Thursday, June 5, 2014

KIVULI cha NAKALA HALISI na Mwalimu Frank Philip

Karibu katika makala haya ya Mafundisho ya Neno la Mungu yanayoletwa kwenu na Mtumishi wa Mungu Frank Philip.


Mwalimu Frank Philip
Katika maisha ya kila siku, tumekuwa na utaratibu wa kutumia KIVULI (copy) cha nakala HALISI (original), kwa matumizi mbali mbali. Mara nyingi, kama sio zote, kivuli cha nakala halisi huweza kutumika kama nakala halisi, hadi kuwe na ulazima wa kuonesha nakala halisi. Kwa mahali pengine, kivuli cha nakala halisi hakiwezi kusaidia kitu, hadi nakala halisi iwepo. Kwa matumizi ya kuanzia (preliminary use), kivuli cha nakala, huwa ni kitu cha msaada; kwa matumizi mengine maalum, kivuli hakimfai mtu kitu. Kwa mfano, huwezi kusafiri na kuingia nchi nyingine kwa kutumia vivuli vya nyaraka za kusafiria. Ndiyo ilivyo hata kwa nchi tunayoiendea baada ya maisha haya, jina lake ni Yerusalem mpya, ushukao kutoka juu. Huwezi kuingia na kivuli cha wokovu, unahitaji vazi halisi. Wokovu ni vazi jeupe, limeoshwa kwa Damu ya Mwana-kondoo. Huwezi kuingia kwenye karamu ya Mwana-kondoo bila vazi halisi.

Sifa moja kubwa ya kivuli cha nakala halisi ni kufanana sana, hasa kwa kubeba taarifa muhimu. Mara nyingi, kama sio zote, kulingana na kinakilishi (photo copier), ni vigumu kubainisha kati ya kivuli na halisi, hadi kwa kutumia vifaa maalum (counterfeit detectors). Bwana Yesu akasema, “acheni msing’oe, msije mkang’oa na ngano pia”! Hii inaonesha mfanano wa hali ya juu kiasi kwamba unaweza kung’oa ngano ukidhani ni gugu. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa watu wenye majina ya kuwa hai, kumbe! Wamekufa. Tunadhani tuko na wenzetu, kumbe ni kivuli tu! Dhambi huleta mauti. Atendaye dhambi ni wa Ibilisi, japo anaishi, amekufa. Kweli hatuokolewi kwa matendo ya sharia, ila matendo yako yatakufanya kuwa kivuli au halisi.

Kwa kuelezea jambo hili, Bwana Yesu alitumia mfano wa magugu na ngano (Mathayo 13:24-30). Kwa bahati mbaya, kila shamba la ngano huwa na magugu, tena mengi. Ndipo wanafunzi wake waliposhangaa, kwanini Bwana hakutoa kibali cha kung’oa magugu mara moja? Bwana Yesu alisema “acheni magugu na ngano vikue pamoja”. Angalia neno hili, wakati ngano inakua, na magugu yanakua pia. Laiti kimoja kingekua zaidi ya kingine, ndipo tofauti ingekuwa dhahiri. Lakini ona sasa, kila ngano ikuapo, magugu hukua pia!

Nikitizama mfano wa magugu na ngano najifunza mambo mengi. Kwanza, magugu na ngano yanaweza kuwa kiwakilishi cha jamii ambayo hapa naita “shambani mwa Bwana”, kwa lugha nyepesi, mkusanyiko wa waaminio. Sasa najua shambani mwa bwana ni zaidi ya mkusanyiko wa waaminio, lakini kwa sasa, nachukua kundi la wana wa Mungu kama ngano, na kundi la wana wa giza kama magugu. Ona jambo hili, wote wanakaa katika shamba moja; na Bwana anasema, usiwatenganishe, waache wakue pamoja! Pili, nikaona jambo hili kuwa la msingi sana, Je! Kama ngano ingetengwa kabisa na magugu, tungejuaje sifa za ngano fulani katika kupambana na mazingira yake? Nani angejua tofauti ya ngano bora na mbovu, dhaifu na njema? Kwa maana, kama ngano ikizidiwa na magugu, basi kila mmoja atajua udhaifu wake. Kumbuka imeandikwa “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo” (Ufunuo 21:17). Lakini kukiwepo na ngano ambayo itastahimili magugu, na kuzaa kati ya magugu hayo, na kuonekana kwa dhahiri tofauti yake baina ya magugu, hiyo itakuwa ngano njema na yakusifiwa. Naam, yafaa kutunzwa ghalani, kwa maana ni ngano njema. Kwa ngano dhaifu, mara ipandwapo, hukua ila ilitingwa sana na magugu, na yamkini kushindwa kuzaa, na hatimaye kufanana na magugu kabisa. Ngano dhaifu namna hii, isiyozaa, haina tofauti na gugu, kwa maana imefanana sana, japo kwa jina, inaitwa ngano, hiyo ni gugu tu.

Mara nyingi nimesikia watu wakilalamika juu ya wenzao makanisani, ambao kazi yao ni kuwaangusha wengine kwenye dhambi. Nikatafakari na kuona jambo hili, Je! Ngano yaweza kuwa gugu kwa sababu kuna magugu mengi na yenye nguvu? Nikaona tena na kutambua, yamkini kama sio ngano dhaifu sana, basi hiyo itakuwa nakala ya ngano halisi. Kwa lugha nyingine, tunaweza kuita “gugu lilofanana sana na ngano”, kumbe sio ngano na ni gugu tu. Tazama jambo hili, tunafundishwa kuutambua mti kwa matunda yake, je! na ngano haitatamblika kwa kuzaa ngano? Naam, kama ngano imo kwenye shamba la ngano, na haizai ngano, hiyo huwekwa akiba kwa moto, wakati wa mavuno ujapo. Tazama, yamkini imefanana sana na ngano hata kuzaa, ila inazaa mapooza. Ndipo mvunaji huja na pepeto lake mkononi (counterfeit detector), na kila kisicho halisi (kivuli) hutambulikana na kutengwa na kitu kilicho halisi (original). Hapo ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno.

Watu wengi wamefarijika kwa sababu ya kufanana na nakala halisi, bila kutafuta kujua kuwa wao ni halisi au kivuli tu. Utawakuta wako msitari wa mbele katika masinagogi, huduma, na hata wamebeba majina na vyeo vitakatifu kabisa. Haijalishi, gugu hukua pia; jinsi kulivyo na ngano zilizokua sana, hali kadhalika, kuna magugu yaliyokua sana. Nafasi zao na majina yao yamekuwa sana, ila kumbe ni magugu tu. Ona sasa, Bwana anasema, “acheni magugu msiyaguse hadi siku ya mwisho”, kuna pepeto (ungo) mkononi mwa avunaye, ndipo kila jambo litakuwa dhahiri sana. Je! Utafarijika na kujisifu, kisha kutosheka kwa sababu unakubalika na watu? Haya, kama mapepo yanakutii na ishara na miujiza inafanyika, ndio tujue kwamba wewe ni ngano? La! Hasha, Bwana aliwaambia wanafunzi wake “wasifurahi kwa sababu mapepo yanawatii, bali wafurahi kwa sababu majina yao yameandikwa mbinguni”. Mtume Paulo akijua hii shule ya Bwana wake, ndipo akasema “ajaponena kwa lugha za wanadamu na za malaika, ajapokuwa na unabii, imani TIMILIFU hata kuweza kuhamisha milima, kama hana upendo, yeye ni shaba iliyao na upatu uvumao; yeye sio kitu kabisa”. Ona jambo hili, magugu huweza kukua na kunakili mambo mengi sana, na kufanana sana na ngano, hata kutenda kama ngano. Ni juu yako kujikagua na kujijua kama wewe ni ngano au gugu, kisha kuchukua hatua.

Siku moja nilikuwa nasikiliza redio wakati wa mchana. Nikawasikia watangazaji wawili wa kike, wakijadili mada kuhusu ukahaba. Mmoja akasema “hivi kwanini tunawashangaa wale wajiuzao hadharani, wakikimbilia magari kutafuta wateja?” Ndipo mwenzake akasema, “tofauti ya hawa wasimamao barabarani na wengine, ni hali ya kujikubali na kutokuwa wanafiki, hawajifichi, wao ni malaya na si siri”. Mimi ningesema, hao wajiuzao kwa wazi ni magugu ambayo hayana haja ya kujifananisha na ngano. Ndipo mmoja wapo wa watangazaji akaendelea kusema, “siku hizi kuna watu wana kazi zao, na maisha yao, ila wana wateja wao na wanawasiliana kwa simu. Wengine, wana mahusiano ya aibu hata kama sio kwa malipo ya fedha. Tofauti ni namna ya kufanya biashara, huyu anataka pesa, na mwingine anataka kujifurahisha tu, hao wote ni kundi moja na jina lao ni moja, malaya”. Mimi ningeita hao wafanyao hayo kwa sababu yoyote ile, ila kwa siri kwa sababu wapo katikati ya wana wa Mungu, hao ni magugu yaliyojifananisha na ngano. Sasa ona tena, magugu haya yaliyojifananisha na ngano, kumbe yapo hadi kwenye nyumba za ibada! Ndipo mmoja hulamba asali, kisha kufuta mdomo na kujikausha, eti, kwa sababu kafanana sana na ngano, na yumo kati ya ngano zingize, hakuna ajuaye! Basi magugu ya namna hii, japo majina yao ni ngano, Bwana anajua walio wake, na anawataka wale walitajao Jina la Bwana wauache uovu. Mbona magugu mengine ndio yanalitaja Jina la Bwana kuliko hata ngano halisi? Naam, ndivyo ilivyo, ili yaweze kujificha vizuri katikati ya ngano. Siku yaja, kutakuwa na makundi mawili, ngano na magugu, nakupa shauri, chagua kuwa ngano halisi sasa. Kwa maana, kila jambo lawezekana kwa yeye aaminiye.

Kwa bahati mbaya, wakati mwingine magugu huwa na nguvu sana hata kutawala na kufunika ngano. Lakini tunatiwa moyo, “tusiogope sisi kundi dogo”. Hebu angalia maisha ya Bwana, akijua kwamba yeye ni Kuhani, tena mkuu sana asimamaye mbele za Baba, huku akijitoa mwenyewe kama sadaka ya dhambi, hakujali kuzingwa na magugu mengi na yenye nguvu. Alisimama katika nafasi yake, hata kuumaliza mwendo na kutimiza kusudi la Mungu maishani mwake.

Ona jambo hili, wakati wa huduma ya Bwana, kulikuwa na mfumo wenye makuhani tayari. Hawakumtambua, kwa sababu hakuwa katika ajira yao (payroll), hakuwa na vyeo vyao, hakusema kama wao, hakuvaa kama wao, hakuheshimiwa kama wao, lakini, alizidi kujinyeyekesha kwa sababu alijua neno hili, ufalme wake ni mkuu kuliko ufalme wa wanadamu. Hakutafuta vyeo na majina ya heshima. Walipomfukuza aliondoka zake; walipomkaribisha alikaa. Jina lake ni Mwana-kondoo. Ona sasa, hata watu wa nyumbani mwake na jamii yake hawakumkubali, ndipo Bwana akasema “nabii hana heshima ila kwa watu wake mwenyewe”! Je! Unataka heshima kwa sababu wewe ni nabii? Ndio, unaweza kupata heshima na mali nyingi, ila kumbuka, ili uwe mkuu katika Ufalme wa Mungu, imekupasa kuwa mdogo na mtumishi wa wengine. Ukijua kwamba yuko Bwana juu yetu, na sisi wengine, hakuna aliye bora kuliko mwenzake, na imetupasa kutangulizana na kumhesabu mwingine kuwa bora zaidi. Je! Umeona jinsi tumeharibu utaratibu huu? Tumetafuta kujulikana, mali, nguvu, heshima na vyeo. Kisha kuinua majina yetu kuliko Jina la Bwana wetu, kumbe sisi ni watumwa na vijakazi tu .Wengi wametafuta kuacha alama za majina yao duniani, kwa mfano wa mnara wa Babeli. Siku yaja, tutatoa hesabu ya roho za watu, na kudaiwa damu za watu vichwani mwetu, na wala sio minara mirefu.

Je! Wapo watafutao faida yao badala ya faida kwa Bwana wao aliyewaweka shambani? Je! Wapo waharibuo ngano kwa sababu wao ni magugu, na wanajificha kati ya ngano? Je! Kuna faida gani kuitwa ngano wakati unajijua kwamba wewe ni gugu? Tazama, Mungu ni wa rehema, kila amrudiaye Bwana atasafishwa na uovu wake kusahaulika kabisa. Huyo ataitwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, natazama yote yamekuwa mapya. Anza leo, wala mtu asikuhukumu kwa jana yako, kwa maana hatuendi jana, tunaenda kesho. Huko mbele ndipo kulipo na wokovu wetu; tunaokolewa kwa neema, lakini atakayevumilia hadi mwisho ndiye atakayeokoka.

Natazama, yuaja na mawingu kama alivyoahiidi. Yesu anakuja mapema. Shika sana ulichonacho asije mtu akaitwaa taji yako.

Frank Philip.

 

No comments:

Post a Comment