MAISHA ni safari ndefu, kila mtu anapoamua kufanya kazi
huwa ana matarajio fulani.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Mchungaji Benjamin Bukuku
wa Huduma ya Kweli Itakuwaweka Huru yenye makao yake makuu Moshi mkoani
Kilimanjaro.
Mchungaji Bukuku alikuwa mfanyabiashara maarufu ghafla
akajikuta akichunga kondoo wa bwana.
Katika mahojiano yake na gazeti hili Mchungaji Bukuku
anaelezea safari yake ya kitumishi na mikakati aliyonayo kwa jamii ya Watanzania.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii katika ukumbi wa
Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, anasema ibada zake huwa
zinatolewa ndani ya ukumbi wa chuo hicho kila Jumapili.
Anasema katika maisha yake hakutegemea kuwa mchungaji
kwani alikuwa akijihusisha na ujasiriamali kazi aliyoipenda kwa sababu
ilimuingizia kipato.
Anasema hakupenda kufanya kazi ya utumishi kwani miaka
ya nyuma ilikua ni kazi duni, wachungaji wengi walikuwa na maisha magumu.
Anasema uchungaji haikuwa kazi ya kuitamani hususan kwa
aliyekuwa akijishughulisha na biashara ingawa alipenda kusaidia kazi ya Mungu
iweze kusonga mbele.
“Niliamini kwamba watu wakibadilika nchi itapona amani
itadumishwa, taifa litakuwa na watu wema wenye hofu ya Mungu hivyo
nilihakikisha katika kile ambacho Mungu ananijalia sehemu nasaidia kwenye
Injili.
“Siku moja katika hali isiyokuwa ya kawaida mzigo wa
kumtumia Mungu ulianza kuwaka moyoni, ghafla niliamua kufungua kanisa mjini
Moshi, mkoani Kilimanjaro.
“Nilifungua kanisa lijulikanalo kwa jina la Amani liko
chini ya Kanisa la Tanzania Assemblies Of God ambalo nililianzisha miaka ya 1980 hadi
hivi leo japo nimefungua makanisa mbalimbali vijijini malengo ambayo ninayo ni
kuhakikisha nafungua makanisa mengi vijijini na kuyasaidia kwa hali na mali.
“Kwa miaka yote hiyo nimefarijika kuwapa ujumbe wa
upendo Watanzania bila kujali tofauti za imani zao, mimi kwa muda mrefu
nimekuwa mdau wa amani popote niendapo nahubiri upendo pamoja na amani kwa
kutumia kauli mbiu yangu ya kweli,” anasema.
Akifafanua kauli mbiu hii ya “Kweli Itakuweka Huru”
anasema Watanzania wanatakiwa waambiwe ukweli kwani wakishaufahamu watawekwa
huru katika maeneo mengi ikiwepo magonjwa, uchumi na mambo mengine muhimu.
Lengo lake lingine anasema ni kukemea maovu na
kuwaambia watu kuachana na maovu ikiwepo kuwahimiza watu kufanya kazi kwa
bidii.
“Baada ya kufanikiwa sana mkoani Kilimanjaro sasa
huduma yangu ya kweli itakuweka huru imefungua tawi jijini Dar es Salaam…
Jumapili iliyopita ilikuwa ibada yetu ya kwanza mamia ya wakazi wa jiji
waliweza kuhudhuria mkakati ukiwa ni kuwafikia maelfu ya wakazi,” anasema.
Mbali na hayo anasema kwa sasa kuna tatizo la maadili
kwani miaka mingi kulikuwa na utamduni mzuri wa kupendana ambapo popote
Tanzania ukienda hakuna mtu yeyote anayeweza kukuuliza wewe unatoka dini gani.
Hilo anasema lilitokana kwa sababu jamii iliishi kwa
amani, upendo na undugu wa hali ya juu huku kila Mtanzania kuchagua imani
anayoitaka.
Naungana na kauli ya Rais Mstaafu mzee wetu Ally Hasan
Mwinyi kwa kauli yake iliyokuwa imejaa hekima za hali ya juu kwamba masuala ya
imani hayalazimishwi Katiba iko wazi mtu aabudu dini yoyote anayoitaka mradi tu
havunji sheria za nchi huu ndio utaratibu ambao tumeuzoa na umedumisha amani
yetu.
Maoni yangu kwa serikali iliyoko madarakani kwa sasa
isiogope mtu hata awe kiongozi wa dini kwani amani ikitoweka hakuna atayesalia
bali watu watakimbia ovyo.
Kwa mujibu wa mchungaji Bukuku atahakikisha anahubiri
ujumbe wa amani pamoja na upendo kwani ndio kazi ya viongozi wa dini.
“Viongozi wote wa dini ni vema tukaheshimu na kuzifuata
sheria za nchi na tusitumie vibaya sheria ya uhuru wa kutoa maoni, nionavyo
mimi kama atatokea kiongozi yeyote wa dini akatoa kauli inayohatarisha amani ya
nchi serikali isimuogope imkamate na imfungulie mashtaka.
“Pia kauli za baadhi ya viongozi wa dini zinachochea
hivyo ni vema serikali isiogope mtu hasa kwenye eneo la uvunjaji wa sheria,”
anasema.
Anasema kwa sasa amejipanga kuhakikisha anaeneza ujumbe
wa amani nchi nzima ambapo kwa kuanzia ameanza na Dar es Salaam, kisha
ataendesha semina mbalimbali pamoja na makongamano ya kuhamasisha masuala ya
amani na upendo.
Akizungumzia kazi za Rais Jakaya Kikwete anasema ni
mchapakazi mzuri na ana nia njema ya kuwatumikia Watanzania.
“Sisi kama huduma tumekuwa tukimuombea sana yeye pamoja
na baraza lake la mawaziri na serikali nzima kwa ujumla tatizo ninaloliona ni
la kimfumo ameingia madarakani amewakuta watu wamezoea mfumo fulani ambao
kuufumua ipo kazi,” anasema.
Kuhusu kusaidia jamii Mchungaji Bukuku anasema wamekuwa
wakisaidia wajane na yatima ambapo kipo kitengo maalum kabisa katika kanisa
lake kinachosaidia jamii.
Mbali na wajane anasema kitengo hicho pia huwa
kinawasaidia wachungaji wa vijijini.
Source: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment