu wakati sisi tunacho kitu cha tofauti na cha thamani sana.

Kitu kinachozangaza ni jinsi ambavyo mwamini anajiita Mwamini yaani mtu aliyempokea Kristo lakini anashindwa kuamini Neno la Mungu.

Kama wewe ni Mwamini na umempokea Yesu katika Maisha yako jiulize maswali yafuatayo;

1.      Mwamini ni Nani

2.      Faida za Kuwa Mwamini

3.      Vitu gani vitakusaidia uwe mwamini Mzuri

4.      Kwanini unakuwa na hofu wakati wewe ni mwamini

Tusome Neno la Mungu kutoka Waraka wa Kwanza wa Petro 2: 5-10

“5 Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

 

6 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Tazama! Naweka huko sioni jiwe kuu la msingi, jiwe la thamani kubwa nililoliteua. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa."

 

7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, "Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi."

 

8 Tena Maandiko yasema: "Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu." Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo.

 

9 Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu. 10 Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea. “

Msisitizo wangu utakuwa katika msitari wa 9 na wa 10, Ukisoma huu msitari je ukiwa Mwamini ni kweli unaamini hivyo? Na unaishi hivyo?

Kama unaamini hivyo usingekubali yule jirani yako ambaye hamjui Kristo aendelee kukaa bila kumjua Kristo lakini kwasababu huamini hivyo umeshindwa kumshuhudia matokea yake Waamini wamejikuta wakishuhudiwa na watu wa mataifa na mara nyingine wamejikuta ndio wafuasi wa watu wa Mataifa kwasababu wameshindwa kuwashuhudia. Unakuta mwamini anaanza kuongea na kuishi kama mataifa kwasababu tu anaogopa kwamba hawezi hata kumtetea Yesu aliye naye kwahiyo anajiweka kama wao(Kuji-adjust).

Lakini napenda uende na huu mstari ukatafakari Mwamini ni Kuhani wa Kifalme,Taifa takatifu,Mtu wa Mungu mwenyewe,hebu angalia ilivyo na nguvu.

Hakikisha unalielewa Neno la Mungu na unalihishi usifanye neno la Mungu kama Pain Killer kwamba unalitumia pale tu unapopata maumivu fulani,liwe sehemu ya maisha yako na hata changamoto ikija hutatikisika, hazitabadilisha kuwa wewe ni Nani kwasababu unajitambua.

Wakorintho wa Pili 4: 5-6  “ 5 Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. 6 Mungu ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo.”

Raha ya maisha ya wokovu iko katika Neno la Mungu.

Amua Leo kubadilika Ishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu na Neno la Mungu na sio hofu inayotoka kwa Ibilisi.

Usiombe kwasababu unamuogopa Shetani omba kwasababu unataka mahusiano na Mungu na iwe ndio maisha yako, Amina

 

 

No comments:

Post a Comment