Tuesday, May 6, 2014

Uchumba hadi Ndoa: Usioe au Kuolewa kwa msukumo wa Sababu hizi kumi zisizofaa






Karibu tena katika Makala haya ya Mahusiano na Ndoa, leo Washauri wenu tuko Tayari kabisa kuwaletea somo zuri kabisa la kujiepusha kuingia katika ndoa kwasababu tu ya misukumo isiyofaa

Leo tutaanza kuongea juu ya kuolewa au kuoa kwa msukumo wa sababu tano zisizofaa, sababu tano zingine tutamalizia wiki ijayo, Karibu Sana

 

Tunaposema sababu zisizofaa ina maana kuna sababu Nzuri tu zinazofaa za kwa mtu kuamua kuoa au kuolewa sasa hizo tutaleta baada ya kumaliza hili

 

1.      Kuwa huru na ulinzi au kufuatiliwa na Wazazi

Vijana wengi wameamua kuoa au kuolewa kwasababu labda wazazi wao wamekuwa wanaingilia sana uhuru wao kwa mtazamo wao

Kama tunavyojua maana pia hata sisi tulikuwa vijana, kijana anakuwa anatamani sana kuwa huru kujipangia maisha yake labda afanye hivi na vile au arudi nyumbani usiku au saa ingine asirudi kabisa, sasa mzazi anakuwa mkali atamuuliza maswali kwanini unafanya hivi, kwanini umechelewa, kwanini unachelewa kazini, nakadhalika nakadhalika, au labda ana mahusiano mzazi anayatilia mashaka, sasa kijana mwingine anaona wazazi wanaingilia uhuru wake, Kwahiyo sasa anaamua ili kuondokana na hiyo adha hawa wazazi wananizingua sana ngoja niolewe tuone watanifuatilia huko kwa mume au nyumbani kwangu.

Sasa ni kweli utakuwa umeoa au kuolewa kama huo tu msukumo wa kuoa kwakweli ndugu yangu sio sahihi, kwasababu baada ya muda maswali na ufuatiliaji ule unaweza kuanza tena kwa mwezi wako atataka kujua ratiba zako sasa kwasababu wewe ndicho ulikimbia kwenu huoni kama hapa utakimbia tena, Hebu tafakari kabla hujaamua hiyo ni sababu kweli ya msingi ya wewe kuolewa…

 

2.      Kukimbia matatizo ya nyumbani kwenu

Kila familia ina changamoto zake, wengine uchumi unayumba, nyingine baba mlevi na mkorofi labda, au magomvi yasiyoisha, wengine kusakamwa, wengine ukaa uswahilini sana hupapendi kwakweli, sasa kwa kuona hivyo na labda wanakataa usipange unaamua kuoa au kuolewa ili uwe mbali na kero hizo za nyumbani.

Ina maana wewe huwezi kuvumilia mawimbi ndugu yangu, kama umeshindwa kuvumilia changamoto za wazazi wako hivi huyo unayemuona kwamba anakuambia anakupenda sasahivi je kweli akipata au changamoto utaweza kukaa kweli, maana leo anaweza kukosa kazi, hela ukajikuta uko katika maisha ambayo hata uliyokimbia kwa wazazi wako ni mazuri Zaidi, eenhe tuambie utakimbia tena au? Ndio maana leo tuko hapa kukusaidia na kukushauri lazima utafakari kabla hujaamua ili usije ukaamua kuingia katika ndoa kwasababu ambazo hata hazina tija, zipo sababu zenye tija tutakuja kuzifundisha.

Tafakari ndugu, mdogo na mwanangu, je kuna lingine linalokufanya uamue uchukue huo uamuzi.

 

3.      Unajiona mnyonge na hufai wala hustahili na huna sifa sasa akitokea mtu anasema anakupenda unaamua fasta

Kuna watu labda mazingira waliokulia au ufahamu walionao juu ya maisha umewafanya wawe wanyonge na kujiona hawafai, hawastahili, hawana sifa ya kuoa au kuolewa

Inaweza kuwa labda wazazi waliwalelea katika mazingira ya unyongee sana wakiwaambia kwamba hawafai, wamekuwa wakijidharau sana, wakijishusha sana

Na hii hata wanapokuwa na marafiki wanaendeleza hii tabia , kwahiyo hata mashuleni wanajulikana ni watu wasiofaa, wanyongee sanaa sana, hawana sifa na kibaya wao wenyewe wanajitambulisha hivyo

Labda mwingine anavyojiona na umbile lake anaweza kujidharau au kudharauliwa

Sasa mtu ambaye yuko katika mazingira hayo akatokea tu mtu akawambia anampenda anaweza kuamua haraka sana kwasababu labda hakuwahi kupata mtu anayemdhamini, lakini hiyo tu haitoshi kuwa sababu ya kuoa au kuolewa



 

4.      Kumonyesha mtu aliyekuacha kwamba umeoa au umeolewa

Katika maisha ya Ujana kuna mambo mengi sana, unaweza ukawa na mtu huyu ukidhani mnaweza kuja kuoana lakini ikaja ikaishia uhusiano ukavunjika

Mahusiano yanapovunjika yanaleta maumivu kwa pande zote , sasa mwingine usipokaa sawa unaweza kwa hasira na kumuonyesha huyo labda aliyekuacha kwamba na mimi naweza kuoa au kuolewa

Unamuonyesha kwamba hata wewe bado uko kwenye chati kwamba umepata mtu na huyo mtu tena anakuoa au anakubali kuolewa , ni kweli inafurahisha na utajisikia vizuri lakini hii isiwe tu ndio msukumo mkubwa wa wewe kuoa au kuolewa kwasababu kumbuka unaoa na unaolewa na mwanadamu na yeye atakuwa na madhaifu tu kama mwanadamu mwingine yeyote wewe olewa au oa tu kwasababu zinazofaa ambazo tutawaletea wiki zijazo tukimaliza hili. Usifunge ndoa kwa kujionyesha kwamba wewe ni kiboko, uko juu na hushindwi, au kwasababu unataka kumkomesha mtu.

 

5.      Kwasababu marafiki zako wameolewa

Yamkini ulikuwa na marafiki zako mmemaliza wote chuo au mnafanya nao kazi au biashara au mko nao kanisani mko rika sawa, sasa wanaoa na kuolewa na unajikuta umebaki peke yako, unaanza kupata msongo wa mawazo jamani mimi nimemkosea nini Mungu, mbona hakuna anayenikubali mimi au anayeniona mimi. Je wakati wa Bwana umefika mpendwa. Mimi kuna jambo Mungu alinifundisha ikifika majira na wakati wake kwakweli lazima litimie. Katika Mhubiri 3: 1 neno la Mungu linasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.”  Mpendwa wangu usifunge ndoa na mtu tu yeyote kwasababu tu unakimbizana na mikumbo, hapana kwasababu unaweza kujikuta unakaa katika hiyo ndoa uliyoingia kwa mwezi mmoja tu kwasababu haikuwa wakati wake, ulifanya kwasababu wenzako wamefanya. Zipo sababu nzuri tu za kuoa na kuolewa lakini sio hii mpendwa.

Kabla hujaamua kukubali kuolewa jiulize tu ukiwa peke yako na Mungu atakusaidia hivi kweli huu msukumo unaonisukuma nioe ni kweli ndio tu sababu ya kufanya haya maamuzi.

Ni muhimu kutafakari kwasababu Ndoa ni maisha, kama Mungu amekupa miaka mingine hamsini hapa duniani kumbuka utakuwa unaishi na huyo mtu je uko Tayari?

 

Halleluya mpendwa wangu, Tuonane tena wiki ijayo tukiendelea na zile sababu zizofaa zilizobakia….Barikiwa

 

Na ukiwa na kitu chochote usisite kutuandikia nenda kwenye Contacts kuna email na namba za Simu tutajibu, Aminaa

 

1 comment:

  1. Aminaa Aminaa, Mkibarikiwa na Sisi tunabarikiwa maana tunafurahi kufanya kile tulichoitiwa

    ReplyDelete