Friday, February 24, 2017

Mambo matatu Yanayokwamisha Malengo Yako - Joel Nanauka

Joel Nanauka
Kuna watu wengi sana wanaokufa na vipaji vyao,wanakufa na uwezo wao ambao kama wangeutumia basi ungeweza kuwasaidia sana kubadilisha maisha yao.Hata leo unaposoma makala hii,ndani yako kuna vipaji na uwezo wa kukufanya ufanikiwe kama utaanza kufanya mambo ambayo yamewasaidia wengine kufanikiwa pia.Katika saikolojia ya mafanikio imegundulika kuwa watu wengi wanapokuwa wazee sana huwa wanajilaumu kuwa hawakuishi maisha waliyotakiwa kuishi na walipoteza muda kutofanya yale ambayo yangeweza kubadilisha maisha yao.

Wengi waliohojiwa wakiwa wazee sana huwa wanasema wanatamani kupata fursa ya kurudia umri mdogo tena,na kama wakiipata hiyo fursa basi wataishi maisha yao kwa namna ya tofauti sana na vile ambavyo waliishi miaka yao yote iliyopita.Hii inaonyesha kuwa kama na wewe pia hautajua mambo ya kuyafanya kwa sasa unaweza kuingia katika kundi la watu ambao watakuwa wanajilaumu mara watakapokuwa wazee.

Nawe najua unasoma makala hii kwa sababu unatamani kufanikiwa kufikia kilele cha ndoto yako,lakini ukweli ni kuwa kama hautakuwa tayari kuchukua hatua madhubuti basi itakuwa ngumu sana kwako kufanikiwa.Uamuzi wa kufanikiwa hakuna mtu anayeweza kukufanyia isipokuwa wewe mwenyewe.

Mara nyingi uamuzi wa namna hii unaweza kutokana na kutaka kuepuka shida fulani au kutamani kupata raha fulani.Wengi waliofanikiwa walihusisha kitu kimojawapo kati ya hivi viwili.Kuna ambao walipitia hali ngumu sana katika maisha yao na kwa sababu hiyo walijikuta wamefika sehemu wamechukia maisha ya umaskini na wakakata shauri ndani ya mioyo yao kuanza safari mpya ya mafanikio,hawataki kabisa aidha wao au ndugu ama watoto wao wapitie hali ya mateso ambayo wao wamepitia.Wengine ni wale ambao waliishi maisha ya kawaida tu lakini wameona jinsi watu wengine ambavyo wamefanikiwa katika maisha yao na wao wametamani kuishi kama hao wengine.Katika maisha hakuna mtu anayefanikiwa kwa bahati mbaya,hata wewe kama unataka kufanikiwa ni lazima uamue kuanzia leo.

Swali la msingi ambalo ni muhimu kujiuliza ni kuwa;hivi kwa nini watu wanayajua haya ila hawachukui hatua?Leo nataka tuziangalie sababu kubwa 3 ambazo zimekwamisha malengo ya watu wengi:

Hofu ya kufanya jambo jipya

Ni ukweli ulio wazi kuwa kila mtu huwa hapendi kuondolewa kutoka mahali alipopazoea.Hii ndio maana kuna watu wakienda kanisani kila jumapili watakaa upande huohuo na wengine kiti kilekile na wakikuta kuna mtu amekaa huwa wanaona kama vile wamekalia kiti chao.Hata nyumbani,ukichunguza vizuri kuna watu huwa wanakaa kochi hilohilo ama kiti hichohicho wakati wa kula hata kama hajawahi kupangiwa kuwa akae hapo.Ndivyo ilivyo katika maisha ya kawaida watu wengi huwa hawapendi kubadilika.Kuna watu kila wakienda na kurudi kazini wanapita njia ileile kwa miaka nenda rudi,hata kama kuna njia nyingine hawajawahi kujaribu kabisa

Hebu jichunguze kitu ambacho unakifanya kwa sasa hivi umekuwa ukikifanya kwa muda gani na kwa nini haujabadilisha hadi leo.Leo fikiria kuna kitu gani kipya ambacho unaweza kuanza kukifanya kwenye maisha yako?Usikubali mwaka huu uiishe kabla haujaanza kufanya kitu kipya tofauti na unachofanya sasa hivi.Tajiri mkubwa wa marekani aliyekuwa anamiliki viwanda vya magari Henry Ford aliwahi kusema “Kama ukiendelea kufanya mambo yaleyale ambayo umekuwa ukifanya sikuzote basi utapata matokeo yaleyale ambayo umekuwa ukiyapata”.Je,unataka kuanza kuishi maisha ya tofauti?basi anza kufanya mambo ya tofauti kuanzia leo.

Hofu ya Kufeli/Kushindwa

Sababu nyingine inayowafanya watu washindwe kufanikiwa ni ile hofu ya kushindwa.Kuna watu wengi sana ambao wameogopa kufanya jambo fulani kwenye maisha kwa sababu ya hofu ya kuwa watashindwa.Mara nyingi,wazo la kwanza ambalo watu huwajia katika akili yao inapofika kufanya jambo fulani huwa ni “itakuwaje nisipofanikiwa?”.Kuna watu wanaogopa kufanya biashara kwa sababu ya kuwa na hofu ya kupata hasara,kuna watu wanaogopa kuomba kazi mahali kwa sababu ya hofu ya kukataliwa,kuna watu wanaogopa kuanza kulima kwa sababu ya hofu ya kupata hasara. Mtu mmoja mwenye hekima aliwahi kusema “Kila kitu ambacho kwa sasa hauna na unakitaka,kipo upande wa pili ukishaivuka hofu”.Mafanikio yako yamejificha nyuma ya hofu inayokukabili.

Kama kweli unataka kufanikiwa katika maisha yako ni lazima uanze kuishi katika namna ambayo hofu ya kufeli haina nafasi.hebu jiulize leo,kuna mambo mangapi ambayo unatamani kuyafanya lakini kinachokuzuia ni hofu ya kushindwa?Leo anza kuishinda hofu hiyo na anza kuchukua hatua mara moja.Kuanzia leo ningekushauri kutumia kanuni hii aliyowahi kuisema mwandishi maarufu sana wa marekani Jack Carnfield aliposema –‘Usiogope kufeli bali ogopa mafanikio ambayo unaweza kuyakosa unapoogopa kujaribu”

Kutumia visingizio vya kutokuwezekana

Jambo la tatu linalosababisha watu wafeli katika maisha yao ni ile hali ya kutumia visingizio walivyonavyo katika maisha yao.Wengine watatumia visingizio vya kutokusoma/kutokuwa na elimu ya kutosha,wengine watatoa visingizio vya hali mbaya ya uchumi,wengine watatoa visingizio vya familia walizotoka,wegine watatoa visingizio vya kukosa mitaji n.k.UKweli ni kuwa wakati wowote ule ukitaka kupata visingizio vya kutofanya jambo fulani basi utavipata vingi sana,ila kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima uamue kutokuwa mtu wa visingizio kabisa katika maisha yako.Mkufunzi wa mafanikio wa Marekani Jim Rohn aliwahi kusema “Kama kweli unataka kitu utatafuta namna ya kupata,ila kama hautaki basi utatafuta visingizio”.Ukiona unatoa visingizio vingi ni kwa sababu bado haujadhamiria kupata unachotaka.

Kuna mambo mengi leo ukiulizwa kwa nini huyafanyi ututaanza kutoa visingizio,kumbuka kuwa kila unapotoa visingizio unapoteza uwezo wako wa kutatua changamoto inayokukabili.Kuanzia leo amua kuwa mtu ambaye hautoi visingizio na badala yake uwe mtu wa kuchukua hatua.Kuna Watu wanatoa visingizio kila siku;watamlaumu mzazi,ndugu ama rafiki.Kama uantaka kufanikiwa basi wewe usiwe mmoja wao.Amua kuachana na visingizio kuanzia leo na anza mar amoja leo kufanya hiyo biashara, kilimo n.k Chukua hatua.

See You At The Top

©Joel Nanauka



No comments:

Post a Comment