Na Mchungaji Florian Katunzi
Bwana asifiwe mtu wa Mungu, bado naendelea na mtiririko wa somo hili ambalo ninaamini litafanyika msaada kwako na hata kwa jirani yako. Pia napenda kukumbusha ya kuwa kitabu hiki kitatoka siku chache zijazo hivyo jiandae kukipokea.
Wiki jana tuliangalia utangulizi wa somo hili ambapo nilikufundisha juu
ya habari za Mfalme Nebukadreza aliyekuwa kiongozi wa dola yenye nguvu sana ya Ukaldayo
na pia alikuwa muabudu miungu. Mara
baada ya kifo chake Mungu alimuinua Mfalme Koreshi ambaye alikuwa mpakwa
mafut wa BWANA na alifanya makusudi yote ambayo Mungu aliyaweka.
Leo tutakwenda
kuangalia juu ya aina tano za funguo za kufungua malango na milango. Endelea…………
AINA TANO ZA FUNGUO ZA KUFUNGUA MALANGO NA MILANGO;
UFUNGUO WA KWANZA
1: NENO LA MUNGU
Neno ni kauli ya Mungu yenye Mamlaka, Uweza
na Nguvu za ki-Mungu zenye kuleta mageuzi ya kiroho na kimwili.
Yesu Kristo
alithibitisha yakuwa Neno la Mungu lina mamlaka na nguvu pale alipolitumia
kufungua mafungo yaliyofunga watu wa Mungu sawasawa na injili ya Luka 4:36 “Mshangao
ukawashika wote, wakasemezana wakisema, ni Neno gani hili, maana awaamuru pepo
wachafu kwa uwezo na nguvu, nao hutoka.”
Tunajifunza pia
kwa Neno vitu vyote vinavyoonekana
na visivyoonekana viliumbwa maana Mungu aliziumba mbingu na nchi kwa Neno lake.
Alisema iwe na ikawa.
“Hapo mwanzo
kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo
mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye
hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao
ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza
halikuiweza.” Yohana 1:1-5
Tukitaka
kufungua malango na milango iliyofungwambele yetu sharti kwanza tuwe na ufunguo
wa Neno la Mungu. Maana Neno ni taa na nuru ya maisha yetu. Aliye na Neno
haendi gizani kwa sababu kwa Neno la Mungu hakuna lisilowezekana.
“Kwa kuwa
hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” Luka 1:37
Neno la Mungu
kamwe halipiti hivyo tukilishika Neno kila lango na malango hakika yatafunguka.
“Mbingu
na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe” Mathayo 24:35
Neno lake
husimama katika kweli daima. Neno la Mungu huja kwetu likiwa hai, likifungulia
imani yetu.
“Ndipo BWANA
akaniambia… naliangalia neno langu, ili nilitimize”
Yeremia 1:12
UFUNGUO WA PILI
IMANI
Imani sikuzote
imekuwa ndiyo alama ya wanafunzi wa Yesu. Wanafunzi wa kwanza walijulikana kama
WAAMINI. Yesu alisema “… Yote yawezekana kwake aaminiye”
Mark 9:23
Imani
humaanisha kumtegemea Mungu kwa hali zote. Wakati Adamu alipofanya dhambi,
alijitoa katika kumtegemea Mungu na kujitegemea (ambako ni kutokuamini). Hii
ndiyo sababu Mungu ameweka kipaumbele kwenye imani. Imani ni njia ya
kuturudishia uhusiano na Mungu (kumtegemea Mungu). “Basi Imani, chanzo chake ni
kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Warumi 10:17
Tunajifunza
yakuwa pasipo Neno la Mungu hakuna imani ya ki-Mungu. Maana yake ufunguo wa
kwanza ndiyo unaotupeleka kwenye ufunguo wa pili.
Kumtegemea
Mungu ndiko kunakoitwa imani. Kwa imani unatoka kwenye kutokuweza hadi kuweza.
Kwa imani hakuna lisilowezekana.
A: IMANI NI NINI?
Imani ni tendo la utii katika kuitikia kile
Mungu alichokisema katika Neno lake.
Imani ya kweli
inaelezewa katika Utii na Kutenda kulingana na
Neno la Mungu.
“Basi imani ni
kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”
Waebrania 11:1
Hivyo pasipo
imani haiwezekani kumpendeza Mungu; kwa maana kila mtu amwendeaye Mungu lazima
aamini kwamba yeye yuko, naye huwapa thawabu wale wamtafutao sawasawa na Neno
lake. Ni lazima tumtafute Mungu kwa juhudi na kutamani kwa bidii uwepo wa neema
yake.
Imani na utii
haviwezi kutengana kama vile ambavyo kutokuamini na kutokutii kusivyoweza
kutengana. “Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake,
kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; hawakuigopa amri ya mfalme. Kwa imani
Musa alipokuwa mtu mzima akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni
afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika
dhambi kwa kitambo; akihesabiwa ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri
mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. Kwa imani akatoka Misri asiogope ghadhabu ya
mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.” Waebrania 11:23-27
B: KWELI TATU ZA IMANI
Msingi wa kuwa na imani kwa Mungu uko
katika kweli tatu muhimu:
Asili ya Mungu;
a.
Hawezi
Kubadilika.
“Kwa kuwa mimi, BWANA, sina
kigeugeu..” Malaki 3:6
b.
Hawezi
Kushindwa
“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo
yote, Na yakuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika”
Ayubu 42:2
c.
Hawezi
Kudanganywa
“Mungu si mtu, aseme uongo; wala si
mwanadamu ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?”
Hesabu 23:19
Kristo
amefanyika chanzo cha imani yetu kwa Mungu. Ukweli kuhusu kifo chake na ufufuko
hutoa msingi wa kuamini kwetu.
“Kristo Yesu,
aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi”
1Wakorintho 1:30
Ili imani
itende kazi ya kufungua malango na milango katika maisha yetu, ni lazima kutii
Neno la Mungu. Imani HUTENDA KAZI pale mtu aliyeamini anapofanya sehemu yake
kwa imani, hiyo humfanya Mungu naye kutenda sawasawa na kuamini kwa mtu.
Angalia mfano wa mwanamke aliyekuwa na msiba wa kutokwa damu muda wa miaka kumi
na miwili, aliposikia Neno la uponyaji kupitia Kristo Yesu aliamini na
kuadhimia moyoni mwake kumwendea Yesu Kristo kwa imani ili apate kufunguliwa. “Na
tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi
namiwili alikuja kwa nyuma, akagusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema
moyoni mwake, nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona
Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako
imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.” Mathayo 9:20-21
Matokeo ya
imani sikuzote mwisho wake ni ushindi kwake yeye aaminiye na kumletea utukufu
wa Mungu katika maisha yake ya kiroho na kimwili. “… kila kitu kilichozaliwa na
Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo
imani yetu” 1Yohana 5:4
Itaendelea……………………..
No comments:
Post a Comment