Monday, December 12, 2016

MAOMBI YA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO - SEHEMU YA 5

Na Mchungaji Florian Katunzi - EAGT City Center

Bwana asifiwe mtu wa Mungu. Bado tunaendelea na mfululizo wa somo hili ambapo katika matoleo yaliyopita nilikufundisha juu ya funguo tatu na nikakwambia faida na namna ya kuzitumia. Na leo tunaendela na ufunguo wa  nne …

Endelea….

UFUNGUO WA NNE

MAOMBI
Maombi:  maana yake ni kusemezana na MUNGU au kutafuta uso wa BWANA; katika hali ya unyenyekevu na kicho “Toka mbinguni BWANA aliwachungulia wanadamu, AONE KAMA YUKO MTU mwenye akili, Amtafutaye Mungu.” Zaburi 13:2
Katika kipengele hiki tunakwenda kujifunza maombi kama ufunguo wa kufungua milango na malango yaliyofungwa.
 “BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikamuru nzige kula nchi, na nikiwapelekea watu wangu tauni; ilkiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima. 2Mambo ya Nyakati 7:12-16

Tunajifunza kwa mfalme Sulemani jinsi alivyo jinyenyekeza na kusimama madhabahuni pa BWANA ikiwa ni ishara iliyowazi ya kuwa BWANA ndiye mfalme wa wafalme astahiliye kuabudiwa na kutukuzwa. Hivyo tunajifunza mambo manne yafuatayo:-
(1) “Ikiwa watu wangu watajinyenyekesha” watu wa Mungu lazima watambue ushindi wao dhidi ya malango ya giza unapatikana ndani mwa maombi sio nje ya maombi. Mtu akijinyenyekesha sawasawa na Neno la Mungu hakika atashinda na zaidi ya kushinda. “… Ikawa, Musa alipoinua mkono wake, Israeli walishinda; na aliposhusha mkono wake Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa Yoshua akaangamiza amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga…” Kutoka 17:8-16
Kwa kuinua mikono yake kwa BWANA Musa anaonyesha wazi jinsi anavyomtumaini na kumwamini Mungu. Waamaleki walipotokea kupigana na Israeli lengo lao ni kuwazuia wasipite walifunga malango na milango kwa njia ya kuanzisha vita. Nguvu ya ushindi ya Israeli ilitegemea kudumu katika Maombi, Imani na utii kwa Mungu. Wakati maombi ya Musa yalipokoma (aliposhusha mikono) mtililiko wa nguvu za Mungu ulikoma kwa watu wa Mungu. Hii ikiwa dhahiri kwamba tunapoomba nguvu ya Mungu hushuka na kinyume chake tusipoomba hakuna nguvu ya Mungu inayoshuka. 

Pia tunajifunza ya kwamba Baraka za Mungu na Ulinzi wa Mungu havishuki hivhivi kwetu mpaka tuvishushe kwa njia ya Maombi. “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea naye atafutaye huona naye abishaye atafunguliwa.” Mathayo 7:7-8

(2) “Na Kuomba” maana yake, watu wa Mungu lazima waombe kwake bila kukoma kwa ajili ya kupata rehema na neema zitokazo kwa Mungu na lazima wamtegemee moja kwa moja na kumwamini yeye aingilie kati. Bwana Yesu Kristo anasema; “…imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa.”
Luka 18:1-
Katika maisha ya imani yako mapito mbalimbali yenye magumu, vita, dhiki, njaa, magonjwa na adha mbalimbali ambazo mtu wa Mungu anakabiliana nazo (changamoto za maisha). Pamoja na changamoto zote hizi hatukati tamaa bali tunatiwa nguvu katika yeye Kristo Yesu. Maandiko matakatifu yanasema “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa n je unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.” 2Wakorintho 4:16-18

(3) “Kutafuta uso wa Mungu” Watu wa Mungu ni lazima wamrudie Mungu kwa bidii na kwa moyo wote na kutamani uwepo wake na sio tu kujaribu kukimbia shida ndipo milango yao na malango yao yatakapofunguliwa siku zote za maisha yao. Katika maisha ya huduma ya Yesu Kristo hapa duniani aliutumia ufunguo huu wa kuutafuta uso wa Mungu aliye hai na maombi yake yalisikiwa na uweza wa Mungu ulikuwa ukimtoka na kuponya watu. Alianza kwa maombi (Luka 4:1-14), akadumu katika maombi (Luka 6:12-19)  na kumalizia katika maombi (Luka 22:39-46).  Tofauti sana na maisha ya wakristo walio wengi ambao huomba wakati wa shida na majaribu.  “Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na ingawa ni mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu ya milele kwa watu wote  wanao mtii; kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki” Waebrania 5:7-10

(4) “Kuziacha njia zao mbaya” Watu wa Mungu ni lazima watubu kwa kweli ya Mungu na kuziacha njia zao mbaya ndipo maombi yao na dua zao zitasikiwa. Bwana Yesu Kristo alisema “… amin, amin, nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani siku zote; mwana hukaa siku zote. Basi mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kwelikweli.” Yohana 8:34-36

Hivyo BWANA anataka kabla ya mambo yote katika maisha yetu tufanye maombi kwa sababu ndiyo ufunguo unaofungua njia. Pasipo kufungua milango na malango kwanza hatuwezi kupenya kiroho na kimwili. Tukisoma maandiko matakatifu yanaonyesha dhahiri hakuna mtu wa Mungu aliye shinda pasipo maombi tangu baba zetu wa imani mpaka manabii walishika sana ufunguo huu wa maombi. “Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukurani, zifanyike kwa ajili yua watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na imani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.” 1Timotheo 2:1-6

Haya ni Maombi yenye kujengwa katika Msingi wa Neno la Mungu,
Imani itokanayo na Neno la Mungu. Mwombaji ni lazima Aombe sawa sawa na Neno la Mungu.

Yesu baada ya kubatizwa kabla ya Huduma alianza kwa Maombi, ambayo yalifanya mbingu zimfungukie. Kwa mantiki hiyo tunajifunza yakuwa Maombi ufungua malango na milango ya mbingu. Tunaona mfano wa Kristo Yesu kama kielelezo; 
“Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua, sauti ikitoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, nimependezwa nawe.” Luka 3:21-22

Katika maisha yetu ya ukristo tukitaka kufungua milango na malango kwa ajili yetu wenyewe, kwa ajili ya watoto wetu, kwa ajili ya mali zetu sharti tutumie kwa bidii ufunguo huu wa Maombi, sawasawa na ushahidi wa Neno la Mungu lilivyonenwa kwa kinywa cha mtumishi wa Mungu Ezra alipokuwa anaongoza watu wa Mungu toka uahamishoni Babeli kwenda kujenga na kufungua milango na malango ya Yerusalemu. pamoja na kuwa na kilakitu cha kujengea kama vile dhahabu, fedha na vitu vingi vya thamani. Ezra hakuvitegemea hivyo bali aliutegemea mkono wa BWANA ulio hodari ndio maana aliitisha mbiu ya kufunga na kuomba ili kujitafutia njia iliyonyooka itokayo kwa Mungu kabla ya kuanza safari. Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote. Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani, kwa maana tulikuwa tumesema na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao. Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali.” Ezra  8:21-23

Yako mema toka kwa Mungu aliye hai kwa Mwombaji. MBINGU ZIKIFUNGUKA ndani mwa Maombi, Magonjwa yataondoka katika miili ya watu, Maana Maombi hushusha Uweza wa Ki-Mungu wenye nguvu ya kufungua Mafungo yote. Yesu Kristo baada ya Kuomba, Mbingu zilifunguka, kilichotokea ni Udhihirisho wa nguvu za Ki-Mungu zenye kuponya watu.

“Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba. Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya.” Luka  5:16-17

UWEZA WA BWANA ndio unaofungua Malango na Milango kwa Mwombaji. Pasipo Maombi hakuna kitakacho tendeka katika maisha ya mkristo anaye mtegemea Mungu. “Ikwa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake, akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita mitume, Simoni, aliyemwita jina pili, Petro na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simon aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemuu, na Pwani ya Tiro na Sidoni, waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakita kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.” Luka  6:12-19

Yesu Kristo, anafanya Maombi usiku kucha maana yake anakesha katika Maombi. Matokeo yake ni Udhihirisho wa nguvu na uweza wa ki-Mungu unashuka kwa watu na kuwaponya. Ndani mwa maombi ndimo tunamovishwa Uweza na Nguvu za ki-Mungu aliye hai zenye kuangusha malango na ngome za kuzimu.

Yesu Kristo alikuwa na uwezo katika Kutenda na Kunena, lile Neno alilolisema kwa watu liliambatana na Uwezo na Nguvu. Maana wako watumishi wengi wa Mungu ambao wananena tu lakini neno lao halina nguvu matokeo yake kondoo wa BWANA wanaingia na mizigo yao kwenye ibada na wanatoka na mizigo yao. Kukosa funguo za ufalme wa Mungu ni jambo la hatari kwa mtumishi wa Mungu.

Unapomwendea Mungu sharti ujue unasimamia Neno gani la Mungu, maana Mungu hulituma Neno na ndani yake ndimo ulimo Uzima. Katika maisha yetu ya wokovu tunaweza kukutana na watu wengi wenye wivu na nia ovu, kama hawa makuhani wa kisadukayo kwa wivu wao waliwakamata mitume wakawatupa gerezani lakini kwa mkono wa BWANA wenye nguvu alituma malaika wake akawafungua mafungo yao;  sawasawa na Neno la Mungu. Toka kitabu cha Matendo ya Mitume 5:18-20 Neno linasema; “Wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza, lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu.”  

Hapa tunajifunza ya kuwa hatuko peke yetu katika mapito yetu yuko asiyeshindwa. Wajapofunga magereza yao, wajapofunga ndoa zetu, wajapofunga watoto wetu wasiolewe, wajapofunga uchumi wetu yatupasa tumwite Mungu aliye hai naye hakika atatufungua maana kwa msaada wa BWANA tutatenda makuu, na maadui zetu tutawakanyaga kwa nguvu zake. Japo gereza liliendelea kulindwa na walinzi na malango yake na milango yake kufungwa BWANA aliposhuka ndani ya gereza alifanyika mlango wa kutokea.  “Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, wakisema, gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani.” Matendo 5:22-23

Kila kilicho kamatwa kikawekwa ndani ya Gereza la Kiganga na Kichawi, gereza la magonjwa, gereza la nyumba ndogo, gereza la kuzaa kufa kufa na mapooza, gereza la kufeli katika masomo/ kutokufaulu katika mitihani, gereza la uchumi, Lazima VITAFUNGULIWA.

 “Basi watu wote wakulao wataliwa, na adui zako wote watakwenda kufungwa, kila mmoja wao, na hao walio kuteka nyara watatekwa, na wote waliokuwinda nitawafanya kuwa mawindo. Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA” Yeremia  30:16-17

BWANA akufungulie Mlango na Milango sawa sawa na Kuomba kwako. Mungu analiangalia Neno lake apate kulitimiza, hivyo Omba sawa sawa na Neno utapata jawabu lako. Usiogope, Maana hutapatwa na aibu tena; Tunayo mamlaka ya kugeuza kila hali sawasaw na Neno la Mungu alilonena kwa kinywa cha nabii Isaya na kusema; “Nimeziona njia zake; nami nitamponya, nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia.” Isaya  57:18

Maombi yanafungua Malango na Milango ya Mbingu. Naye BWANA humwongoza daima mtu Mwombaji na Kuishibisha nafsi yake mahali pasipokuwa na maji na kumtia nguvu. Sawasawa na Neno la Mungu lililonenwa na kinywa cha nabii Isaya“Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.” Isaya  58:11

AYUBU aliomba Ustawi kwa ajili yake, kwa ajili ya watoto wake na mali zake. Akatoa Sadaka za kuinuliwa mbele za Mungu aliye hai akiziambatanisha na Maombi yake. Naye BWANA akamwitikia na kumstawisha katika hayo aliyoyaomba na kuyatolea sadaka.

 “Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote. Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa UKINGO pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.” Ayubu 1:5-10
Katika fungu hili la Neno la Mungu tunapata kielelezo cha mtu wa imani, mchaji wa Mungu, mwelekevu na aliyejiepusha na uovu. Tunapata taswira ya maisha yake ya kiimani jinsi alivyo yajenga katika msingi wa maombi, hata wakati wa mapito yake BWANA aliendelea kuwa Ukingo kwake. Ndiyo maana alisema “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, nay a kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; nami nitamwona mimi nafsi yangu, na macho yangu yatamtazama wala si mwingine…” Ayubu 19:25-27 

Ayubu alifanya maombi maalumu kwa ajili ya watoto wake hakuwaacha wajiendeendee bali alisimama kama kuhani wa familia yake, akawainua mbele za Mungu kwa maombi na sadaka. Nasi katika maisha yetu tumepewa ukuhani usioondoka katika Kristo Yesu. Yatupasa kusimama imara katika maombi kuyafungua malango na milango, kwa ajili yetu sisi, watoto wetu na mali zetu. Kwa kuwa Mungu anamtafuta mtu miongoni mwetu atakayesimama mbele zake mahali palipo bomoka na kujenga boma. “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.” Ezekieli 22:30

No comments:

Post a Comment