Thursday, May 2, 2013

Vitu Muhimu vya kuangalia unapojiandaa kupata mwenzi wako wa maisha.......Part IV


 
Leo tutaanza kuangalia vitu unavyotakiwa kuangalia kwa mtu unayetegemea kuwa mwenzi wako wa Maisha;

Tutaanza na Jambo kubwa muhimu ambalo likikosewa linaleta matatizo makubwa kwa wanandoa,na wengi wamekuwa wakiangalia sana vitu vya mwilini wanalisahau jambo hili,twende tujifunze;

1.      Uhusiano wake na Mungu ukoje

Kitu cha muhimu sana na utakachokipa uzito angalia uhusiano wa huyo anayetaka kuwa mwenzi wako ni uhusiano wako na Mungu ukoje? Je amempokea Yesu kama Bwana wa Maisha yake,kama ndio sio uishie hapo unaendelea mbele enhee je maisha yake ya wokovu yakoje ? Je yuko makini kiasi gani na vitu vya Mungu,maana mwingine ameokoka lakini hana umakini kabisa na Mungu na maisha yake yuko busy na mambo mengine tu ya kidunia zaidi. Mwingine unakuta anakuwa busy kanisani,anaimba kwaya,ni muhudumu lakini anafanya tu kwa interest sio kwamba anafanya kwa sababu anampenda Mungu ni hobby tu sasa mpendwa usidanganike na mtu ambaye anajionyesha yuko busy tu lazima umsome ana ushirika gani na Mungu. Hili eneo la mahusiano yake na Mungu nalo lina vipengele vichache ambavyo tutataangalia;

a.      Je ana hofu ya Mungu

Mtu mwenye hofu ya Mungu anakuwa makini sana na mambo ya Mungu,na anampa Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yake. Yaani kabla hajakwambia utajua huyu mtu anamuogopa Mungu.

Hili utaliona kwa jinsi anavyofanyia watu wengine kama washirika wenzake,wafanyakazi wenzake au wanafunzi wenzake na pia familia yake.

Mtu mwenye hofu ya Mungu anaogopa dhambi na hachukulii vitu vya Mungu kwa mazoea zoea tu. Kinawachowaponza watu wengi ni ile kuzoea wokovu,mtu anazoea wokovu na anaanza kuchanganya mambo ya kidunia anayaweka katika wokovu.

b.      Je ni Mcha Mungu

Tukiangalia Neno la Mungu katika Mithali 16: 6 “Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu”,katika neno hili tunaona umuhimu wa mtu kuwa mcha Mungu

Itamsaidia kujiepusha na maovu, Ule uchaji ambao uko ndani yake utamfanya aogope kutenda dhambi. Kwahiyo utakuwa na uhakika kwamba atakuwa ni mume au mke sahihi kwako kwasababu atakuheshimu wala hatakunyanyasa maana anao uchaji wa Mungu ndani yake,Haleluya! Kwahiyo mpendwa angalia sana huyo mpendwa kama anasema ameokoka je uchaji wake ukoje? Maana watu wengine wapo wapo tu nani rahisi kuzolewa na upepo wa Ibilisi na kufanya yale mambo ambayo Ibilisi anapenda.

c.       Je analijua neno

Uwe na uhakika kwamba huyo mwenzi wako analijua neno la Mungu na ana muda wa kulisoma na kulitafakari.

Mwingine anakuwa hajui neno kabisa au anakuwa hataki kujifunza,kwa Mkiristo kutojua neno la Mungu ni hatari sana,maana neno la Mungu ndio chakula cha rohoni sasa usipokula chakula ina maana roho itakufa kwa njaa matokeo yake kuna kuwa na ukristo wa jina tu.

Neno katika Mithali 13:13 linasema ”Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu”

Neno liko wazi kabisa kwamba mtu anayedharau neno anajiletea uharibifu, kwahiyo mpendwa ukiwa na mwenzi ambaye hana maisha ya neno la Mungu atakuwa na maisha yenye uharibifu ambayo si tofauti kama wana wa dunia,anaweza kufanya vitendo ambavyo havimpendezi Mungu maana hana neno ndani yake.

Kuwa makini sana na Mungu akusaidie akupe mwenza ambaye anatoa muda wake kusoma neno,maana atakuwa na maisha ya ushindi na hata changamoto zikija hatatikisika maana yeye ni maisha yake yamejengwa kwenye mwamba imara na sio mchanga. 

d.      Ana imani au misingi gani katika maandiko

Siku hizi kuna huduma nyingi sana  na makanisa nayo ni mengi, kwahiyo yatupasa kuwa makini maana wengine sio wake na wako kwa ajili ya kupotosha neno. Tuangalie neno la Mungu katika 1Yohana 4:1 linasema “Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, Maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni

Ukisoma neno hilo hapo juu utajua kwamba sio kila anayejifanya busy na mambo ya Mungu ana maanisha hivyo yatupasa tuchunguze kwa makini,sio tu unampata mwenzi hujui japo ameokoka anaamini nini? Unaweza ukajikuta umeingia katika dimbwi la mafundisho potofu kisa mwenzi wa maisha.Muulize Roho Mtakatifu aliye ndani yako kama huyu mtu ni kweli yuko katika mafundisho sahihi? Maana kama utakaza Roho utajikuta unapoteza ule uhalisia wa wokovu na kuwa katika njia za upotofu ambalo litakutoa kabisa katika kusudi kuu alilokuitia Mungu. Amen! Mungu akusaidie uweze kuepuka watu wa jinsi hii.
 
Tutaendelea wiki ijayo na vitu muhimu vya kuangalia kwa mtu unayetegemea awe mwezi wako.
Karibu tena na Mungu akusaidia unapoinza hii safari uimalize kama yeye alivyokusudia,Amen
 
 

No comments:

Post a Comment