Shalom Mtu wa Mungu, leo nakuletea somo muhimu sana juu
ya kukubaliana na mwenzi wako jinsi mtakavyokuwa mnaishi na ndugu zenu, yaani
wakwe kwa upande wa mwanaume na mwanamke pia.
Ni muhimu mkaweka
msingi mapema maana wazazi na ndugu za pande zote mbili ni muhimu sana
sana kwenu wala hawahitajiki kuupuuziwa ila tu msipoweka mipaka inaweza kuleta
shida kubwa sana katika maisha yenu ya huko mbele mtakapokuwa mmefunga ndoa.
Wakati mwingine ndugu za pande zote mbili wamekuwa
wakijisahau na kufikiri wana nafasi ya kuamua juu ya maisha yenu kama wanandoa.
Lakini katika Biblia tunaona kuna mifano mingi jinsi wanandoa walivyoishi
vizuri na wakwe zao kukawa na uhusiano mzuri kati ya wakwe na mkwe kama Ruth na
Naomi walivyopendwa na kuishi vizuri na wakwe zao.
Lakini pia tunaona jinsi ambavyo Mfalme Daudi
alivyopata shida na baba mkwe wake Mfalme Sauli hadi Sauli akataka kumuua
Daudi.
Mahusiano mabaya kati ya mkwe na wakwe yanaweza
kusababisha wanandoa kuishi kwa shida kubwa sana na mara nyingine imesababisha
ndoa kuvunjika kabisa na kuleta chukizo mbele za Mungu.
Sasa ili kuepusha hayo ndio maana tuko hapa leo
kukuambia kwamba msije mkajisahau mkaongelea tu jinsi mtakavyojenga Masaki au
Kibada bila Kuzungumzia jambo hili mapema maana kama usipoliweka sawa hutaishi
kwa Raha, Ninaposema Ndugu hapa namaanisha ni mama,baba,kaka,dada,shangazi,mjomba,bibi
,babu na ndugu wengine wa kwako wewe au wa mwenzi wako pamoja na uzao wao.
Zingatieni yafuatayo ili kuepusha hiyo migogoro
inayosababishwa na ndugu;
1.
Zungumza na Mwenzako
Mzungumze jinsi mtakavyoweka mipaka kwa ndugu zenu wote
itayaepusha ndugu kuingilia mahusiano yenu
Kwa mfano sikilizeni ushauri kutoka kwa wakwe maana pia
ni mzuri sana kwasababu wao kwanza wameona mengi kuliko nyie ila kabla ya
kufanya maamuzi make chini mkubaliane lipi mfanye au lipi mliache kwanza. Kwa
kufanya hivyo mtakuwa na mahusiano mazuri maana mmeshirikishana kwenye maamuzi
juu ya mashauri mliyopata.
Ni hatari sana ukapigiwa simu na mama au baba au mjomba
wako kwamba mwanangu kuna kiwanja huku Mwabepande wewe kwa vile ulikuwa na hela
Bank ukaikimbizia huko ukanunua bila kumuambia mwenzako, halafu baadae ajue
kwamba umemruka katika maamuzi . Mshirikishe maana ndio unategemea kuishi naye
anaweza kukupa ushauri mzuri ambao utaweza kupata kitu kizuri na cha thamani na
saa nyingine kukuepusha na hasara.
2.
Muwe wazi kwa Ndugu na ishi nao kwa Akili
Inategemea na ndugu zenu wakoje na wanawachukuliaje,
kuweni tu wawazi kwamba Bwana ninavyomjua mchumba wangu hili jambo hatalikubali
labda uniruhusu nimwambie kwanza tusikie mawazo yake.
Ukimshirikisha kwanza kabla hujaamua atajisikia vizuri
na anaweza kuruhusu mfanye chochote na ndugu.
Kama mna ndugu ambao si warahisi sana kuelewa wanapenda
uchokozi ishi nao kwa akili jifunze kunyamaza ni silaha kubwa sana.
Ukinyamaza na kuongea na mwenzako kwamba nimenyamaza
kwasababu naona nikiongea naweza kuchochea moto zaidi atakuelewa kwamba
hujadharau ndugu zake na mtaweza kuomba Mungu aseme na hao ndugu waweze
kuwaelewa na kuwachukulia.
Kuwa wazi kwa ndugu kwamba kwasasa hatuwezi kufanya
maamuzi haya ya kifedha kwasababu hatuko vizuri kifedha labda kwasababu
tunajiandaa na maandalizi ya harusi au mambo mengine ambayo nyie mmeona ni ya
muhimu zaidi.
3.
Badilika
Kama ndugu wa mwenzako wanalalamikia tabia fulani
ambayo unayo jichunguze na ifanyie kazi ubadilike labda una dharau, majivuno na
kiburi ongea na Roho Mtakatifu atakushauri ni wapi ubadilike na atakuwezesha
kubadilika, Mungu anabadilisha watu san asana kuliko unavyodhani ila hawezi
kufanya mpaka umwachie.
Ila kama wanataka ubadilishe kitu ambacho kiko nje ya
uwezo wako na kiko nje ya mapenzi ya Mungu , zungumza na mwenzako mliombee hilo
maana watakuwa tu wanataka kuwavuruga au kutaka mjisikie vibaya. Maana kuna
rafiki yangu aliambiwa huyo mwenzi wako hatumtaki kwasababu anatoka kabla
fulani sasa hebu niambie je huyo dada angebadilisha Kabila wapendwa ilimhitaji
Mungu aingilie kati na kama ikiwa ngumu sana mumuone mchungaji wenu atawashauri
au atazungumza na hao wazazi.
4.
Watarajiwa mshirikishane kila kitu na kupendana kwa Dhati
Kama nilivyokwisha kusema huko nyuma watarajiwa inabidi
muunganishe na Upendo wa hali ya juu, Maana Neno linasema Upendo huficha wingi
wa Dhambi.
Kama mwenzako anakupenda hataona madhaifu yako bali
atakusaidia kwa upendo uweze kubadilika na sio kuungana na ndugu zake na
kukusema na kukukashfu.
Shirikianeni kwa upendo ili kuwa na bond, ndugu wakijua
mnapendana kwa dhati watakosa nafasi ya kuwahangaisha na Maneno ya mafarakano.
Mungu akubariki sana unapojindaa kuingia katika Hatua
hii ya Ndoa, na hata kama huna Mchumba soma haya na Omba Mungu kwa Imani ujue
kwamba yuko mtu wako aliyekuandalia kwahiyo usikate tamaa kaa mkao wa Kuoa au
Kuolewa muda si Mrefu Mungu anakutembelea, Aminaaaaaaaaaaaa!
Endelea kusoma Rejoice and Rejoice Mambo mazuri
yanakuja, na soma masomo ya huko nyuma yako masomo ya muhimu sana ya kukuandaa
kuwa mwanandoa mwenye ushindi Katika Kristo Yesu.
No comments:
Post a Comment