LEO TUKO NA MCHUNGAJI JOSHUA SILOMBA
Mchungaji Joshua Silomba |
Rejoice
Blog: Labda tuanze kwa kujua majina yako kamili na ikiwa unatumia
jina tofauti kwenye kazi zako za muziki?
Joshua
Silomba: Naitwa Joshua Silomba wakati mwingine huwa naitwa Pastor
Joshua kutokana na huduma yangu ya kichungaji.
Rejoice
Blog: Je, umeokoka? Unaabudu katika kanisa gani?
Joshua
Silomba: Nimeokoka, ninaabudu kanisa la T.A.G Toangoma na pia ninatumika
kama Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo (Mchungaji wa Vijana/Sifa na Kuabudu).
Rejoice Blog: Historia yako kwa kifupi ya kuimba, yaani ulianzaje na wapi
ulianzia?
Joshua Silomba: Nakumbuka nilianza kuimba nikiwa mtoto kabisa kule nyumbani
Vwawa, Mbozi. Baba yangu alikuwa Mchungaji na familia kwa ujumla ni ya Kikristo
hivyo muda mwingi tulikuwa tukiimba nyumbani na kanisani pia hasa kwenye Sunday
School. Nilikigundua zaidi kipaji changu cha kuimba nilipoanza kusoma Shule ya
Sekondari miaka ya 2000, nilipofika kidato cha pili niliendelea zaidi kugundua uwezo
wangu wa kuongoza ibada (kuimbisha), kupiga muziki na pia kutunga nyimbo. Mwaka
2003 nilikabidhiwa rasmi jukumu la kufundisha kwaya ya kanisa la TAG Mji Mkuu nikiwa
Morogoro na tangu hapo nimeendelea kumtumikia Mungu katika maeneo yote niliyoyataja
hapo juu (Kuongoza ibada, kupiga muziki, kutunga nyimbo zangu binafsi na kwaya na
pia kufundisha kwaya na timu za kusifu na kuabudu).
Joshua akiiongoza ibada na sifa kanisani |
Rejoice Blog: Katika kuimba kwako, je, umeshatoa albumu yoyote? Majina ya
albamu?
Joshua Silomba: Nimewahi kutoa albumu mwaka 2010 iliyoitwa MUNGU WETU
HASHINDWI (audio) na kwa sasa nina albumu nyinginei itwayo JAMBO JIPYA (audio) ambayo
niliitoa rasmi tarehe 04.12.2016.
Rejoice Blog: Wimbo unaoupenda zaidi kati ya nyimbo zako ni upi?
Joshua Silomba: Kwa kweli napenda nyimbo zangu zote kwa kuwa kila wimbo umebeba
ujumbe maalumu na pia sababu maalumu ya kutungwa kwake. Hivyo, kila wimbo una
mguso wa kipekee napozisikiliza na kuziimba pia.
Rejoice Blog: Nani anasambaza na kusimamia kazi zako? Na je,
anakusaidia vizuri?
Joshua Silomba: Kwa sasa sina msambazaji wala mtu anayesimamia kazi zangu,
labda kwa hapo baadaye.
Rejoice Blog: Ni msanii gani wa muziki wa Injili anayekuvutia na unapenda
kufuatilia kazi zake?
Joshua Silomba: Kwa Tanzania ni
wengi wanaonivutia katika muziki wa Injili hususani wanaoimba nyimbo za sifa na
ibada. Kwa nje ya nchi kwa sas anapenda sana kumsikiliza na kumfuatilia William
McDowell.
Rejoice Blog: Kuna mafanikio gani umeyapata katika kuimba nyimbo za Injili?
Joshua Silomba: Mafanikio ninayoyaona kwa sasa ni kupanuliwa zaidi kwa wigo
wa kihuduma, watu wengi zaidi wanaendelea kunifahamu na kufuatilia ninachofanya
katika huduma yangu. Pia naendelea kuwafahamu na kukutana na wadau mbalimbali wa
muziki wa Injili kama vile wazalisha muziki (producers), waongoza video (video
directors) na waimbaji ambao wananipa changamoto ya kufanya kazi katika ubora na
viwango vya hali ya juu.
Rejoice Blog: Umekutana na changamoto gani katika huduma yako ya
uimbaji?
Joshua Silomba: Changamoto ni nyingi ila kwa uchache, nimepata sana
changamoto ya kifedha katika kufanikisha malengo yangu ya kihuduma hivyo kufanya
kazi zisizona viwango ninavyovitaka, ucheleweshwaji wa kazi studio au kupoteza kabisa
(nimewahi kurekodi nyimbo ambazo hadi sasa sijazipata kwa miaka zaidi ya
miwili, pia nimewahi kurekodi video ambazo sijawahi kuziona pasipo maelezo yanayojitosheleza).
Changamoto nyingine ni kutopata ushirikiano kwa waimbaji wengi waliotangulia kwenye
huduma hii ya uimbaji na mwisho, mfumo wa vyombo vya habari wa Tanzania (Redio,
TV, nk) hautii sana moyo hasa kwa waimbaji wanaoanza huduma hivyo ziko nyakati ambazo
nilikatishwa sana tamaa na mfumo huu.
Rejoice Blog: Unaonaje muziki wa Injili hapa Tanzania? Na hasa wa aina
unayoimba wewe?
Joshua Silomba: Muziki wa Injili Tanzania unazidi kukua na changamoto inazidi
kuwa kubwa hasa kwa upande wa ubora na viwango. Lakini pia kwa upande mwingine,
muziki wetu umeingiliwa sana na mamluki, hivyo kusababisha waimbaji wengi hata wasio
na shida kuonekana ni wababaishaji.
Rejoice Blog: Unatoa ujumbe gani kwa waimbaji wa nyimbo za Injili ambao
kwa njia moja ama nyingine wanajisahau na kujichanganya na mambo ya dunia hii?
Joshua Silomba: Nashauri waimbaji wanaojisahau na kujichanganya na mambo
ya kidunia wajitambue na kurejea kwenye misingi ya Neno la Mungu ambalo linatuongoza
kupita katika njia za haki na utakatifu. Zaidi wanatakiwa kutubu na kusimama kwenye
kweli ili utumishi wao usiwe bure.
Rejoice Blog: Zaidi ya kuimba ni kitu gani kingine unakifanya?
Joshua Silomba: Kama nilivyosema hapo awali, mimi ni Mchungaji Msaidizi wa
Kanisa la TAG Toangoma na nina wajibika zaidi kama Mchungaji wa Vijana na Sifa na
Kuabudu (Youth/Worship Pastor). Najishughulisha pia na kilimo, ufugaji na biashara.
Pia ni MC kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kikanisa.
Rejoice
Blog: Je, kimaisha uko wapi? Ndoa na watoto vipi?
Joshua Silomba: Ninaishi Toangoma, Dar Es Salaam. Nina mke (Bertha) na mtoto
mmoja (Doreen).
Rejoice Blog: Una ujumbe gani kwa Waimbaji wa Nyimbo za Injili hapa
Tanzania?
Joshua Silomba: Tupendane, tuwe na umoja na pia tuishi maisha halisi ambayo
yatamtukuza Mungu.
Rejoice Blog: Na kwa jamii inayoguswa na kuburudishwa na nyimbo za Injili
una ujumbe gani kwao?
Joshua Silomba: Waendelee kututia moyo na kutupa ushirikiano tunapotoa nyimbo.
Rejoice Blog: Ahsante sana Joshua Silomba kwa muda wako, Mungu akubariki
na kukuinua unavyoendelea kumtumikia kwa uaminifu
Joshua Silomba: Amina! Nawashukuru pia Rejoice Blog kwa kazi nzuri mnayoifanya
ya kuibua na kutangaza vipaji vya waimbaji wa nyimbo za Injili. Mungu awainue zaidi
ili muwafikie watu wengi.
Kupata zaidi habari za huduma yangu kwa sasa natumia Facebook, page yangu natumia
jina Joshua Silomba. Msomaji anaweza ku-like na ku-share na wengine ili waweze kujua
habari mbalimbali zinazohusu huduma yangu. Pia YouTube kwa sasa nimeweka wimbo
(audio) unaoitwa Jambo Jipya wanaweza
kuusikiliza kwa kubofya link HAPA
Mawasilianoi zaidi piga: +255717387212/+255754773512
Mwisho kabisa napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa msomaji kutoa muda
wake kufuatilia habari za muziki wa Injili kupitia Rejoice Blog.
~~~
UBARIKIWE ~~~
No comments:
Post a Comment