Wednesday, June 19, 2013

Vitu muhimu vya kuangalia unapojiandaa kuwa na mwenzi wa maisha........Sehemu ya 7


 
Leo tunaendelea na somo letu la saba kwenye mtiririko wa Vitu muhimu vya kuangalia unapojiandaa kuwa na mwenzi wa maisha.

Tunaendelea kuangalia vitu ambavyo unatakiwa kuangalia kwa huyo anayetegemewa kuwa mwenzi wako,ili usije ukajikuta unajiingiza katika mtego ukaja kulia.

Leo tutaangalia kipengele muhimu sana cha kuangalia kwa huyo mtarajiwa wako ambacho ni;

 Je huyo mtarajiwa wako ni mkweli kwa kiasi gani;

“Mithali 12:22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake”

Kutokana na andiko hilo hapo juu tunaona kwamba Mungu wetu hapendi Uongo,mtu muongo ni chukizo kwa Bwana bali mwaminifu ni furaha ya Bwana.

Ni muhimu sana kuhakikisha kwamba mtarajiwa wako ni mkweli ikiwa na maana kwamba kila alichokuambia kuanzia historia yake ya nyuma,maisha yake ya sasa,anapofanya kazi,biashara au shule ni kweli viko hivyo.

Ngoja nikupe ushuhuda kidogo kabla sijaendelea,Kuna dada mmoja alichumbiwa yule mchumba alimpa historia ambayo kwakweli ilimsisimua yule dada kwamba ana CPA,ACCA,Masters mbili na anafanya kazi shirika moja kuubwa la kimataifa.

Kwa ninavyomjua yule dada sio kwamba alikubali hayo mahusiano kwasababu ya hivyo vitu ila alikuwa tu amempenda huyo mtumishi kama alivyo bila vitu vyake. Siku zilivyokwenda ndivyo yule mtumishi akawa anaendelea kuongeza CV yake kwamba ana kile na hiki na kwamba ana undugu na wakubwa Fulani Fulani.Yule dada aliamini kwamba anavyoambiwa ni kweli kwasababu yeye kila alichomweleza mwenzake ni kweli tupu. Sasa siku moja yule akakutana na rafiki yake ambaye alikuwa hajamuona siku nyingi,katika furaha akamwambia ana mchumba ambaye ana sifa hizo hapo juu basi yule rafiki akamfurahia mwenzake na nafikiri alitamani kumuona huyo mwenzi wa rafiki yake. Siku ikafika yule dada akakutana nao siku moja akamwambia huyu ndio mtarajiwa wangu akamwambia ndio yule uliyeniambia akasema ndio. Kumbe yule rafiki alikuwa anamjua vizuri sana yule mchumba kwamba ni tapeli tu wa mjini na hana hata kigezo kimoja na anafanya biashara ya kawaida. Ilikuwa ni aibu sana maana yule dada ilibidi afuatilie kujua na mambo mengine aliyokuwa amemwambia akagundua kwamba amedanganywa vyote.

Na hapo ndipo lilitimia andiko la Mithali 12:19 “Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.”

Mtu anaweza kusema uongo ukaonekana kama kidogo kumbe nyuma yake ana mambo kibao ambao yamejengwa ndani ya uongo,maana ukiolewa au kuoa mtu muongo ndio sasa unaanza kuishi maisha ya stress anakwambia nimeenda kazini kumbe hajaenda,anakwambia niko Ubungo kumbe yuko Posta,anakwambia hiki kumbe anafanya kile. Mtu muongo atafanya maisha ya mwenzake yawe ya taabu kubwa sana.

Katika huo ushuhuda hapo juu kilichomsaidia huyo dada ni kwamba alikuwa mtu wa maombi ndio maana Mungu aliweza kufunua hiyo tabia,angekuwa anakwenda na akili zake asingeweza kufunuliwa hayo. Ndio maana mtu yoyote akiniambia nina mchumba ninapenda kuwaambia sasa ujue kwamba umeanza safari ya mapambano usichekelee hiyo pete au hizo zawadi kaaa katika maombi ili mpango wa Mungu usimame,Haleluyaa wapendwa.

Mungu akusaidie sana,kama nilivyoshauri huko nyuma tafuta mtu wa watu utakaokuwa ukiomba nao juu ya jambo hilo na mambo mengine,iko nguvu kubwa katika Maombi maana tunasema na Baba Mungu wetu moja kwa moja.

Kama hujawahi kusoma masomo haya anzia somo la kwanza uweze kupata picha kamili kuna mambo muhimu sana nimezungumzia.

Tukutane tena wiki ijayo maana somo ni refu na sitaki kukupa vitu vingi kwa mara moja,ili uelewe kabisa na kufanyia kazi.

 

Karibu sana na Mungu wangu wa Mbinguni ambaye ni muweza akutembelee siku ya leo.

 

1 comment:

  1. Shalom mtumishi,
    kweli tunahimhitaji Mungu sana atusaidie maana mambo mengine ni vigumu kuyajua unless Mungu mwenyewe aingilie kati.

    ReplyDelete