Tuesday, November 15, 2016

MSANII WA WIKI - FRIDA FELIX

LEO TUPO NA....
Frida Felix

Leo katika Msanii wa Wiki tuko na binti anayechipukia katika Muziki wa Injili, Frida Felix.

Tayari kuna baadhi wanamfahamu kwa kazi zake za utambulisho na wengine hata wamehudumu naye pamoja katika huduma mbalimbali.

Leo tumebahatika kupata nafasi ya kumfahamu zaidi na kujua zaidi kuhusu huduma yake ya Muziki wa Injili na kuhusu maisha yake binafsi.

Frida Felix
Rejoice Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?

Frida: Jina langu ni Frida Felix na situmii jina lolote tofauti kwenye muziki

Rejoice Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?

Frida: Ndiyo nimeokoka, na ninaabudu katika kanisa la TAG City Harvest

Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, yaani ulianzaje na wapi ulianzia?
Frida: Nilianzia Sunday School nikiwa bado mdogo. Nilianza nikiwa Songea kanisa liitwalo Redeemed Assemblies of God; nilikuwa nikiabudu hapo na kuimba kwaya ya watoto.


Rejoice Blog: Katika kuimba kwako, je, umeshatoa album yoyote?

Frida: Nimetoa single mbili mpaka sasa, albamu bado kidogo. Single ya kwanza inaitwa “Neno” na ya pili inaitwa “Watawala”

Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya hizo mbili ni upi?

Frida: Naupenda zaidi “Neno”

Rejoice Blog: Ni kwa sababu gani unaupenda wimbo huo zaidi?

Frida: Kwa sababu huu ni wimbo ambao namuomba Mungu anifundishe njia zake na aniongoze kwa Neno lake ambalo ni msingi wa maisha yangu kama mwamini.

Frida Felix
Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je, anakusaidia vizuri?

Frida: Sijaanza mambo ya usambazaji kwa kuwa sijatoa albamu. Pia kwa sasa najisimamia mwenyewe. Nilipotoa singles nilipeleka redioni na pia watu walizipata kupitia mitandao kwenye SoundCloud, Mkito na Mdundo.

Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda kufuatilia kazi zake?

Frida: Napenda sana kundi la Joyous Celebration la Afrika ya Kusini, pia Mary Mary na Tasha Cobbs.

Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?

Frida: Kuimba nyimbo za Injili kumeimarisha sana uhusiano wangu na Mungu kwa sababu najihisi karibu zaidi na Mungu ninapomwimbia. Kama mwimbaji wa nyimbo za Injili inabidi usome sana Neno la Mungu na kuomba sana.

Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya uimbaji?

Frida: Changamoto nilizokutana nazo hasa ni za kiuchumi. Kwa sababu kuingia studio nzuri na kurekodi nyimbo kunahitaji fedha, kufanya video, promo ya nyimbo pia kunahitaji fedha.

Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania?

Frida: Kwa kweli unakua siku hadi siku, na unabadilika kwa sababu kila siku Mungu anaibua waimbaji wapya na wazuri.


Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mamba ya dunia hii?

Frida: Mungu hadhihakiwi. Apandacho mtu ndicho atakachovuna!


Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?

Frida: Mimi ni Legal Officer, kitaaluma ni mwanasheria, kwa hiyo najihusisha na na mambo ya sheria ambayo ndiyo taaluma niliyoisomea

Rejoice Blog: Je, kimaisha uko wapi? Umeolewa au bado?
Frida: Bado sijaolewa na sina watoto

Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa Tanzania?

Frida: Wautafute uso wa Mungu, maana jukumu letu kubwa ni kuokoa roho za watu waliopotea kupitia huduma zetu

Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili una ujumbe gani kwao?

Frida: Waendelee kusikiliza nyimbo za Injili maana kuna uwepo wa Mungu katika nyimbo hizo.


Rejoice Blog: Ahsante sana Frida Felix kwa muda wako na kwa ushirikiano wako, Mungu akubariki na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu

Frida: Amen. Ahsante sana. 

Frida Felix
Huyo ndiye mwanamuziki wa Nyimbo za Injili Frida Felix tuliyenaye kwa siku ya leo katika segment ya "Msanii wa Wiki" ambaye kwa sasa nina imani utakuwa umemfahamu hatua moja zaidi.

Fridah pia ni mwimbaji wa kundi la Kusifu na Kuabudu la kanisani kwake, liitwalo The City Shakers.

Unaweza kutazama wimbo wake wa “Neno” YouTube hapa na “Watawalahapa

Waweza kupata pia nyimbo zake katika audio katika mitandao kwenye SoundCloud, Mkito na Mdundo

Kwa mawasiliano ya moja kwa moja na Frida Felix, mpate katika Social Networks za Instagram, Twitter, Facebook kwa @fridafelixofficial na pia waweza kumpata kwa simu namba 0712 093 696

Mungu akubariki msomaji wangu, tukutane wiki ijayo ili kumfahamu msanii mwingine wa muziki wa Injili. Ahsante

No comments:

Post a Comment