Neno la Mungu katika Luka 16:15 “ Hapo akawaambia,
Ninyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana
kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka.”
Leo nimesukumwa niongee juu ya jambo hili linalotusumbua sisi Wakirsto na jamii kwa ujumla. Imekuwa kama kawaida siku hizi watu kuishi maisha ya unafiki.
Unafiki ni hali ya kutukuwa na maisha ya ukweli kwa
kuwa na maisha ambayo hayana picha halisi ya kile kilichoko ndani ya moyo ya
mtu.
Mtu mnafiki anafanya hivyo ili kupata sifa kwa watu
wanamzunguka kama vile wachungaji,mabosi ofisini,marafiki na ndugu.
Mara nyingi lengo la mnafiki ni kuweka picha nzuri yake
kwa watu huku akihakikisha kwa njia yoyote ile wengine wanaonekana wabaya.
Sio rahisi sana kumjua mnafiki maana anaweza kujifanya
rafiki yako ili uwe wazi kwake apate nafasi ya kujua mtazamo wako ili aende
kueleza kwa watu wengine kwa njia ya tofauti ambayo inakufanya uonekane mbaya.
Kama neno linavyosema hapo juu katika Luka 16:15 Mungu
anajua mioyo ya wanafiki kwamba wanajifanya wema mbele za watu lakini hawako
hivyo.
Pia katika Mathayo 6: 1“Angalieni msifanye wema wenu
machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya hivyo, hampati
thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.”
Neno linatuasa kabisa kutojifanya kwamba ni wema mbele za watu ili hali
ndani ya mioyo yetu hatuna upendo nao,Mungu hatatupa thawabu kama tuna tabia
hiyo.
Mtu mnafiki atakuja kukuambia hivi unajua wewe ni
rafiki yangu sana yaani fulani kwakweli hakupendi kabisa,kumbe hapo anataka
wewe useme kitu juu ya huyo fulani ili yeye akirudishe kwake.
Mnafiki mara nyingine anaweza kuwa chanzo cha
uchonganishi na magomvi katika sehemu za kazi,makanisani na katika makundi
mbalimbali,inaweza ikachukua muda sana kujua ni nani anayesababisha maana
anakuwa ana picha nzuri kwa kila mmoja na anahakikisha kila mtu anamuona yeye
ni mtu mzuri sana kumbe moyoni hamaanishi kabisaa.
Unafiki umesababisha mafarakano kwa
ndoa,makanisani,kazini na katika familia pia.
Mnafiki anaweza kusababisha watu fulani wasipate haki
zao kwasababu anakuwa ametumia wema wake ambao ni fake kuhakikisha anaharibu
sifa za mwenzake labda kwa mambo aliyoanzisha yeye halafu akayageuza yaonekane
kwamba mwenzake ndio ameyafanya au kusema.
Unaweza kuchukulia unafiki kwamba si dhambi ukaona kama
vile ni kitu kidogo lakini tunajua neno la Mungu linasema dhambi zote ni sawa.
Hii tabia ya unafiki inaweza kusababisha hata kifo
mpendwa kwa mfano kama mtu akaambiwa hayo yaliyosemwa na mnafiki na halafu
akapata mshtuko unaomsababisha labda kupoteza maisha,sasa hapo yule mnafiki si
atakuwa na mkono katika kifo hicho?
Kuna watu wamepoteza ndoa,kazi,ushirika
makanisani,undugu na urafiki kwasababu tu kuna mnafiki mmoja alikwenda
kuwazunguka.
Leo nimekuja kukumbusha kwamba tujichunguze wapendwa
kama kuna hata mbegu ndogo tu ya unafiki ndani mwetu tutubu na tuache kabisa
maana sio kusudi Yesu alilotuitia hapa duniani.
Tuwe makini tusije tukajisahau tukajikuta tumeingiwa na
hii tabia ya unafiki,naomba tuombe Mungu atuwezeshe ili tuache kabisa kama
tunayo maana Mungu ni mwaminifu na anasamehe dhambi.
Kuna mpendwa mmoja alishawahi kuingia kwenye tofauti na
wakwe zake hakujua tatizo limeanzia wapi baadae ndipo alikuja kujua kuna rafiki
yake wa karibu ndio alikua chanzo alifanya unafiki wake ndio ulisababisha yote
hayo.Ilikuwa mbaya sana maana wote walikuwa ni wapendwa wazuri tu
Nimekupa huu mfano ili uone jinsi unafiki unavyoweza
kuharibu mahusiano ya watu na kufanya watu wasiishi kwa furaha.
Katika msitari wa biblia hapo juu tunaona aina nyingine
ya unafiki kutoka kwa watu ambao wanajifanya ni watumishi wa Mungu lakini kumbe
sio,hii imechukua kasi sana hapa nchini na duniani kwa ujumla. Ashukuriwe Mungu
aliyetupa Roho wake Mtakatifu ambaye ni mshauri maana ndio anaweza kutushauri
ili tusije tukaingia katika mitego yao.
Ni maombi yangu hii roho ya unafiki iondoke katika
makanisa na maisha yetu,wa kuindoa ni mimi na wewe kwa kujihadhari nayo kwa
kushauriana,kuombeana na kulijaza neno la Mungu kwa wingi katika maisha yetu.
Mungu atusaidie maana peke yetu hatutaweza kujiepusha
nahii roho ya unafiki.
No comments:
Post a Comment