Wednesday, May 21, 2014

Uchumba hadi Ndoa: Sababu Kumi zinazofaa kumfanya mtu aamue Kuoa au Kuolewa


Mpendwa wangu Shalom,
 
Karibu tena katika Makala haya ya Uchumba hadi Ndoa, yanayoletwa kwenu na Washauri Wenu wa Ndoa na Mahusiano.

Wiki mbili zilizopita tuliangalia sababu 10 zisizofaa kuamua kuoa au kuolewa, ambapo tulipata nafasi ya kuchambua mambo mengi na ya muhimu.


Basi leo Karibu tena tuendelee na Somo lingine, Leo tutazungumzia Sababu Kumi(10) zinazofaa kumfanya mtu aamue Kuoa au Kuolewa;


1.      Ndoa ni Mpango wa Mungu

Mungu ndiye Mwanzilishi wa Ndoa, tunasoma katika Mwanzo 2: 18 “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”

Mungu aliona si vema mtu awe peke yake na ndipo akamfanyia msaidizi(MKE) wa kufanana naye. Kwahiyo unaona kabisa Ndoa ilikuwa ni mpango wa Mungu na sio kwamba baba yetu Adamu alijiamulia tu kwa msukumo wake mwenyewe. Na hii muhimu sana kwa Wakristo kujua kwamba Mungu anatuwazia mawazo mema, yeye bila kuombwa na Adamu anaona huyu ngoja nimpatie mwezi wake ambaye anafanana naye, Mungu alijua akimpa ambaye hawafanani itakuwa kasheshe. Mungu ni Mpangaji Mzuri sana kwakweli Uzuri wake haulezeki nikiangalia jinsi amefanya mambo yake huwa namshangaa na kumsifu tu.

Katika maisha yako ya kila siku najua umekuwa na mahitaji mbalimbali ambayo unayapeleka mbele za Mungu kwa njia ya maombi, kwa mfano Kufaulu mitihani, kupata kazi, kupona magonjwa , kupata kazi nakadhalika nakadhalika, Sasa kama umemuomba Mungu akakujibu juu ya hivyo vitu vingine kwanini kwenye swala la Ndoa usimwamini Mungu hivyohivyo.

Kabla ya kupata mwezi na baada ni vizuri kuwa katika hali ya maombi ili mapenzi ya Mungu yatimizwe, ili Mungu akupe mtu yule aliyemkusudia ambaye unafanana naye. Kwasababu ukipata unayefanana nae mtaishi kwa upendo na kuchukuliana.

Kwahiyo ni ombi langu kwako ndugu yangu mpendwa kwamba Mungu akupe neema ya kukaa katika maombi katika hatua yoyoye ambayo uko, iwe hujapata mwenza , au umeshampata au uko ndani ya Ndoa.

Hiyo itakusaidia sana kuwa na maisha ambayo Mungu amekukusudia kwasababu utakuwa unatembea katika mpango wa Mungu


2.      Kuonyesha Upendo wa Mungu kwa Mwenzi wako

Mungu wetu ni Upendo na upendo wake ni wa Agape, yeye alitupenda wakati sisi tuko katika dhambi na wala hatuna chochote ambacho tumempa.

Upendo wa Mungu sio kama ambao baadhi ya watu wanao, hauna masharti, watu wengi wana upendo wa masharti ule wa Nipe Nikupe, nakupenda kwasababu ya Pesa, au nakupenda kwasababu ya najua nitapata upendeleo fulani fulani, na siku hizi imekuwa hatari sana vijana wengi wanaoa au kuolewa na watu kwasababu hao watu wana vitu fulani kama magari, nyumba, hela, au vyeo

Lakini Upendo wa Kweli ni ule wa Mungu ambao hauna masharti, tunapaswa kuingia katika Ndoa ikiwa ni njia nzuri ya kuonyesha Upendo wa Mungu kwa wenzi wetu.

Ndoa ni sehemu sahihi kabisa ya wenzi kuonyesha upendo wa Agape kwa kila mmoja,kumpenda mwenzako akiwa mzima au mgonjwa, akiwa na fedha ua hana, akiwa na cheo au asipokuwa nacho, kumuonyesha mwenzako upendo bila kusubiri kupata chochote kama Mungu na Kristo walivyotupenda kwanza.

 

3.      Kuonyesha Upendo wa Kweli kwa Mwezi wako

Ndoa ni sehemu muhimu sana ya kuonyesha upendo kwa mwezi wako, kwahiyo ni vizuri kuoa  au kuolewa kwa makusudi ya kutaka kuonyesha upendo kwa mwenzi wako

Katika Ndoa kunatakiwa kuonyesha aina tatu za Upendo;

·         Phileo ambao ni ule upendo wa Kimahaba kwa mpenzi wako, kwahiyo unapooa au kuolewa ndugu mpendwa ujue una jukumu la kuonyesha upendo wa kimahaba kwa mwenzi wako

·         Eros ni vizuri kuingia kwenye ndoa kwa shauku ya kutaka kuonyesha upendo wa kimapenzi kwa mwenzako, kuwa Tayari na furaha kwa ajili ya ile zawadi kubwa ya Tendo la Ndoa Mungu aliyoiandaa

·         Agape wanandoa pia wana jukumu la kuonyesha upendo wa Mungu kwa kila mmoja kama nilivyokwisha kuelezea hapo juu

              Kwa hiyo Upendo kwa mwenzi wako ni jambo la msingi sana nan i msukumo unaoruhusiwa kufanya maamuzi ya kuingia katika Ndoa, kwahiyo mpendwa kama hujaingia hebu jichunguze je kuna upendo , ni nini  

             Msukumo wako?


4.      Shauku ya kuazisha familia pamoja

Mungu ametupa Ndoa ni Zawadi kubwa sana ya kuanza familia pamoja, na familia sio lazima watoto maana mnaweza msijaliwe watoto, kuna familia nyingi tu hawajapata watoto na wanaishi kwa furaha

Watu wowote ambao Mungu atakupa uishi nao basi ndio familia yako, kwahiyo katika hali yoyote ambayo utajikuta uwe na watoto au usiwe nayo machoni mwa Mungu wote mna thamani, na usiingie kwenye ndoa kwa msukumo wa Mtoto mtoto tuu, kwasababu asipokuja au akichelewa utapata msongo wa mawazo na itakuwa ni mwanzo wa shetani kukuibia furaha ya Bwana ndani ya Ndoa yenu.Halleluya wapendwa

5.      Shauku ya kuwa na mwenzi utakayeshirikiana naye tendo la Ndoa kama Mungu anavyotaka

Haleluya pia kuingia kwenye ndoa kwa matarajio ya kuwa kushiriki tendo la Ndoa na mwenzi wako ni jambo zuri lakini Isiwe ndo msukumo pekee tu wa kuingia kwenye ndoa kama nilivyozungumza katika sababu kumi zisizofaa za kukufanya uingie katika ndoa.

Kama utaamua kuingia kwenye Ndoa kwa msukumo huo wa tendo la Ndoa tu , sasa mwenzako akapata matatizo ya kiafya ambayo hayatamruhusu kufanya hilo tendo, unafikiri itakuwaje si matatizo?

Hili tendo pia ni zawadi Mungu ametoa kwa wanandoa tu, kwahiyo ewe kijana mwenzangu muombe Mungu akuwezeshe ujizuie hadi utakapoingia kwenye ndoa, utakuwa huru Zaidi.

Naomba nisisitize jambo hapa, yamkini umeokoka ukiwa huko nyuma ulishafanyaga hilo tendo au ulianguka ukafanya hilo tendo, Nakusihi TUBU, na adhimia moyoni mwako kwamba unakwenda kutembea katika usafi na uweke mwili wako kuwa dhabihu mbele za Mungu kwamba Hutafanya hadi katika Ndoa, nakwambia mpendwa Mungu ni mwaminifu tena atakuheshimu na atakuvusha na Shetani atashindwa, Halleluya, ujitambue kabisa kwamba wewe ni Kuimbe Kipya na mwili wako ni Hekalu la Roho Mtakatifu usikubali watu wakuchezee chezee, Aminaaaa.

Hata akaja mkaka anatoa mapepo 100 kwa dakika 5 usidanyanyike yeye ni mwanadamu tuu, simama Imara na Mungu ndio ataona moyo wako na kukuletea yule aliyemkusudia katika maisha yako, na hayo yatakufanya uwe na Ndoa yenye Ushuhuda kwasababu ulimuheshimu Mungu, Haleluyaaaaaa….

 

Wapendwa wangu Mungu awabariki naomba tukutane tena wiki ijayo tukiendelea na sababu tano zilizobaki, Mungu aendelee kujifunua kwamba wewe unayemngoja tena mngoje kwa furaha maana Bwana anakwenda kukutokea na utamshangaa, wewe ambaye umeshapata endelea kuomba ili iwe kweli ni mapenzi yake na wewe uliekwisha kuingia endelea kumtafuta Bwana akupe hekima ya kuishi na mwenzi wako, na Baraka za Baba yetu Ibrahimu ziambatane nanyi wote, Amen!

 

Endelea kutembelea Rejoice and Rejoice Blog mambo mazuri yanakuja, Halleluyaaaaaaaaaaaaa

 

1 comment:

  1. Very nice..a great article! Stay a blessing!

    ReplyDelete