Tuesday, April 1, 2014

Mambo ya Msingi Kanisa linayoweza kupata kwa Kujua au Kufahamu Asili yake na Mwalimu Samwel Mkumbo


 Amani ya Kristo iwe pamoja nawe mtu wa Mungu, Karibu katika makala haya yanayoletwa kwenu na Mwalimu Samwel Mkumbo ambaye ni Graduate wa Chuo Kikuu Dar es Salaam na alikuwa Coordinator wa Fellowship ya God Kingdom Business (GKB)
 
Mwalimu Samwel Mkumbo
UTANGULIZI...

Lengo kubwa la somo hili ni kutazama ni vitu gani ambavyo kanisa la Tanzania na Ulimwengu kwa ujumla linakosa kwa sababu tu Kanisa halijachukua maamuzi ya kujua Asili yake na namna ambavyo MUNGU analitazama Kanisa.

Na labda niweke wazi jambo hili ya kwamba si azimio kubwa katika Somo hili kusema ASILI ya Kanisa kwa namna ya Historia ya kuzaliwa kwake kwa kutaja miaka au labda matukio ya muhimu, la hasha! Japo tunaweza kuangalia Historia kwa sehemu kidogo tu ikibisi kufanya hivyo ili kujua mambo mengi zaidi.

Maana ninajua wapo wazee wetu wa Imani na wenye kuijua Historia ya Kanisa la Tanzania na Ulimwengu kwa ujumla na wanafundisha hayo hivyo basi Azimio kubwa ndani ya Somo hili ni kutaka Kanisa lijue Asili yake kwa namna ya Uzao na Nafasi yake! Ndio! ASILI YAKE kwa kuangalia UZAO na NAFASI yake.

SEHEMU YA KWANZA

Moja ya jambo ambalo MUNGU analitaka ni sisi watu tuliookoka Kujua Asili yetu ndani ya Asili tuliyokuwa nayo. Yaani inapasa tufahamu kuwa sisi ni kina nani tunatoka wapi na tunakwenda wapi, naam ni watu wa shina na chipukizi gani?

Na mara kadhaa kwenye Biblia Mungu anataka na watumishi wake wanafanya juhudi kutaka kutujulisha asili ya Kanisa, maana tunapoijua asili ya Kanisa kuna mambo ya msingi tunayapata ndani yake na ambayo tusipojua asili ya Kanisa hatuwezi kuyapata, na hayo mambo si kama ni ya ziada kwamba tukiyapata sawa na tukiyakosa sawa, HAPANA! Ni mambo ya MSINGI na ni Muhimu sana Kanisa likafahamu kwa upana wake hasa vijana ambao kesho na keshokutwa ndio watakaokuja kuliongoza na kulilea Kanisa, ndio! Ni muhimu sana sana.

1 Petro 1:18 inasema hivi;

Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;


Sasa huo mstari hapo juu unaeleza mambo Matatu (3), Mawili ni tofauti, na la Tatu linafunganisha/linaunganisha hilo la Kwanza na la Pili. Lakini katika hayo Mawili nitafundisha moja tu katika Somo hili, maana huo mstari unaonesha mambo yafuatayo;

-UTHAMANI WA KANISA

-ASILI YA KANISA

Lakini hayo yote yanafungwa na neno UFAHAMU, maana yangu ni hii yote hayo Mawili niliyoyataja hapo juu, yaani UTHAMANI WA KANISA na ASILI YA KANISA tunatakiwa kuyafahamu.

TAZAMA NAMI:

…mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu… Inazungumzia UTHAMANI WA KANISA.

…mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;....Inazungumzia ASILI YA KANISA.

Nanyi mfahamu kwamba.,.. Sehemu hii ndio ya kwanza katika mstari huo inaunganisha yote hayo mawili, yaani anachotamani mtume Petro kwa Kanisa ni kwamba TUFAHAMU ASILI NA UTHAMANI wa KANISA.

Ngoja nikueleze jambo hili, KUFAHAMU jambo au KUJUA jambo Fulani ni muhimu sana, lakini KUJUA ASILI ya jambo Fulani au Nguvu ndio MSINGI WA KILA KITU ndani ya hilo unalolifahamu.

Itaendelea tena Wiki Ijayo siku kama ya Leo usikose, Barikiwa...

No comments:

Post a Comment