Wednesday, March 15, 2017

Mahusiano Kuelekea Ndoa - 2

Na Azgard Stephen

Sir Azgard na mkewe
Habarini wana wa Mungu. Niliweka hapa somo hili, linalohusu mahusiano. Niliweka maswali kadhaa, naomba leo nianze na swali la kwanza lililohoji, upendo hasa ni nini?

Zipo definition na aina za upendo kadhaa zinazofahamika, ikiwemo aina maarufu ya upendo ijulikanayo kama AGAPE, upendo wa kimungu baina ya mtu na mtu na Mungu na mtu. Lakini pia upo upendo wa ndugu na rafiki, na upo upendo ule wa baina ya wapenzi ikiwemo mke na mume.

Huu wa mwisho hasa ndio nataka nizungumzie hapa. Nianze kwa kusema upendo huu ni hisia (feelings, emotions), hisia ambazo mtu mume au mke anazipata kwa mtu mahsusi, na kumuona mtu huyo kuwa sehemu yake. Hii najua ni ngumu kumeza, kwa wengi, kwani kwa wengi wetu upendo ni wajibu.

Kinachonifanya mimi nimpende Julieth kuliko wadada wengine wote ni hisia ndani yangu juu ya Julieth kuzidi hisia zangu kwa watu wengine wote.

Nawajibika kumpenda Yona, Herieth, Willy na Adeline, lakini kwa Julieth siwajibiki kwani iko katika hisia zangu muda wote na mahali pote. 

Hili ni muhimu, kwa mtazamo wangu, kulijua kwani huwa tunafanya makosa kupenda kwa wajibu pale tunapotaka kuingia kwenye mahusiano. Yaani tunasema, nawajibika kumpenda mchumba wangu no matter what! Ni sahihi kabisa, lakini si nzuri

Si nzuri kwa sababu kumpenda mchumba/mke wangu haitakiwi kuwa wajibu bali hisia chanya juu yake (strong feelings, emotions and affections). Yaani nikimuona moyo wangu unaruka, damu inabadili muelekeo na concentration katika jambo ninalolifanya inapotea, focus inakuwa kwake. Kwa mtazamo wangu, huu ndio upendo.

Sasa sisemi kuwa katika upendo huo hakuna kuwajibika, hasha, lakini nasema katika upendo huo unajikuta unawajibika kwa furaha (miaka 7 kama visiku vichache tu, Yakobo). 

Upendo huu hautoi jasho, bali unatoa bubujiko la raha moyoni.

Sasa kuna vitu vingi vinachangia kuchipusha upendo huu, vichache vikiwa ni hivi vifuatavyo;

1. Utu wa ndani wa huyo umpendae. Sura huzeeka, lakini utu wa ndani hudumu milele. Hii ni muhimu sana kwa hukufanya uendelee kumpenda huyo mpenzi/mchumba/mke wako hata pale utu wa nje unapochakaa

2. Sura ya huyo umpendae. Hapa mnaweza kunipiga mawe, lakini ukweli ni kwamba hii ni muhimu pengine kuliko tunavyofikiri. Kama kwa mfano wewe unapenda mkaka mwenye kifua kipana, halafu ukaingia kwenye mahusiano na mkaka mwenye kakifua ka njiwa, trust me, utakuwa majaribuni siku zote za mahusiano hayo. Unaweza ukashinda, lakini ukweli unabaki kuwa uko majaribuni. Kadhalika kama wewe unapenda mdada mwenye tumiguu twa soda halafu ukaingia kwenye mahusiano na mdada ambaye hajapewa hiyo miguu, my friend you are in trouble. Utashinda lakini ukweli unabaki kuwa uko vitani. Hapa sasa ndio kupe nda inakuwa wajibu, because you dont feel her. Ushauri wangu usimtie mdada/mkaka wa watu majaribuni, shambani mwa Bwana kuna kondoo wa kila aina, go for your type.

3. Mawasiliano baina ya watu nayo huchangia katika hili. Kwa mfano, mimi kipindi kile nikiwasiliana sana na dada Judy, kuna ukaribu unajengeka mioyoni mwetu,kuna namna tunahusiana. Communications brings relations, inategemea tu uhusiano gani utazaliwa. Watu wengi wameingia na wanaingia kwenye mahusiano kwa njia hii.

Hayo machache, yakiwemo mengine mengi uyajuayo, huzalisha hisia za upendo baina ya watu wawili wa jinsia tofauti.

Maandiko katika Mwanzo, kama ambavyo niliweka kwenye post iliyopita, yanatanabaisha hayo yote niliyosema.

Mahusiano ya Ibrahim na Sara yalijengwa katika mawasiliano, maandiko yanasema walikuwa ndugu wa baba mmoja. Lakini pia maandiko hayakusita kusema Sara alikuwa mzuri wa umbo, Rebeka alikuwa mzuri wa sura na Raheli alikuwa mzuri wa uso. Hata Yusufu maandiko yanasema alikuwa mzuri wa sura. Maandiko yasingeweka wasifu huu kama usingekuwa na mchango katika kile kilichotokea.

Lakini pia maandiko yaliweka wazi kabisa wasifu wa ndani wa Rebeka na Raheli, hali kadharika Yusufu.

Nikutakie baraka za Bwana.

Sir.Azgard

No comments:

Post a Comment