Rev Florian Katunzi |
KARIBU katika makala haya
yanayoandaliwa na hufundishwa na
Mchungaji Florian J. Katunzi wa kanisa la EAGT City Centre, lenye makao yake
viwanja vya Mwal. Julius Kambara Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam. Wiki
hii tukijifunza kipengere
kisemacho: Maombi hurejesha nguvu ya
Uzima. Endelea….
Biblia
katika kitabu cha Yohana 11:1-46, inaonesha jinsi Yesu alivyoomba baada ya kufika
katika kaburi la rafiki yake Lazaro. Bwana Yesu aliomba hivi:
“……Akainua macho
yake juu, akasema, Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia… akalia kwa sauti kuu,
Lazaro, njoo huku nje.”
Maombi
ya Yesu Kristo yalikuwa tofauti na maombi ya Martha na Mariam dada zake
Lazaro,wao waliomba na kuamini Lazaro watamwona siku ya mwisho, Yesu Kristo
akaomba, kwa kuita kwa sauti kuu, Lazaro njoo huku nje.
Ile
nguvu ya mauti ikasikia sauti ya maombi ya Yesu Kristo, nasi tuliomwamini
Kristo tunayo mamlaka ya ki-Ungu ndani mwetu, yenye uwezo wa kugeuza mauti kuwa
uzima.
Uwezo
huu wa ki-Ungu tunakuwa nao pale tunapodumu ndani mwa maombi kwa kuwa
tunavishwa nguvu ya kuvunja mafungo yote ya mauti na kuzimu.
Ushahidi
wa kimaandiko unapatikana katika “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na
nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru.”
Luka 10:17
Mauti
inasikia sauti ya maombi, Mkristo mpendwa usipuuze maombi, Lazaro alitoka
kaburini, si kwa Yesu kusimama mbele ya kaburi alimozikwa siku nne zilizopita, bali, alipoomba, akatamka, akaita Lazaro toka
nje, Lazaro akatoka nje, aliyekuwa amekufa akatoka ni mzima.
Ndugu
zake Lazaro walisema ananuka, ameoza, lakini Yesu akasema ondoa jiwe.
Hakuangalia harufu wala kuoza kulikoletwa na nguvu ya mauti na kuzimu.
Ni
ukweli kuwa akili ya kibinadamu na hesabu za kisayansi zinaonesha kuwa mwili wa
nyama ukishakosa oxygen na kulala kaburini kwa siku nne, ni lazima uoze na
kunuka, ndugu wa Lazaro walikuwa na sababu zote za kuamini hivyo, lakini
walisahau kuwa waliyekuwa naye alikuwa
ndiye uzima na mauti haikuwa na nafasi
kwake.
Yesu
mwenyewe anasema: “….Usiogope mimi ni wakwanza na wa mwisho, na aliye hai; name nalikuwa
nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti
na kuzimu.” (Ufunuo 1:17-18).
Hata
wewe leo unaweza kuwa na tatizo kubwa
linalofanana na mwili wa Lazaro kaburini, ndugu jamaa na rafiki wanakuaona kama uliyekwisha kabisa,
unayesubiri ufufuo siku ya mwisho, lakini ndani mwa Maombi upo uzima wako, kama
vile Mtumishi wa Mungu Ayubu alivyonena baada ya mateso na maumivu mazito.
Ayubu
alisema hivi:
“Watu wa mbari yangu wamekoma, na rafiki
zangu niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu na vijakazi vyangu,
wanihesabu kuwa mgeni; mimi ni mgeni machoni pao. Namuita mtumishi wangu wala
haniitikiii ingawa namsihi kwa kinywa changu. Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa
mke wangu name ni chukizo kwa ndugu zangu.
Hata watoto wadogo hunidharau; nikiondoka,
huninena. Wasiri wangu wote wanichukia; hao niliowapanda wamenigeukia. Mfupa
wangu umegandamana na ngozi yangu na nyama yangu, nami nimeokoka na ngozi ya
meno yangu tu….. laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa
kitabuni! Yakachorwa katika mwamba wa milele, kwa kalamu ya chuma na risasi.
Lakini mimi najua ya kuwa mteteaji wangu yu hai, na yakuwa hatimaye atasimama
juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini, pasipokuwa na
mwili wangu nitamwona Mungu; nami nitamwona mimi nafsi yangu, na macho yangu
yatamtazama, wala si mwingine.Mtima wangu unazimia ndani yangu!”
Jambo la
msingi hapa ni kuwa mtetezi wako yu hai hata kama unanuka, hata kama umo kaburini, hata kama umeonekana
umekufa kiuchumi, Yesu Kristo anayo nguvu ya kufufua pale tunamwomba; ndani mwa
maombi tunapata uzima.
“Ukaniite siku ya mateso; nitakuokoa, na wewe
utanitukuza,” Zaburi 50:15.
Ndani
mwa Yesu Kristo imo nguvu ya uzima, yatupasa tukae ndani mwake pasipo kuzimia
moyo.
Mpaka
mifupa mikavu ikapokea uzima, si kwamba
Mtumishi wa Mungu Ezekieli aliomba siku moja tu, urejesho ukatokea, hapana yalikuwa ni maombi
endelevu.
BWANA ni
mwaminifu pale tunaposimama katika maombi na anatuambia:
“Nanyi mtajua ya
kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapo yafunua makaburi yenu na kuwatoa ninyi katika
makaburi yenu watu wangu. Nami nitatoa roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi …”
Mungu
wetu anataka tujue kuwa yeye ndiye
atuwezeshaye; tumwishie kwa maombi ndani mwa maombi, maana uzima wa mtu
haukufichwa katika mali alizo nazo.
Ustawi
wa mtu haukufichwa katika fedha alizonazo, bali katika roho wa Mungu aliyemo
ndani mwetu. Roho wa Mungu akiwa hai ndani mwetu; matokeo ya nje yataonekana.
Maandiko
yanaonya sana, mtu wa Mungu kuishi bila kufuata taratibu za kiroho; kwa
kutegemea upako wa mwili, lakini ndani mtu hana kitu.
“Basi, kama ni
hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili; kwa
maana mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili mwataka kufa; bali kama mkiyafisha
matendo ya mwili kwa roho Mtaishi . kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa
Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa
hamkupokea tena Roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa
wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja
na Roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam
kuteswa pamoja naye, ili tupate kutukuzwa pamoja naye. Rumi 8:12-17.
Deni
letu kwa Mungu ni kuwajibika ndani mwa maombi maana amtafutaye Mungu atamwona
na amwitaye Mungu atamwitikia, hatuwezi kumwita Mungu nje ya maombi, bali ndani
mwa maombi, hivyo inuka sasa uombe, ni wakati wa maombi.
Itaendelea…….
amen
ReplyDelete