AINA TANO ZA FUNGUO ZA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO
Na Mchungaji Florian Katunzi - EAGT City Center
UFUNGUO WA TANO
NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU
Neno
“Nguvu” kwa lugha ya Kigiriki ni (dunamis) ina maana ya zaidi ya Nguvu au Uwezo
wa kawaida. “Inaashiria hasa nguvu iliyo katika utendaji wa ki-Mungu, hii ni
nguvu zaidi ya nguvu.
(Dunamis
is not just any power; it is miraculous power or marvelous works. Dunamis can also
refer to “Moral power and excellence of soul according to the Greek lexicon).
Nguvu ya Roho mtakatifu inajumuisha mamlaka ya kutoa pepo wachafu na upako wa
kuponya magonjwa. Roho mtakatifu ndiye ufunguo wa kumshinda adui shetani na
kazi zake. Roho mtakatifu ni zaidi ya nguvu ama uweza. Katika maandiko
matakatifu, Yesu kristo alionyesha unafsi wa Roho mtakatifu kwa kumwongelea
kama nafsi ambapo alisema; “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli
yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia
atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.” Yohana 16:13
Kimsimgi
tunajifunza kwa Yesu Kristo kabla ya kuanza huduma yake hapa ulimwenguni,
alipokwisha kubatizwa na Yohana mbatizaji, wakati anaomba mbingu zilifunguka
Roho mtakatifu akashuka juu yake kwa Nguvu tangia hapo maandiko matakatifu
yanathibitisha “Ikawa watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye
anaomba, mbingu zilifunuka; Roho mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa
kiwiliwili, kama hua, sauti ikatoka mbinguni wewe ndiye mwanangu mpendwa wangu
ninyependezwa nawe.” Luka 3:21-22
Tunajifunza
katika maandiko haya yakuwa Nguvu ya Roho mtakatifu haishuki kwa mtu hivihivi
mpaka awe anaomba. Lakini wako wakristo wengi wanaotaka kujazwa Roho mtakatifu
wakati hawana maombi katika maisha yao. Maombi ufungua mbingu zimfungukie
mwombaji. Baada ya Yesu kristo kujazwa Roho mtakatifu, maandiko matakatifu
yanashuhudia wazi yakuwa aliongozwa na Roho muda wa siku arobaini katika maombi.
“Naye
Yesu, hali amejaa Roho mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho
muda wa siku arobaini nyikani.”
Luka 4:1
Pia
yunajifunza ili milango na malago ya ukombozi wa mwanadamu yapate kufunguliwa
ilibidi Roho mtakatifu ashuke kwa nguvu na uweza mkuu ili kumfunika mwanamwali
bikra apate uwezo wa kubeba mimba pasipo kukutana na mwanamume kwa jinsi ya
kibinadamu.
“Mwezi
wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina
lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake
Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia
nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye
akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna
gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.
Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yesu.
Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha
enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme
wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili,
maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, ROHO MTAKATIFU ATAKUJILIA JUU
YAKO, na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu ya hicho
kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, mwana wa Mungu.”
Roho
mtakatifu akishuka kwetu huja na nguvu zake aliye juu katika Uwezo na nguvu za
Roho Mtakatifu, tunavishwa uwezo wa kuangusha ngome zote zilizofunga Malango na
Milango yetu ya Baraka za kiroho na kimwili, ndiyo maana Bwana Yesu kristo
alisema, Mtapokea nguvu akisha kuwajilia Roho Mtakatifu. Mkristo nguvu yako
haimo katika vitu vya upako kama vile; mafuta ya upako, maji ya upako, sabuni
za upako, chumvi ya upako, kitambaa cha upako, udongo wa upako, kiganja cha
nabii wa upako nambo yafananayo na hayo yanayoibuliwa kila kukicha katika ibada
zilizotungwa kwa akili za binadamu. Ndugu mpendwa katika kristo yachunguzeni
maandiko vema; mpate kuijua kweli inayoweza kuwawekeni huru mbali na mateso.
Tukiwa na msimamo thabiti wa kiimani yatupasa kuliamini Neno la Mungu sio
maneno ya watu, watawaijieni kwa mfano wa wanakondoo lakini ndani ni mbwa mwitu
wakali. Maagizo ya Yesu Kristo aliye mwanzilishi wa huduma hii iliyokubwa na bora
anasema; “Lakini mtapokea nguvu, akiisha
kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Matendo
1:8
Yesu
kristo aliwaambia wanafunzi wake msitoke Yerusalemu bali mwingojee nguvu ya
Roho mtakatifu, ambayo kwa hiyo watatenda kazi ya kufungua waliofungwa. Maana
pasipo huyo Roho mtakatifu hakuna atakayeweza. Tunaona akina Petro na Yohana
baada ya kupokea Nguvu ya Roho mtakatifu waliweza kunena habari za Kristo Yesu
na ufalme wake kwa ujasiri na nguvu. Hata wengi walistaajabu walipoona ujasiri
wao. “Ndipo Petro akijaa Roho mtakatifu, akawaambia, enyi wakubwa wa watu na
wazee wa Israeli … wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana
hapana jina jingine katika mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa
kwalo. Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na wakajua ya kuwa ni watu
wasio na elimu, wasio na maarifa wakastaajabu wakatambua ya kwamba walikuwa
pamoja na Yesu.” Mdo 4:8-13
Kwa
hiyo Roho mtakatifu akiwa kwa mtu hujidhihirisha kwa madhihiriho ya ishara,
miujiza na maajabu ambayo huwastaajabisha wengi wayaonapo. Roho mtakatifu
uhuisha nafsi zetu na miili yetu toka kwenye mafungo ya giza kwa kutufungulia
malango na milango. Tunajifunza kwa Lazaro alipougua, akafa, akazikwa kwa muda
wa siku nne alikuwamo kaburini lakini kwa nguvu za Roho mtakatifu Yesu alipaza
sauti yake akamwita Lazaro toka kwa wafu akawa hai tena. Hata sasa Roho
mtakatifu bado anatenda kazi kwa wote waaminio maana tukimwita katika Kristo
Yesu ushuka kuokoa na kuponya wengi. Hata kama lipo kaburi limefunga maisha
yako ya kiroho na kimwili kwa uweza na nguvu za Roho mtakatifu sharti
ufunguliwe. (Through Power of Holy Ghost we Force out evil spirit). Maandiko
yanasema katika injili ya Yohana; “Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa
Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndie Mariamu yule
aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye
alikuwa hawezi. Basi wale waumbu wakatuma ujumbe kwake wakisema, Bwana, yeye
umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali
ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo. Naye
Yesu alim,penda Martha na umbu lake na Lazaro. Basi aliposikia ya kwamba
hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha, baada ya hayo,
akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena. Wale wanafunzi wakamwambia,
Rabi, juzi juzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe
unakwenda huko tena? Yesu akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu
akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. Bali akienda
usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake. Aliyasema hayo; kisha baada
ya hayo, akawaambia, Rafiki yrtu, Lazaro amelala, lakini ninakwenda nipate
kumwamsha. Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona.
Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena
habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa.
Nami nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; lakini na
twendeni kwake. Basi Tomaso, aitwaye pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe,
twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye. Basi
Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. Na Bethania
ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadri ya maili mbili hivi, na watu wengi katika
Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya
ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba yesu anakuja, alikwenda kumlaki, na
mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, bwana, kama
ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo
yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, ndugu yako atafufuka.
Martha akamwambia, najua yakuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu
akamwambia, mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa,
atakuwa anaishi, naye kila aishie na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je!
Unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe
Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimmwenguni. Naye alipokwisha kusema hayo,
alikwenda zake, akamwita umbu lake Mariamu faraghani, akasema, Mwalimu yupo
anakuita. Naye aliposikia aliondoka upesi, akamwendea. Na Yesu alikuwa hajafika
ndani ya kijiji, lakini alikuwa akalipo palepale alipomlaki Martha. Basi wale
Wayahudi waliokuwapo na Mariamu nyumbani, wamfariji, walipomwona jinsi alivyoondoka
upesi na kutoka, walimfuata, huku wakidhani ya kuwa wanakwenda kaburini ili
alie huko. Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka
miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu
hangalikufa. Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye
wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, akasema, Mmemweka wapi?
Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. Yesu akalia machozi. Basi Wayahudi wakasema,
angalieni jinsi alivyompenda. Bali wengine wao wakasema, je! Huyu aliyemfumbua
macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife? Basi Yesu, hali akiugua
tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe
limewekwa juu yake. Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki,
akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. Yesu akamwambia,
Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? Basi wakaliondoa
lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, baba, nakushukuru kwakuwa
umenisikia. Name nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote; lakini kwa ajili ya
mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kukusadiki kwamba ndiwe
uliyenituma. Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku
nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso
wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.” Yohana 11:1-44
Roho
mtakatifu huleta uzima badala ya mauti; akatoka nje maana yake, akahuwishwa
Lazaro toka kwa wafu japo alikuwa amekufa na ameoza. Ijapokuwa alikuwa ananuka,
nguvu ya Roho Mtakatifu iliposhuka juu yake aliyekuwa katika hali ya kufa
ikamwinua Lazaro toka kwa wafu akawa hai tena. Ni vema kila mmoja aliyeamini
kutambua kuwa Roho mtakatifu ni Ufunguo unaotoa nafsi nyingi katika mafungo ya
giza. Kwa nguvu za Roho mtakatifu hata kazi zetu za kimwili zaweza kuhuishwa
inaweza kuwa Biashara, Kazi, Elimu vyote vilivyozikwa na kufishwa kuwa hai
tena. Kama BWANA alivyonena kwa kinywa cha nabii Ezekieli na kusema; “Nanyi
mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa
ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani
yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa
mimi, BWANA, nimesema hayo, na kuyatimiza, asema BWANA.” Ezekieli
37:13-14
Kwa
nguvu za Roho mtakatifu sharti malango na milango vifunguliwe ndani mwa maombi
sio nje ya maombi kwa kuwa tunapomlilia Mungu na kumwita, yeye hushuka na
kutufungua mafungo yetu yote. “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa
nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama pazia la hekalu likapasuka vipande viwili
toka juu hata chini, nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka, makaburi yakafunuka;
ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala, nao wakiisha kutoka makaburini
mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.”
Mathayo 27:50-57
Nchi
ilitetemeka
Wakuu
wa anga lazima watetemeke maana Roho Mtakatifu ni nguvu iliyo juu ya yote
lazima Wakuu wa nchi washushwe, Wakuu wa giza washushwe, Wakuu wa majini
washushwe katika viti vyao kwani Kila goti lazima lipigwe mbele ya Kristo Yesu
Mwokozi.
Miamba
ilipasuka
Wako
watu wamefungwa nafsi zao katika miamba na majabali mazito, lazima ipasuke ili
wote waachiliwe waliofungwa vifungo kwenye miamba kupitia nguvu ya Roho
mtakatifu.
Makaburi
yakafunuliwa
Kaburi
ni kifuniko kibaya sana kinachotesa wengi. Wengi wanafunikwa makaburini kupitia
makafara ya tambiko. Kwa nguvu za Roho Mtakatifu miili mingi ya watakatifu
waliofungwa na nguvu ya kaburi watainuka.
Kama
pazia la hekalu lilivyopasuka, ndivyo kila kizuizi kilichowekwa katika maisha
yako ya kiroho na kimwili kitapasuka toka juu mpaka chini. Huu ndio ulikuwa
mwisho wa Agano la kale na kuwa mwanzo wa Agano jipya. Katika Kristo Yesu
yakale sasa yamepita tazama yamekuwa mapya. Katika ulimwengu wa Roho watu wengi
wamefungwa na mapazia ya mabibi na mababu zao, mapazia ya kiganga na kichawi,
mapazia ya mizimu na matambiko, lazima tuwafungue watu wa Mungu mapazia hayo
ndani mwa maombi haya ya kufungua milango na malango. Yesu akasema mfungueni
sanda mwache aende zake. Ikiwa na maana Lazaro alipofufuka alitoka kaburini
akiwa amevaa sanda (vazi la wafu) ndiyo maana Kristo Yesu aliagiza avuliwe hilo
vazi yaani sanda ndipo aachwe huru aende zake. Hapa tunapata siri nzito ya
kiroho ya kuwa wako wakristo wengi waliookolewa toka katika mafungo ya giza
lakini hawajahamishwa na kuingizwa katika ufalme wa mwana wa pendo lake. Ni jukumu
letu watumishi wa Mungu kufanya maombi na maombezi ya kuwafungua watu baada ya
kuamini. Maana KWELI ya Mungu kupitia Neno ndiyo inayomuweka mtu huru mbali na
mateso. Ni muhimu sana tukafundisha na kuombea sawasawa na Neno la Mungu. Maana
wako wanaodhania ya kuwa baada ya kuokoka vita vyao vimeisha kumbe wokovu ndio
mwanzo wa vita vya kiroho na kimwili. Kwa mantiki hiyo ndiyo maana Bwana Yesu
akawaambia wanafunzi wake; “Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni,
roho i radhi ila mwili ni dhaifu.”
Marko 14:38
Hata
wana wa Israaeli walipokwisha kuokolewa toka utumwani Misri kwa nguvu na uweza
mkuu, tunajifunza kwao jinsi walivyokutana na vipingamizi ambavyo viliwafanya
wamlilie Mungu na kupigana vita. Walipigana kiroho, wakapigana kimwili. Mfano
halisi ni vita vyao na Waamaleki “Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana
na Israeli huko Refidimu. Musa akamwambia Yoshua, tuchagulie watu, ukatoke
upigane upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo
ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu. Basi Yoshua akafanya kama Musa
alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya
kile kilima. Ikawa, Musa alipoinua mkono wake, Israeli waliposhinda; na
aliposhusha mkono wake, Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa
mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri
wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake
ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake
kwa ukali wa upanga. BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe
ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa
Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu. Musa akajenga madhabahu, akaiita
jina lake Yehova-nisi; akasema, BWANA ameapa; BWANA atakuwa na vita na Amaleki
kizazi baada ya kizazi.” Kutoka
17:8-16
Wanadamu
kwa jinsi ya ubinadamu wao wanaweza kufanya jitihada zao za kiganga na kichawi
au za kawaida katika mwili wakakuwekea vipingamizi ili wewe mtu wa Mungu
usiinuke. Lakini katika nguvu za Roho mtakatifu tutashinda na zaidi ya
kushinda. Angalia mfano, Yesu Kristo walijaribu kumzuia asifufuke toka
kaburini kwa kulilinda kaburi kwa kutumia askari wenye silaha na kuweka jiwe
kubwa juu ya kaburi. “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya
Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema,
Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya
siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya
tatu; wasije wanafunzi wake wakamiba, na kuwaambia watu, amefufuka katika wafu,
na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akaawaambia, mna askari,
nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinnda kaburi salama,
kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.” Mathayo
27:62-66
Lakini
ilipofika saa ya Roho mtakatifu kudhihirisha nguvu zake, walinzi pamoja na
silaha zao walikuwa kama wafu. Maandiko yanathibitisha; “Hata sabato ilipokwisha,
ikapambazuka siku ya kwanza ya juma, mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa
pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la
nchi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja
akaliviringisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme na mavazi
yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa
kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi, kwa maana
najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa, kwani amefufuka kama
alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie
wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda galilaya;
ndiko mtakakomwona. Haya nimekwisha waambia.” Mathayo 28:1-7
Roho
Mtakatifu ni Nguvu ya Mungu na ni Pumzi ya Mungu yenye kuleta uhai tena. Kama
Kristo alihamishwa toka kwa wafu nasi tutahamishwa kiroho na kimwili kwa nguvu
za Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU UFUNGUA VIFUNGO VYA
UTASA;
Kwa
nguvu za Roho Mtakatifu na uweza wake Sara alipokea uwezo wa kuwa na
mimba alipokuwa amepita wakati wake. Milango na malango ya utasa yaliyomfunga
Sara muda wa miaka wa ishirini na mitano, kwa imani ilifunguliwa.
“Kwa
imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita
wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.” Waebrania 11:11
Hata
sasa kwa uwezo wa nguvu za Roho
Mtakatifu, wako wakristo wengi watafunguliwa ndani mwa maombi ya kufungua
milango na malango ya UTASA yasiwafunge tena maana yeye aliyeahidi ni
mwaminifu na kusema, hatakuwepo mwenye kuharibu mimba wala aliye tasa katikati
yetu.
Roho
Mtakatifu akufunike kama kivuli wewe uliyekuwa umefunikwa na roho chafu za
mashetani. Roho Mtakatifu na nguvu zake zikufunike kama kivuli, ili Vuli la
uchawi na uganga litoke kwako. Kwa nguvu za Roho mtakatifu tumevishwa uweza na
Kristo Yesu wa kufungua na kufunga na tutakachokifungua kitafunguliwa katika
Mungu aliye hai. Na tutakachokifunga kitafungwa katika Mungu aliye hai. Maana
maandiko yanasema;
“Na ufungua wa nyumba ya Daudi nitauweka
begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala
hapana atakayefungua.” Isaya 22:22
Nguvu
zake Roho mtakatifu zitakapokufunika, Utatenda makuu kwa uwezo wake. Katika
yeye Roho Mtakatifu, Wagonjwa wanapokea uponyaji, wanaosumbuliwa na nguvu za
mapepo wanawekwa huru mbali na mateso, walioshushwa chini na kudharauliwa
wanainuliwa tena. “Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na
kuponya maradhi.” Luka 9:1
Ni
lazima tuhamishwe kwa Maombi yenye Imani. Usikubali kuteswa na kugandamizwa,
Mtwike Yesu fadhaha zako, mizigo yako, taabu zako, vilio vyako naye atakuhamisha tu. Bwana atazitangua ishara zao wachawi na
waganga, Maana kwa nguvu za Roho Mtakatifu hakuna uchawi wala uganga kusimama
mbele yako tena. BWANA wa majeshi anasema; “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala
hapana uganga juu ya Israeli.” Hesabu 23:23
Ushuhuda wa dada mmoja
Dada
mmoja toka pale Kilimanjaro; alinijia akiwa na mateso ya magonjwa yaliyomkumba
alipopigwa na upepo njia panda akiwa anakwenda dukani pale kijijini kwao. Baada
ya kupigwa na upepo alianguka na kuzimia, alipozinduka alijikuta yuko hospitali
akiwa amelazwa. Baada ya miaka miwili kupita tangu apigwe na upepo wa ajabu,
ndipo alipokuja kwenye Ibada ya Maombezi ya kufungua Milango na Malango. Ndipo
nilipomwombea kwa kuziita nguvu za Roho mtakatifu zenye kung’oa kila aina
ya mapando yaliyopandikizwa kwa watu wa
Mungu. Hapa tunaona wachawi wanatumia upepo kumloga na kumwingia dada huyu.
BWANA anatuma nguvu ya Roho mtakatifu katika kanisa la kwanza kama uvumi wa
upepo. Maandiko yanathibitisha kwamba; “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste
walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa
upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.
Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja
wao.” Matendo ya Mitume 2:1-4
Upepo
wa kichawi na kiganga uliokuwa unamtesa huyu dada ulimalizwa nguvu zake na
kubatilishwa kwa Nguvu za Upepo wa Roho Mtakatifu, nikatengua kila aina ya
upepo mchafu ulio mpitia kwa jina la Yesu Kristo.
No comments:
Post a Comment