Friday, November 2, 2012

UCHUNGU

UCHUNGU
 


 
Leo napenda kuzungumza juu ya Uchungu na jinsi tunavyoweza kujiondoa katika hii hali ya uchungu……..



 Waebrania 12:15
 
“Mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”


Mara nyingi katika maisha tunakunatana na vitu vingi ambavyo kwa njia moja au nyingine vinaumiza sana mioyo yetu. Unaweza kukutana na mtu akakuambia yaani moyo wangu unauma sana kutokana na jinsi Fulani alivyonifanyia. Kuna mambo mengi sana ambayo yamepelekea watu kupatwa na uchungu  mioyoni mwao,vitu hivyo vyaweza kuwa kama;

·       Kijana alikuwa amechumbiwa au amechumbia halafu ghafla mwenzake anavunja uhusiano tena mwingine anamwacha mwenzake bila taarifa anasikia tu leo harusi ya aliyekuwa mchumba wako

·       Wanandoa wameoana muda mrefu lakini bado hawajabahatika kuwa na mtoto

·       Mume au Mke kumuacha mwenzake

·       Kuondokewa na mpedwa wako kama vile baba,mama ,mtoto ,mume,mke au mtu yoyote wa karibu.(Nakumbuka nilivyoondokewa na baba yangu ghafla nilipatwa na uchungu sana)

·       Kupatwa na ugonjwa ambao hautibiki  au jambo lingine lolote ambalo linampata mtu na kumpa uchungu moyoni mwake.

·       Wewe ni kijana au dada una umri mkubwa tu hujapata mwenzi wa maisha

Kila mtu ana njia yake ya kuonyesha uchungu, wengine ndio wale utasikia wamepigana kama njia ya kulipizana kisasi,lakini sisi kwakuwa ni viumbe vipya tunatakiwa kuwa tofauti maana neno la Mungu linasema  katika Warumi 12:19 Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza asema Bwana."

Mtu mwingine akiwa na uchungu anajifungia kabisa hataki kuonana na mtu yoyote na hataki hata mawasiliano na mtu yoyote,anakuwa anajifungia tu na kulia. Lakini hii njia haitamsaidia kabisa kumaliza uchungu bali anajizidishia uchungu tena anaweza kupata matatizo mengine zaidi.

Wengine wakiwa na uchungu wanaharibu vitu eti kuvunja vunja vitu kama vile TVs,Vyombo basi hapo ndio uchungu utaachia ,jamani hayo sio mapepo kweli? Maana shetani ni muhuni sana anaweza kuja kwa njia ambayo watu wakachukulia tu ndivyo anavyokuwaga hivyo huyo,kumbe kipepo kimejificha ndani.

Mtu mwingine akiwa na uchungu anakuwa anapungua uzito sana au kunenepa kwasababu inategemea na kila mmoja anavyochulia jambo,mwingine anaweza hakawa hapendi kabisa hata kula na mwingine hata kama atakula basi mawazo yanamfanya apungue tu uzito.

Sasa wapendwa wangu hebu tutafakari kwa pamoja,sawa ni kweli kabisa jamani yule kaka au dada amekuacha mataa tena masikini sijui na nguo mlishashona au kununua,ni kweli kabisa mmekaa katika ndoa kwa miaka 10 au zaidi na bado hamjapata mtoto,ni kweli kabisa mmeondokewa na wapendwa wenu mliowapenda na kuwazoea,ni kweli kabisa umefukuzwa kazi au kuna mtu anakufanyia hila kazini ili ufukuzwe kazi au ukose haki zako fulani fulani kazini,ni kweli kabisa jamani una ugonjwa ambao umemaliza hospitali zote lakini wamekuambia hakuna tiba,ni kweli kabisa unajiona kwamba una roho ya kukataliwa hakuna mtu anayekupenda kila unachokifanya hakuna mtu anaona kinafaa au yawezekana wewe ni kijana wa umri mkubwa lakini haujapata mwenzi wa maisha,LAKINI Tuangalie neno la Mungu linasemaje basi kama umeshaumizwa na umekataa tama kabisa na kukosa tumaini napenda kukuambia ndugu yangu liko tumaini hebu tusome wote neno la Mungu kutoka Warumi 12:12 “Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima”.

Tukimtumaini Mungu tutakuwa wenye furaha daima na itatufanya tuwe na saburi katika yale tunayopitia haijalishi ukubwa wa tatizo. Unapomtumaini Mungu unapata nafasi ya kusali kama neno la Mungu lilivyosema hapo juu,ila ukikata tamaa na kutumia akili zako mwenyewe mpendwa wangu hutaweza hata kusali kabisa.

Katika kitabu cha 1Korintho 10:13 neno la Mungu linasema Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.”

Kwahiyo unapopita katika majaribu jipe moyo maana hata neno linasema kwamba majaribu ni ya kawaida kwa binadamu ila Mungu ni mwaminifu hataruhusu jaribu lililo kuzidi na atatupatia nguvu za kushinda na kutoka salama,Sema AMEN mtu wa Mungu!

Ninampenda sana Mungu na Neno lake maana kila changamoto tunazopitia katika dunia hii yeye alishatuwekea majibu yake. Jipe moyo songa mbele maana neno linasema katika kitabu cha Waebrania13:6Ndiyo maana tunathubutu kusema: "Bwana ndiye msaada wangu, sitaogopa. Binadamu atanifanya nini?"

Usikate tamaa,usiogope mruhusu Mungu leo awe msaada wako na uamini kwamba hakuna binadamu,ugonjwa,changamoto inayozidi ukuu wa Mungu,AMINA MPENDWA!

 

Ni maombi yangu, Mungu akuwezeshe kusimama na kusonga mbele na kumtegemea yeye peke yake.

 

Kutoka katika meza ya Rejoice and Rejoice by Luphurise

1 comment:

  1. DADA LUPHURISE hongera sana kwa huduma hii nzuri ambayo Mungu amekupa. kweli kwa ujumbe huu utakuwa umewafikia wengi na hope pia wengi watapata uponyaji kwani katika ulimwengu huu kuna changamoto kibao kuanzia kukataliwa, kuondokewa na uliyempenda sana, kuachwa/kuachika, kutofikia malengo yako ya kimaisha kama kazi, kuoa/kuolewa, masomo, biashara n.k (list inaweza kuwa ndefu. Nashukuru sana mwandishi wa somo hili. umenisaidia sana, utasaidia wengine pia. songa mbele

    ReplyDelete