Tuesday, June 3, 2014

Uchumba hadi Ndoa: Sababu Kumi zinazofaa kumfanya mtu aamue Kuoa au Kuolewa


Karibu tena katika Makala haya yanayoletwa kwenu na Mshauri wako wa Ndoa na Mahusiano, Leo tunaendelea na Sababu Kumi zinazofaa kumfanya mtu aamue kuoa au kuolewa , tukimalizia sababu tano zilizobaki
 
Tuendelee

 

6.      Kuambatana na Urafiki kweli

Lengo kubwa la Ndoa ni wanandoa kuwa na mahusiano ya yaliyojengwa ndani ya urafiki na kuambatana

Rafiki ni mtu ambaye mnashirikiana katika mambo mengi, ni mtu unayependa kumuona na kuzungumza naye mambo yako, ni mtu ambaye ukiwa na huzuni utapenda awe wa kwanza kumwambia, ukiwa na furaha pia utamshirikisha furaha yako. Hata ikitokea mmetofautiana na kugombana na rafiki hutajisikia vizuri utatamani tu utafute njia ya kutatua mgogoro na urafiki uendelee.

Na marafiki wengi wa kweli ambao wamekuwa marafiki wa muda mrefu wamepita katika vipindi vingi, kuna kipindi wamegombana, wamekwazana na wamefurahi sana kwa pamoja lakini wameendelea kuchukuliana na dio maana urafiki wao unaendelea.

Hivyohivyo ndoa inapaswa kujegwa katika urafiki wa dhati na wa kweli, ili kuweza kuchukuliana pale mnapopishana

Kwahiyo ukitaka kuingia katika ndoa uwe Tayari kumfanya mwezi wako kuwa Rafiki hapo utafurahi sana katika ndoa, maana utakuwa huru kwa mwenzako, kumtania, kumweleza chochote, na hata kama hujafurahi utamwambia nay eye pia, na pale mnapokwazana kwasababu ni rafiki itakuwa rahisi sana kusulihisha mgogoro. Kwahiyo kijana na binti yangu ingia katika ndoa na mtazamo huu utakusaidia sana

Usije ukamfanya mwenzako baba au mama yako, mama na baba wana nafasi zao tunaziheshimu, mfanye mwezi wako kuwa rafiki, Haleluyaaaaaaaaaaaa

 

Hata Neno katika Mwanzo 2 : 21- 24 “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake,

na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.

Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.

Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.”

 

Mungu aliona ni vyema wana ndoa kuwa Mwili mmoja na kuambatana, hamwezi kuambatana pia kama sio marafiki ndio maana leo tumeona ndoa nyingi wameshindwa kuambata kwasababu mahusiano yao hayana urafiki, Mungu akusaidie wewe unayetegemea kuingia katika ndoa ujifunze hili na wewe uliyeko katika Ndoa basi anza leo kuwa na urafiki na mwezi wako ili muweze kuambatana, yaani mkifanya mambo yenu kwa pamoja

 

7.      Ushirika

Ndoa ni nafasi nzuri sana ya kuweka ushirika katika matendo,yamkini umelelewa katika mazingira ya ubinafsi mpendwa wangu ambapo chako ni chako, hakuna mtu anavaa hata ndala zako, au hata anayegusa kitu chako, sasa ukiingia katika ndoa ujue mambo yatakuwa tofauti, kama Neno la Mwanzo 2: 21-24 Ndoa ni kuambatana inabidi ufungue moyo wako kuwa Tayari kushirikiana na mwenzi wako katika mambo yote, katika huzuni, changamoto, hali ya kupungukiwa, furaha na raha, sio kwa vile leo umeolewa na mwenzako anavitu basi unashirikiana naye akiishiwa tu au wanavyosema wana dotcom akifulia unamkimbia si sawa, hiyo sio ndoa mpendwa. Jiweke Tayari kushirikiana na mwenzako hapo utaona maisha mazuri utakuwa unaimba haleluyaaaa

 

8.      Kusaidiana mahitaji ya kila mmoja


Katika Ndoa kila mtu ana mahitaji, kuna mahitaji ya kimwili, kiakili na kiroho, unapaswa kuwa tayari kuwa kumsaidia mwenzako anapokuwa na uhitaji wowote

Inawezekana mwenzako akahitaji msaada wa kiroho labda ushauri au maombi, uwe tayari kushirikiana naye na kumtia moyo, au akiwa na hitaji la kimwili uwe pia Tayari kumsaidia usikwepe hili ni jukumu lako na linaongeza vionjo katika ndoa, maana mwenzako utakapomsaidia atajua kwamba unamjali. Maana ni jambo muhimu sana mwanadamu akijua kwamba unamjali

 

9.      Kuinuana ili kufikia kusudi Mungu aliliwawekea duniani

Kila mtu Mungu alipomuumba kuna Kusudi aliloweka ndani ya maisha yake, namaanisha kila mtu usije ukamdharau mtu unayemuona ana suruali moja au sketi moja leo ukafikiri hapo ndio umeona mwisho wake. Unaweza kuwa umeolewa na mtu ambaye anaonekana kama vile hana mwelekeo labda au umeoa mtu ambaye unaona kwamba hana mwelekea labda, mustakabali wake haueleweki eleweki vile nakwambia hivyohivyo unavyomuona Mungu analo kusudi la ajabu ndani yake usimdharau.

Sasa Mungu anapokukutanisha na mwenzi wako unalo jukumu la kumsaidia aweze kufikia lile kusudi Mungu alilimuwekea duniani.

Tafuta kumsaidia alifikie kusudi lake la kiroho, kikazi na kijamii

Epuka sana kuwa kizuizi wa mwenzi wako kufanya kusudi ambalo Mungu amemuwekea duniani, maana utakuwa umeshiriki kuzuia kazi ya Mungu kufanyika, Haleluyaaa

 

10.  Kuinuana Kiroho

Ndoa ni kanisa, na baba ndio Askofu, mama mchungaji, watoto wainjilisti nakadhalika nakadhalika,

Inashangaza sana watu wengine kabla ya kufunga ndoa walikuwa ni watu wa kujitoa sana na kazi ya Mungu, kukiwa na mkutano jangwani yupoo, kukiwa na kuchangia kazi ya Mungu yupo, kuna Semina hapa na pale yupoo, Mkesha yupo wa kwanza, Maombi ndio usiseme tena ndio kiongozi, ghafla anaolewa stori inabadilika haonekani tena kanisani akija ni mara moja moja ndani ya mwezi anasingizia watoto , sijui kazi nakdhalika.

Mpendwa Ndoa aliyekupa ni Mungu maana ndio mwanzilishi wa Ndoa, kwahiyo uwezo wa kuhimili majukumu ya  Ndoa na familia utaipata kwa Mungu, muombe Mungu akusaidie usije ukafanya ndoa yako kuwa kizuizi cha Kutofanya kazi ya Mungu hapa duniani.

Kuna wadada wanashangaza saa nyingine labda ameolewa akabarikiwa kuwa mjamzito sasa  huo ujauzito wala hana excuse ya Doctor, lakini kanisani haendi tena kwasababu kweli ile hali huwa inaleta uvivu, sasa yeye anaflow na huo uvivu hadi anashindwa kuomba , sasa mpendwa unafikiri nani amekupa hiyo Zawadi  ya mtoto kwanini usiendeleze ushirika nae ili aendelee kukupa nguvu na kuku-kuzia huyo mtoto na kumlinda.

Kwahiyo wapendwa wangu mjue Kabisa mnapokwenda kuoana mnalo jukumu na kuinuana Kiroho ili kila mmoja afanye ule utumishi Mungu aliomuwekea ndani yako, wengine wanawazuia wenzi wao kufanya kazi ya Mungu wanawakatisha tamaa labda kwasababu wanaona hamna Hela, lakini mpendwa wangu Pesa sio suluhisho la kila kitu wakati mwingine ni vizuri kumtii Mungu, maana Baraka za kweli zinatoka kwake Mungu ndio atupaye Nguvu ya kupata Utajiri, Haleluyaaaaaaaaaaaa

 

 

Mungu akubariki sana mpendwa wangu, asante sana kwa Kutembelea Rejoice and Rejoice blog

 

Endelea kutembelea Rejoice and Rejoice blog mambo mazuri yanakuja, Aminaaaa

 

1 comment:

  1. amina amina
    huu ujumbe umekaa vema sana unafaaa sana kwa pande zote mbili kabla na baada ya kuoa. ningefurahi sana kama watu wangepitia mambo kama haya na kuyasoma

    ReplyDelete